17Juni2013

 

SMZ kukabiliana na changamoto za tabia nchi

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi yaliyoikumba dunia kwa ujumla, juhudi za makusudi zinahitajika ili kuvihami visiwa vidogo vidogo na mabadiliko ya tabia ya nchi yanayotokana na mazingira.

 

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Islam Seif wakati alipozungumza na vikundi vya mazingira huko katika kisiwa kidogo cha Kwale mjini Unguja.

Alisema mabadiliko ya tabia ya nchi ambayo yameikumba dunia kwa ujumla yanahitaji hatua za mikakati ya kudumu ili kuona hakuna athari kubwa zinazoweza kujitokeza katika kipindi hicho.

Tumeanza kuchukua juhudi za makusudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa lengo la kuvihami baadhi ya visiwa vidogo vidogo ambavyo vipo katika hali mbaya ya mabadiliko hayo.

Alivitaka vikundi vya mazingira katika maeneo ya visiwa vidogo kuhakikisha kwamba wanalinda mazingira na kuachana kabisa la kazi za kukata miti ovyo ambazo ni chanzo cha uharibifu wa mazingira katika eneo hilo.

Aidha alikemea uvuvi haramu unaofanywa na baadhi ya watu katika maeneo ya visiwa vidogo ikiwemo uvuvi wa kutumia baruti na nyavu zenye macho madogo ambazo hazifai kwa matumizi ya shughuli za uvuvi.

Hivi karibuni baadhi ya wataalamu walisema visiwa vidogo vidogo vilivyopo Pemba kikiwemo kisiwa Panza kipo katika hatari ya kutoweka kutokana na kasi ya mawimbi ya bahari kuvamia nchi kavu.

Hatua hiyo imezusha hofu kubwa kwa wananchi hao ambao baadhi yao wameanza kukihama kisiwa hicho na kurudi katika maeneo ya nchi kavu.

Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia mabadiliko ya tabia ya nchi limetoa zaidi ya Sh bilioni 5 kwa Tanzania kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.