RC akaribisha Jukwaa la Biashara Mwanza

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema ushirikiano katika kuibua fursa za kibiashara kuipitia Jukwaa la Biashara linaloandaliwa na TSN kwa ushirikiano na uongozi wa mikoa nchini ni wazo zuri na kutaka liandaliwe kwa haraka katika mkoa wake.

Mkuu huyo wa mkoa alisema hayo wakati uongozi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali ukiongozwa na Mhariri Mtendaji, Dk Jim Yonazi ulipomtembelea ofisini kwake jana, kuzungumzia ushirikiano huo.

Mhariri Mtendaji aliyeongozana na Meneja wa Mauzo na Masoko, Januarius Maganga na Patrice Simbachawene ambaye ni mwakilishi wa TSN Kanda ya Ziwa alimueleza, mkuu wa mkoa namna na faida zinazopatikana kwa mikoa kukaribisha majukwaa ya namna hiyo.

Mongella amefurahia mafanikio yaliyopatikana katika Jukwaa la fursa za Biashara lililoandaliwa na kufanyika mkoani Simiyu, Jumatatu wiki hii na kuhudhuriwa na wawekezaji, wafanyabiashara, na wajasiriamali zaidi ya 160.

Aidha, aliipongeza TSN kwa namna ambavyo inasaidia kuibua fursa zilizopo mikoani ili jamii na wawekezaji mbalimbali wazifahamu, na kuahidi kushirikiana na TSN kuandaa Jukwaa la Fursa za Biashara, Aprili mwaka huu.

Mongella alisema jukwaa hilo litatumika kwa manufaa ya Mkoa wa Mwanza na pia kama utangulizi wa mkutano mkubwa wa wawekezaji utakaofanyika mwakani.

Alihimiza kuongeza na kuboresha ushirikiano kati ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali na wadau mbalimbali hasa walioko mikoani.