Manji ashtakiwa kwa kubwia ‘unga’

MWENYEKITI wa Klabu ya Yanga na mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akikabiliwa na mashitaka ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin.

Manji ambaye pia ni Diwani wa CCM katika Kata ya Mbagala Kuu, wilayani Kigamboni, alifikishwa mahakamani hapo jana saa 7:56 mchana akitokea Kituo Kikuu cha Polisi ambako aliswekwa rumande tangu Februari 9, mwaka huu.

Hata hivyo, baadaye alilazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Muhimbili.

Baada ya kupandishwa kuzimbani na kusomewa mashitaka, alipatiwa dhamana na kuachiwa huru kwa kusaini dhamana ya Sh milioni 10 huku mdhamini wake, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Charles Boniface Mkwasa akisaini kiasi hicho hicho cha fedha, na kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu.

Akisomewa mashitaka hayo na Karani Sarah Mlokozi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha, alidai kuwa mshitakiwa anashitakiwa kwa mashitaka ya kutumia dawa za kulevya kinyume na kifungu namba 17 (1) (a) cha Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya Namba Tano ya mwaka 2015.

Ashitakiwa kwa kutumia heroin Mlokozi alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kati ya Februari 6 na 9, mwaka huu, maeneo ya Upanga Sea View wilayani Ilala katika Mkoa wa Dar es Salaam, ambako alitumia dawa za kulevya aina ya heroin (diacety -morpline).

Jopo la mawakili watatu wa serikali ambao ni Wakili Mwandamizi wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi, Shadrack Kimaro na Osward Tibabyenko, walidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

Aidha, mawakili wa upande wa utetezi ukiongozwa na Alex Mgongolwa, ulidai kwa kuwa upelelezi haujakamilika na kosa la mshitakiwa linadhaminika wanaomba dhamana yenye masharti nafuu kwa kuwa Manji ana dhamana ya watu kwa Kata ya Mbagala Kuu akiwa diwani na pia ni mfanyabiashara maarufu anayeweza kujidhamini mwenyewe.

Hata hivyo, Tibabyenko akiwakilisha upande wa mashitaka alidai kuwa hawana pingamizi la dhamana kwa mshitakiwa huyo. Hakimu Mkeha alisema dhamana kwa mshitakiwa ni dhamana ya Sh milioni 10 na mdhamini mmoja mwaminifu atakayesaini dhamana hiyo.

Adhaminiwa na Mkwasa Baada ya masharti hayo, aliyekuwa Kocha Msaidizi wa timu ya soka ya Yanga na mchezaji mahiri wa zamani wa klabu hiyo , Mkwasa ambaye katika kesi hiyo alijitambulisha kama Katibu Mkuu wa Yanga na mkazi wa Tegeta Kibaoni, alimdhamini mshitakiwa huyo.

Mkwasa pia ni nahodha na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania `Taifa Stars’.

Aidha, Manji alionekana mwenye kudhoofu na baada ya kutoka mahakamani, Wakili wake Mgongolwa alisikika akisema wanampeleka hospitalini kwa kuwa afya yake haijakaa vizuri.

Manji aliondoka mahakamani hapo akiwa kwenye gari la kifahari aina ya Hummer, na kesi yake itatajwa tena Machi 16, mwaka huu.

Mashabiki mbalimbali wa klabu hiyo walifika kwa wingi kujua hatma ya mwenyekiti wao, na wengine walitokwa na machozi pale walipomuona na kumuombea dua.