19Juni2013

 

Leo ni siku ya bajeti

NCHI za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania, leo zinasoma Bajeti zao kwa mwaka wa fedha 2012/2013, huku masikio ya Watanzania wengi wakitaka kufahamu jinsi Serikali yao ilivyojipanga kuchukua hatua za kukabili hali ngumu ya maisha.

 

Dk William Mgimwa ambaye ni takribani mwezi mmoja na ushee sasa anaongoza Wizara ya Fedha baada ya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete, anatarajiwa kuwasilisha hotuba ya Bajeti itakapofika saa 10 jioni leo bungeni mjini hapa.

Mchumi huyo na mfanyakazi wa zamani wa benki nchini, anatarajiwa kusoma hotuba itakayobeba thamani ya Sh trilioni 15 ambazo Serikali ya Rais Kikwete imepanga kuzitumia katika mwaka huu wa fedha utakaoanza Julai mosi na kukamilisha Juni 30, mwakani.

Mapema mwezi huu, Dk Mgimwa aliiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi kwamba fedha hizo za Serikali zinatarajiwa kutumika kwa kuainisha vipaumbele saba muhimu kukamilisha bajeti hiyo ambayo itachukua nafasi ya bajeti inayomalizika ya Sh trilioni 13.

Alivitaja kuwa cha kwanza ni miundombinu ambayo ina vipengele vinne vya umeme wa uhakika, usafirishaji na uchukuzi, maji safi na salama pamoja na mawasiliano. Vipaumbele vingine ni kilimo, maendeleo ya viwanda, rasilimaliwatu, utalii, biashara za ndani na nje na huduma za kifedha. Kwa vipaumbele hivyo, Watanzania watakuwa wanasubiri kwa hamu kuona mchanganuo wake na jinsi Serikali ilivyojipanga katika mwaka huo wa fedha kukabiliana na matatizo kadhaa nchini, kubwa ikiwa ni kupanda kwa gharama za maisha kutokana na bei kubwa ya chakula na nishati.

Mfumuko wa bei ambao ndiyo umesababisha matatizo makubwa yanayowagusa Watanzania kwa sasa umefikia asilimia 18 na inatarajiwa Serikali itakuja na hatua kadhaa itakazochukua ili hali za maisha za watu wake ziwe bora na kuwapunguzia mzigo mkubwa wa kubeba gharama hizo.

Bei ya nishati kwa sasa ni kubwa, eneo jingine ambalo limesababisha ugumu wa maisha, huku pia kukiwa na malalamiko kutoka kwa wafanyakazi wa Serikali na wale wa sekta binafsi, wakitaka kuboreshwa kwa hali zao za maisha kwa kupandishiwa mishahara na maslahi kwa ujumla.

Alipohutubia Taifa katika kilele cha Sikukuu ya Wafanyakazi, Mei Mosi, mwaka huu mkoani Tanga, Rais Kikwete aliahidi kuwa Serikali yake itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma; hivyo leo watumishi hao wanasubiri kumsikia Dk Mgimwa akieleza jambo kuhusu hilo.

Kabla ya kuwasilisha Hotuba ya Bajeti, asubuhi leo, Dk. Mgimwa atawasilisha bungeni taarifa ya mipango ya maendeleo kwa mwaka ujao wa fedha 2012/2013.