25Mei2013

 

Mwakilishi atishia kuzuia bajeti ya Maji

 MWAKILISHI wa Magomeni, Salmin Awadh (CCM) ametishia kuzuia Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati kwa sababu mradi wa kuwapatia wananchi maji safi na salama wa vijiji vya Sogea na Kwahani, haujatekelezwa.

 

Awadh alisema hayo wakati alipouliza swali kuhusu tatizo la maji safi na salama kwa wananchi wa maeneo ya Kwahani pamoja na Sogea.

Aliilaumu Mamlaka ya Majisafi na Salama (ZAWA) kwa kupuuza nguvu za wananchi waliojitolea kutekeleza mradi huo pamoja na nguvu za washirika wa maendeleo.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati, Ramadhan Abdalla Shaaban alisema Serikali haijautelekeza mradi huo wala kudharau nguvu za wananchi waliojitolea kutekeleza mradi huo.

Alisema tatizo kubwa lililojitokeza ni kuzidiwa nguvu za nishati ya umeme za kusukuma maji katika eneo hilo, ambalo linatokana na kuwepo kwa matumizi makubwa ya umeme kutoka kwa wananchi.

“Napenda kumjulisha Mwakilishi wa Magomeni kwamba Serikali haijautelekeza mradi ule...kilichojitokeza ni kwamba eneo lile kuna nguvu za umeme ndogo ya kusukuma maji kwenda kwa wananchi,” alisema Shaaban.

Alisema tatizo lililopo kwa sasa linafahamika na taasisi zilizopo ikiwemo Zawa na ipo katika juhudi ya kulipatia ufumbuzi kwa lengo la kuona wananchi wanapata maji safi na salama.

 Shaaban alikiri na kusema mradi huo umefanikishwa kwa kiasi kikubwa na nguvu za wananchi wa maeneo ya Sogea pamoja na Kwahani ambao walijitolea kujenga tangi la maji kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo.