Magufuli atakiwa mahakamani
- Imeandikwa tarehe 13 Juni 2012
- By Lucas Raphael, Nzega
- Imesomwa mara: 545
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Tabora, imemtumia hati ya kuitwa mahakamani Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli afike Juni 19 kutoa ushahidi katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa ubunge yaliyompatia ushindi Mbunge wa Igunga, (CCM), Dk Dalaly Kafumu.
Shauri hilo lilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye dhidi ya Dk Kafumu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Msimamizi wa Uchaguzi.
Awali Wakili wa Dk Kafumu, Kayaga Kamaliza aliiomba mahakama hiyo itoe hati ya kumuita Waziri Magufuli afike mahakamani hapo kupitia Ofisi za Bunge Dodoma baada ya jana waziri huyo kushindwa kutokea kwa ajili ya kutoa ushahidi.
Magufuli ni mmoja wa mashahidi muhimu wanaotarajiwa kutoa ushahidi wa upande wa mdaiwa.
Anadaiwa kutoa ahadi za ujenzi wa daraja la Mbuntu ambalo ni moja ya changamoto jimboni humo.


