19Juni2013

 

Bajeti yaweka misingi kwa Dira ya Taifa 2025

SERIKALI imeweka wazi miradi ya kitaifa ambayo itatekeleza katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha ambayo italeta matokeo ya haraka na kuweka misingi thabiti kwa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 kwa kiasi cha Sh trilioni 4.5.

Miradi mingine ambayo imetangazwa na Serikali ni ile ambayo iko katika maeneo muhimu ya kiuchumi ambayo utekelezaji wake unatarajiwa kuwezesha ukuaji wa haraka wa uchumi ambao ni shirikishi na kupunguza kiwango cha umasikini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu Stephen Wasira alitaja miradi hiyo mikubwa kuwa ni ujenzi wa kituo cha biashara na uwekezaji Kurasini, uimarishaji wa Reli ya Kati katika maeneo ya Tabora-Kigoma, Isaka-Mwanza na ukarabati wa reli kilometa 197.

Pia katika eneo hilo la reli, kuna ununuzi wa vifaa kwa ajili ya ukarabati wa reli, ukarabati na uboreshaji wa njia ya reli katika eneo la Kidete-Gulwe; ujenzi wa daraja la Bahi, Kintinku na ukarabati wa injini na mabehewa ya treni.

Wasira alisema fedha zimetengwa kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa njia ya reli katika maeneo ya kimkakati ambayo ni reli ya Mtwara-Mbambabay na Mchuchuma na Liganga; reli kutoka Dar es Salaam-Isaka-Kigali-Keza na Geita-Msongati, na reli ya Tanga (Mwambani)-Arusha-Musoma.

Kwa upande wa nishati ya umeme, Wasira alisema fedha zimetengwa kwa jili ya miradi ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam na mitambo ya kufua umeme Kinyerezi.

Kwa upande wa usambazaji; fedha zimetengwa kwa ajili ya miradi ya ujenzi na uimarishaji wa njia za umeme wa msongo mkubwa kutoka Iringa kwenda Shinyanga na kutoka Makambako kwenda Songea.

Katika sekta ya barabara, miradi iliyopewa kipaumbele ni pamoja na barabara zenye kufungua fursa kiuchumi zinazounganisha Tanzania na nchi jirani na zile ambazo zinasaidia kupunguza msongamano mijini pamoja na ujenzi wa madaraja na vivuko.

Wasira alisema sekta ya kilimo na viwanda, miradi itakayotekelezwa inajumuisha ile ya kilimo cha miwa na mpunga katika mabonde makuu ya Wami, Ruvu, Kilombero, Kagera na Malagalasi pamoja na Miradi katika Ukanda wa Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Miradi ya Kilimo ya wilaya (ASDP) na miradi ya kilimo cha umwagiliaji.

Kwa upande wa viwanda miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ile ya chuma na makaa ya mawe Mchuchuma na Liganga, kukamilisha kiwanda cha viuawadudu Kibaha, mradi wa magadi soda Bonde la Engaruka na Uwekezaji katika Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (EPZs) na (SEZs).

Aidha alisema Serikali italipa fidia katika maeneo maalumu ya EPZE yaliyoko Bagamoyo na Kigoma.