Tamwa, Polisi waokoa binti wa umri mdogo kuozeshwa

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga wamezima jaribio la kutolewa posa (kifunga uchumba) mtoto mwenye umri wa miaka 13 mkazi wa Kata ya Maweni jijini Tanga.

Binti huyo alikuwa ni mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Ukonga iliyopo Dar es Salaam ambaye mwaka jana mama yake mzazi aitwaye Sani Godwin alimwondoa kwa lazima shuleni pasipo kufanya taratibu za uhamisho kwa madai ya kwenda kuishi naye jijini Tanga.

Akithibitisha tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba alisema Februari 9, mwaka huu askari wa Dawati la Jinsia katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Chumbageni walipokea taarifa kutoka Tamwa kuhusu maandalizi ya ndoa ya mtoto huyo na hivyo kulazimika kuzifanyia kazi kwa haraka.

“Baada ya kupata hizo taarifa na kuanza kuwasiliana kwa simu na msiri wetu pamoja na viongozi wa Serikali ya Kata ya Maweni walituthibitishia kwamba ipo mikakati ya kumwozesha mtoto huyo ambaye anaishi kitongoji cha Jaributena kilichopo Mtaa wa Kichangani, kwa hiyo tulivamia nyumbani, lakini hatukukuta dalili zozote za uwepo wa harusi,” alisema Kamanda Wakulyamba na kuongeza:

“Tulifanikiwa kumkamata mtoto, mama pamoja na baba mlezi wa mtoto huyo ambao katika mahojiano, mtoto alikiri kwamba familia inaendeleza mpango wa ndoa yake na kwamba Februari 12, mwaka huu ambayo ilikuwa ni siku ya Jumamosi ndio tarehe rasmi iliyokuwa imepangwa ya posa kukabidhiwa hapo nyumbani kutoka kwa kijana mmoja (jina limehifadhiwa kwa uchunguzi) ambaye anafanya kazi ya kuchunga ng’ombe huko huko Jaributena,” alifafanua.

Inadaiwa mtoto huyo aliwaeleza askari kwamba sababu ya yeye kukubaliana na mkakati wa mama yake huyo ni kutokana na mateso aliyopata akiwa nyumbani kwa mama yake mkubwa huko Ukonga pamoja na ushauri wa mama yake baada ya kumwona kwamba shuleni hana uwezo wa kufanya vizuri darasani, hivyo kitendo chake cha kuendelea na shule kitasababisha hasara kwa familia.

Kamanda Wakulyamba alisema katika mahojiano na mama wa mtoto huyo, alidai alimchukua mtoto huyo kutoka Shule ya Msingi Ukonga ambako alikuwa akilelewa na mama yake mkubwa na alifikia uamuzi wa kumwozesha kwa mchunga ng’ombe kwa sababu hana uwezo wa kumpatia mahitaji ya msingi.