22Mei2013

 

Uamsho waibukia Dar es Salaam

JUMUIYA ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar ambayo jana iliahidi kufanya mihadhara katika Viwanja vya Lumumba mjini Zanzibar, ilishindwa kufanya hivyo.

 

Badala yake, iliibukia katika mkutano wa Waislamu kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, ambako ilijitetea na kujitenga na tuhuma za kuhusika katika machafuko yaliyotokea hivi karibuni visiwani.

Vikosi vya polisi vikiwa na magari ya kutoa maji yenye kuwasha vilisambazwa katika Uwanja wa Lumumba tangu mchana kwa lengo la kudhibiti vitendo vya aina yoyote, ikiwamo kufanya mihadhara.

Hata hivyo, kikundi hicho kilifanya mkutano katika msikiti wa Mbuyuni Malindi uliohutubiwa na Farid Hadi Ahmed ambaye ni kiongozi wa Uamsho.

Katika mkutano wa Diamond Jubilee, jumuiya hiyo ya Uamsho pamoja na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, zimetaka masuala ya Mahakama ya Kadhi, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC) na kuundwa kwa vyama vya kidini nchini, yaingizwe rasmi kwenye Katiba mpya.

Tume huru

Akizungumza katika mkutano huo, Shehe Abdallah Said Ally kutoka Jumuiya ya Uamsho Zanzibar, aliitaka Serikali kuchukua hatua haraka na kuunda tume huru itakayochunguza machafuko ya Zanzibar yaliyohusisha kuchomwa kwa makanisa na kuwaanika wale wote waliohusika na matukio hayo.

“Naomba niweke wazi kuwa machafuko ya Zanzibar, Jumuiya ya Uamsho haihusiki nayo wala suala zima la Uislamu au Muungano. Suala hili limepotoshwa vibaya na vyombo vya habari kwa kuwa ukweli ni kwamba limeanzishwa na Polisi wa Zanzibar,” alidai Shehe Ally.

Alidai machafuko hayo yalianza baada ya kukamatwa kwa Shehe maarufu Zanzibar ambaye hata hivyo hakumtaja jina, akidai alikamatwa bila hatia.

Kwa mujibu wa madai ya Shehe Ally, baada ya kukamatwa kwa Shehe huyo, wananchi wengi wa Zanzibar walichukizwa na kuamua kufuatilia suala hilo Polisi, hali ambayo kutokana na wingi wao, baadaye ilitafsiriwa kuwa vurugu na ndipo walipoanza kutawanywa na mabomu na virungu.

Aliendelea kudai kuwa hata wakati wa mkutano wa hadhara wa jumuiya hiyo, mmoja wa washiriki aliamua kwa vitendo kuzunguka Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya kuonesha uhuru wake visiwani humo na kufuatwa na washiriki wengi wa mkutano huo na kuonekana kama maandamano.

Alisema kitendo cha kusingiziwa Waislamu na Jumuiya hiyo ni njama ya kuzuia wananchi wa Zanzibar wasidai kura za maoni kuhusu Muungano ambazo Jumuiya hiyo na Jumuiya nyingine za Kiislam zilishaanza kuiomba Serikali ya Zanzibar ifanye hivyo.

“Ni jambo la kawaida kwa Polisi Zanzibar kuwafanyia udhalilishaji mashehe, hivyo kitendo cha Waislamu kujikusanya kituoni ilikuwa ni ishara ya kusema sasa basi ndio maana tunasisitiza kuundwa kwa tume huru kuchunguza nani hasa alihusika na vurugu hizi,” alidai Shehe Ally.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Kiislamu Tanzania, Shehe Shaban Mapeyo akizungumzia msimamo wa Waislamu wa Bara kuhusu sakata hilo la Zanzibar, aliunga mkono Jumuiya hiyo ya Uamsho, akidai mara zote machafuko yanayotokea visiwani humo, mzigo mzito huangushiwa Waislamu.

Nacte wajiwa juu

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu nchini, Shehe Ponda Issa Ponda, aliwataka Waislamu nchini wajiandae na maandamano makubwa yatakayofanyika Ijumaa wiki hii.

Alidai kuwa maandamano hayo ni ya kushinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Joyce Ndalichako, wajiuzulu kwa kushindwa kuzuia hujuma za kielimu dhidi ya wanafunzi wa Kiislamu.

Pamoja na mambo mengine, Shehe Ponda alidai maandamano hayo yatagusa masuala ya sensa ambapo wanaitaka Ofisi ya Takwimu ya Taifa kufanyia kazi matakwa ya Waislamu ya kuingizwa kipengele cha dini ili ipatikane idadi halisi ya Waislamu nchini, vinginevyo Waislamu wote hawatashiriki Sensa hiyo.

Awali akiwasilisha taarifa ya hujuma za wanafunzi wa Kiislamu nchini, Shehe Ramadhan Saze, alidai katika mtihani wa kidato cha sita takribani shule nane za Maduo, Mwanakwerekwe, Ridhwaa, Ubungo, Nyasaka, Kunduchi, Emannuel na Kirinjiko wanafunzi walifelishwa makusudi ilhali walikuwa wamefaulu.

Alitaka Serikali iunde tume maalumu kuchunguza tukio hilo ambalo baada ya kuingiliwa kati na Waislamu, matokeo ya wanafunzi hayo yalibainika kuwa mazuri.

Mwinyi anena

Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi alisema vurugu zinazohatarisha amani zinaonesha kwamba kuna watu wamevimbiwa na amani iliyopo sasa visiwani.

“Wazanzibari wako macho na hawajalala na wala hawana muda wa kuamshwa… hii ni dalili kwamba miongoni mwetu watu wamevimbiwa na amani iliyopo,” alisema Mzee Mwinyi jana akiwa Manzese Kiboje katika Jimbo la Uzini.

Askofu ahofia udini Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) mkoani Arusha, Thomas Laizer amesema suala la kuchoma moto makanisa Zanzibar si suala la Muungano, kwani lina udini.

Alidai anazo taarifa za kutosha na za uhakika kuwa kwa sasa kuna vijana zaidi ya 300 wa Kiislamu eneo la Unga Ltd katika msikiti mmoja wakifanya mazoezi ya kareti tayari kujiandaa kufanya uhalifu katika makanisa.

Imeandikwa na Shadrack Sagati, Halima Mlacha Dar es Salaam, John Mhala, Arusha na Khatib Suleiman, Zanzibar