20Juni2013

 

Wabunge Tabora wachachamaa bungeni

MBUNGE wa Tabora Mjini, Aden Rage (CCM) na Dk Hamis Kigwangwala wa Nzega (CCM), wamesema Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge sio mkweli na anawapiga changa la macho wananchi wa Mkoa wa Tabora kutokana na ujenzi wa barabara unaofanywa mkoani humo kusuasua.

 

Rage ndiye alikuwa wa kwanza kumwandama Lwenge kuwa amedanganywa kuhusu ujenzi wa barabara hizo ambao umekwama kutokana na wakandarasi kutolipwa fedha zao na Serikali.

Rage alitoa kauli hiyo baada ya Lwenge kujibu swali lake la msingi lililohoji kusuasua kwa ujenzi wa baraza za Tabora na Nzega, Tabora kwenda Manyoni na Tabora kwenda Urambo.

Lwenge akitoa majibu yake, alisema ujenzi wa barabara hizo kwa sasa unaendelea vizuri kutokana na wizara yake kuwalipa makandarasi wanaojenga barabara hizo. Katika majibu yake, Lwenge alisema ujenzi wa barabara ya kutoka Tabora kwenda Nzega yenye urefu wa kilometa 114.9 na Tabora kwenda Urambo wa kilometa 94 na ule wa kutoka Tabora kwenda Manyoni wa kilometa 260 unaendelea kufanywa chini ya mikataba iliyopo.

Alisema hadi sasa makandarasi na wahandisi washauri wanaojenga barabara hizo wameshalipwa Sh bilioni 64.9 hivyo hawana sababu nyingine ya kuchelewesha ujenzi wa barabara husika.

Baada ya majibu hayo ndipo Rage aliposimama na kusema; “Waziri amedanganywa kwani hadi jana hakuna malipo ya makandarasi yaliyofanywa na wizara yake.” Rage alisema hata Kamati ya Bunge ya Miundombinu hivi karibuni ilifanya ziara kwenye barabara hizo na kubaini wakandarasi wamesimama kujenga kutokana na kutolipwa fedha na ni asilimia kidogo tu ya ujenzi imeanza kukamilishwa.

Mbunge huyo alisema hali hiyo imesababisha wananchi wa Tabora kuendelea kuonewa hasa linapofika suala la kujenga miundombinu ya uhakika, jambo ambalo hata hivyo Spika wa Bunge, Anne Makinda alimweleza kuwa suala la wananchi wa Tabora kuonewa sio mahali pake kwani kipindi hicho ni cha maswali.

Hoja hiyo ya Rage iliungwa mkono na Dk Kigwangala aliyesimama na kusema; “majibu ya Naibu Waziri ni changa la macho na ahadi hewa kwa wananchi wa Mkoa wa Tabora”. Dk Kigwangala alisema ujenzi wa barabara hizo ambao awali ulipangwa ukamilike ndani ya miaka miwili, hadi sasa ni mwaka mmoja na nusu ujenzi huo hata robo haujafika na akahoji wananchi wa Tabora wataiamini vipi Serikali kuhusu ujenzi wa barabara hizo.

Kabla ya Lwenge kusimama na kujibu swali la mbunge huyo, Spika Makinda alimtaka Mbunge huyo kuondoa neno changa la macho ili apatiwe majibu na Serikali na mbunge huyo alikubali kufanya hivyo.

Lwenge katika majibu yake aliendelea kuwataka wananchi wa Tabora waiamini Serikali ya CCM kwani ahadi yake ya kujenga barabara hizo itakamilika na fedha zimeshapatikana za kuanza kuwalipa makandarasi hao.

Lakini alikiri kusuasua kwa ujenzi wa barabara hizo kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na kuchelewa kupatikana kwa fedha za kuwalipa makandarasi wanaojenga barabara hizo yakiwemo malipo ya awali na madai ya kazi walizofanya.