Mkulo abanwa bungeni
- Imeandikwa tarehe 14 Juni 2012
- By Shadrack Sagati, Dodoma
- Imesomwa mara: 1418
ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo amezidi kuandamwa bungeni na safari hii ametakiwa kuthibitisha madai aliyowahi kuyatoa kwa Kamati ya Mashirika ya Umma (POAC), kuwa ilikuwa imehongwa na Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC).
Mbunge wa Mwibara Kangi Lugora (CCM) ndiye aliibua hoja hiyo jana baada ya kuomba mwongozo wa Spika na kulikumbusha Bunge kuwa Mkulo wakati huo akiwa Waziri wa Fedha, aliwahi kutoa madai mazito ya rushwa dhidi ya wajumbe wa Kamati hiyo.
Mbunge huyo katika mwongozo wake huo, aliomba Mkulo ambaye alitoa madai hayo yaliyomfanya Mwenyekiti wa POAC, Kabwe Zitto kuweka rehani ubunge wake kuwa ikibainika kuwa Kamati yake imehongwa, yeye angejiuzulu ubunge hakuwahi kufuta kauli hiyo.
Lugora alisema baada ya waziri huyo kutoa kauli hiyo, alidai bungeni kuwa angemwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuchunguza suala hilo na hadi sasa umma bado unaamini kuwa wajumbe wa Kamati hiyo walipewa rushwa na CHC.
Mkulo katika madai yake kwa mujibu wa mbunge huyo, alieleza kuwa wabunge hao walipewa rushwa na CHC ili walitetee shirika hilo lisifutwe. “Mkulo alidai tumehongwa ili tulitetee shirika hilo kwa hisia kali kama tulivyoona wakati ule.
“Mpaka leo hii kumbukumbu za Bunge zinaonesha tuhuma hizo kuwa sisi tulihongwa milioni 60 hazijawahi kufutwa, kwa kuwa leo Mkulo yuko hapa naomba mwongozo wako afute kauli yake au aje hapa na ushahidi kuwa sisi tulihongwa,” alisema Lugora.
Naibu Spika Job Ndugai ambaye jana ndiye alikuwa anaongoza kipindi cha maswali na majibu, alisema, “Nimepokea mwongozo huo na tutautolea mwongozo baadaye.”
Wakati Mkulo alipokuwa Waziri wa Fedha alijikuta anaingia katika mvutano na POAC pale alipowasilisha azimio la Serikali la kutaka kuifuta CHC kwa maelezo kuwa kwa sasa haina kazi na akataka kazi wanazofanya kwa sasa zisimamiwe na Msajili wa Hazina.
Azimio hilo la Serikali lilipingwa na Zitto pamoja na wajumbe wengine wa POAC akiwemo Lugora ambaye ndiye alitoboa namna ambavyo viongozi wa Wizara ya Fedha wanataka kuliua shirika hilo ili waendelee kutafuna mali za Serikali.


