Waziri aonya wanaonunua vyeti vya chanjo

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameonya wasafiri nchini kuepuka kupokea au kununua vyeti vya chanjo ya manjano bila kupata chanjo kwani kufanya hivyo si tu ni kosa la jinai, bali pia ni kuhatarisha maisha ya msafiri na watu wengine.

Aidha, amesema kuanzia Aprili mosi, mwaka huu vyeti vya zamani vya chanjo havitatambulika tena, hivyo wenye vyeti vya zamani wawasilishe vyeti hivyo kwenye vituo vya afya walikopatiwa chanjo ya homa ya manjano ili vibadilishwe.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Waziri Ummy alisema kazi hiyo ya kubadilisha vyeti vya zamani vya chanjo ya manjano ilianza tangu Januari 9, mwaka huu itadumu hadi mwishoni mwa Machi.

Alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila msafiri nchini kuepuka kupokea au kununua vyeti vya chanjo ya manjano bila kupata chanjo kwani kufanya hivyo sio tu ni kosa la jinai, bali pia kunahatarisha maisha ya msafiri na ya watu wengine.

“Ninawaomba wananchi kutoa taarifa kwenye ofisi yoyote ya Serikali iliyo karibu au vyombo vya dola endapo watabaini ofisa au mtu anatoa cheti cha njano bila chanjo hiyo kutolewa. Kitendo hiki ni kinyume na Sheria ya Afya Jamii ya Mwaka, 2009.

Hatua kali zitachukuliwa kwa mtu yeyote anayetengeneza, kuuza au kununua vyeti visivyo halali vya chanjo,” alisema waziri huyo.

Alitaja vituo vilivyoidhinishwa kubadilisha vyeti hivyo kuwa ni viwanja vya ndege ambavyo ni Uwanja wa Ndege wa Kimaitaifa wa Julius Nyerere (JNIA), Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

Vile vile bandarini ikiwemo ya Dar es Salaam, Tanga, Mwanza na Bandari ya Kigoma. Vituo vingine ni mipaka ya nchi kavu ikiwemo Horohoro, Namanga, Holili, Tarakea, Sirari, Isaka, Mutukula, Mtambaswala, Kasumulu na Tunduma pamoja na Mkoa wa Dar es Salaam katika Kituo cha Afya cha Mnazi mmoja.

Alisema wizara imefanya maboresho ya vyeti vya chanjo ya homa ya manjano vilizinduliwa Novemba 24, mwaka jana lengo likiwa ni kudhibiti utolewaji holela wa vyeti hivyo.

Wananchi wenye vyeti hivyo vya chanjo ya homa ya manjano vya zamani ambao walipatiwa chanjo na kupewa vyeti halali wametakiwa kuviwasilisha na hati ya kusafiri kwenye vituo vya afya walipopatiwa vyeti ambako kumbukumbu za chanjo zipo ili wapatiwe cheti kipya.

“Gharama za kubadilisha vyeti vya chanjo ya homa ya manjano ni shilingi elfu tano za Kitanzania kwa raia wa Tanzania na raia wa kigeni ni Dola 10 za Kimarekani kwa wageni waliopatiwa chanjo Tanzania,” alisema.

Chanjo hiyo hutolewa kwa wasafiri wanakwenda kwenye nchi 30 za Bara la Afrika ambazo ni Angola, Benin, Burkina Faso, Burundi, Cameron, Afrika ya Kati, Chad, Congo, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Equatorial Guinea, Ethiopia, Gabon, Gambia, Ghana, Guinea, Guinea Bissau, Kenya, Liberia, Mali, Mauritania, Niger, Nigeria, Rwanda, Senegal, Sierra Leone, Sudan Kusini, Sudan, Togo na Uganda.

Mbali ya hizo, nyingine ni nchi 13 kutoka Bara la Amerika ya Kusini ambazo ni Argentina, Bolivia, Brazil, Colombia, Ecuador, French Guiana, Guyana, Panama, Paraguay, Peru, Suriname, Trinidad na Venezuela kama zilivyoainishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa na hatari ya maambukizi ya ugonjwa wa homa ya manjano, hivyo wasafiri wanaokwenda nchi hizo wahakikishe wanachanja chanjo hiyo siku 10 kabla ya kusafiri na kisha kupewa cheti cha kuthibitisha kupata chanjo hiyo.