18Juni2013

 

Padri akimbia majambazi, aangukia kwa wengine 10

PAROKO wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Martha, Mikocheni, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Audax Kaasa ameumia visigino baada ya kuruka ghorofani katika harakati za kuokoa maisha yake, alipovamiwa na majambazikanisani hapo.

 

Padri huyo alijeruhiwa miguu aliporuka kutoka ghorofa ya kwanza ya nyumba wanamolala kanisani hapo wiki iliyopita, akinusuru maisha yake ambapo alitua chini, na kufikia mikononi mwa majambazi wengine wasiopungua 10 na kumdhibiti huku wizi ukiendelea ndani.

Kwa mujibu wa habari kutoka Polisi Kinondoni, tukio hilo la ujambazi kanisani hapo lilitokea usiku wa kuamkia Alhamisi wiki iliyopita. Majambazi hao waliiba zaidi ya Sh 900,000 na gari aina ya Toyota Escudo namba T 260 AJK na kulitelekeza Sinza Kwa-Mtogole.

Habari zilizopatikana juzi kutoka kwa baadhi ya waumini wa Parokia hiyo na kuthibitishwa na Katibu wa Jimbo, Padri Joseph Masenge zilieleza kuwa baadhi ya waumini wenye mapenzi mema walichanga fedha ili Padri Kaasa apelekwe India kwa matibabu zaidi na ameondoka.

“Tuliona pamoja na juhudi za Jimbo letu kumpa tiba nzuri hospitali za hapa nyumbani ikiwamo ya Muhimbili, tulifikia mwafaka, tuchange ili akatibiwe India na tumepata fedha za kutosha,” alisema muumini ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini wala hakuwa tayari kutaja kiasi cha fedha zaidi ya kusema zilitosha.

Padri Masenge alipoulizwa kwa simu, alithibitisha na kufafanua kuwa hakuna waumini wanaozuiwa kufanya hivyo, kwa kuwa uongozi wa Parokia unajitegemea na kuongeza kuwa matibabu yake yanatarajiwa kuchukua wiki mbili.

“Ni kweli waumini wamempeleka India, ameondoka leo (juzi) saa saba mchana, Jimbo linatambua safari hiyo,” alisema na alipotakiwa kufafanua kama anakwenda kufanyiwa upasuaji na gharama za tiba hiyo, alisema hatua hiyo itafahamika baada ya madaktari kumwona.

Hakupenda kuzungumzia gharama. Hata hivyo, taarifa za awali kutoka kwa waumini wa Mikocheni waliozungumza na gazeti hili, zilidai kuwa Padri Kaasa aliumia zaidi visigino vya miguu na kwamba hawezi kutembea bila msaada wa magongo, hivyo anaweza kufanyiwa upasuaji ikilazimika.

Siku ya tukio, Padri Kaasa akiwa na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kibiti, Padri James Haule aliyefika kanisani hapo kumsaidia huduma za kiroho, walivamiwa na majambazi usiku na kuibiwa Sh 500,000 katika gari na fedha zingine zilizokuwa ndani ya nyumba zinazokadiriwa kuwa zaidi ya Sh 460,000.

Polisi ilieleza kuwa Padri Kaasa ndiye alikuwa wa kwanza kuhisi kuvamiwa na alitoka chumbani na kuruka ghorofani kunusuru maisha, lakini chini aliangukia mikononi mwa majambazi wengine wasiopungua 10 waliomdhibiti.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, John Mtalimbo, aliliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki kuwa majambazi hao ingawa walipora bunduki walinzi watatu wa Kampuni ya Ulinzi ya Murt Lion inayolinda Kanisa, waliitumia silaha hiyo kufanikisha wizi bila kumdhuru mtu na waliitelekeza nje ya ukuta wa Kanisa walipokuwa wakitoka.

“Walipofika waliwafunga kamba walinzi watatu wa Murt Lion na kuwanyang’anya silaha aliyokuwa nayo mmoja, wakaingia ndani, Padri mmoja akaruka ghorofani kujinusuru, huyu ndiye aliyeumia kwa kuruka, lakini si kwa kupigwa na majambazi,” alisema Mtalimbo na kuongeza: “Pamoja na fedha, waliiba simu nne za mapadri hao, walipomaliza, walichukua gari la parokia Toyota Escudo na kuondoka nalo, ilikuwa saa nane hivi usiku, ilipofika saa 1.30 asubuhi Alhamisi, tulikuta gari limetelekezwa Sinza Kwa -Mtogole, likiwa zima na funguo zake, tulilikabidhi kwa wahusika wa Kanisa baada ya kulikagua”.

Mtalimbo alisema baada ya kuchukua maelezo ya walinzi na mapadri hao, upelelezi wa suala hilo unaendelea na wapo katika hatua nzuri ambayo hawezi kuiweka hadharani kwa kuwa itaharibu upelelezi.