'Ninaamini HabariLeo ni bora zaidi'

MADA iliyopita nilizungumzia safari yangu ndani ya chumba cha habari cha HabariLeo. Nilizungumza mambo mengi kuhusu usanifu na namna ambavyo vijana wanaweza kuchukua mfano katika maandiko yangu kuhusu suala la utumishi wa umma na dhamira ya kweli ya kutumikia mwajiri na wateja wake.

Leo napenda kuzungumzia imani yangu binafsi kuhusu gazeti hili ambalo wapo watu wanadhani halina kitu cha maana katika maisha yao.

Kwangu naona gazeti hili la serikali pamoja na kuwa kiungo, ni gazeti rejea na washiriki wake katika kipindi hiki wamejifunza kuandika habari zenye nidhamu ya taaluma na kuachana na ushabiki maandazi ambao wengi wamekuwa wakiushobokea.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, wengi tuliokuwa kwenye taaluma hii kwa miaka kadhaa, tulishuhudia mambo ambayo ni aibu kuyasema hapa.

Mambo ambayo jamaa zangu katika tasnia wanaweza kusema katika jukwaa kwa kebehi na kukubali wakiwa pekee, ushabiki wa siasa uliojengwa katika misingi tata ya chuki lewa isiyo na chembe ya taaluma.

Chuki lewa hii ilisababisha karibu vyombo vya habari vya kitamaduni (mainstream) kuibaka serikali hadharani katika kile kinachoonekana dhahiri kampeni kubwa ya kuondoa CCM madarakani kwa gharama yoyote ile.

Vyombo hivyo havikuona mambo mazuri viliona mambo mabaya vikaendesha kampeni ya hisia na kuacha tundu dogo sana la waelewa kuelewa.

Kama gari lenye gia tano na spidi 140 vyombo hivyo vilikuwa katika namba tano (mkoba) na tena wamekanyaga mafuta mpaka mwisho hivyo pistoni zikawa hazipumui hata kidogo. Kutopumua kwa piston katika gari la petroli kuna raha yake, lakini mwendo mrefu una balaa zake.

Kuna maeneo unatakiwa kupumua kwa staili yake ili vyuma navyo vipate nafasi nzuri na mifumo ya kupoozesha injini iwe katika utaratibu mkubwa zaidi.

Nimetolea mfano wa gari kutokana na ukweli kuwa uandishi wa habari ni taaluma na kila injini ina namna yake ya kumudu wakati mgumu, kwa main stream, ilikuwa basi kuanzia kwenye mchakato wa CCM kumpata rais mpaka katika mchakato wa taifa wa kumpata Rais.

Hapa ndipo HabariLeo lilipojipambanua na katika kujipambanua huko kulifanya kupoteza mashabiki. Lakini lenyewe linaweza kuringia rekodi safi ya kueleza serikali imefanya nini na wagombea wa chama tawala wanafikiria nini.

Katika hili kuna baadhi ya vyama vilikataa waandishi wa habari wa HabariLeo wakisema kwamba hawawezi kwenda na waandishi ambao wanaishabikia serikali; kwamba kufanya kazi HabariLeo ni kushabikia serikali, wakasahau kitu kimoja tu kwamba vyombo vyote takribani asilimia 85 vinaisuta serikali bila kuipa nafasi ya kujieleza.

Mimi nilipoulizwa katika chombo kimoja cha televisheni nilisema HabariLeo kama chombo cha serikali ni mdomo wa serikali na kama kuna mtu anataka kufahamu serikali imefanya nini na inakusudia kufanya nini atalichukua gazeti hilo kwa kurejea na wale wengine wanaoichamba serikali wana sababu zao na wamejipambanua.

Nilisema pia kwamba kama tungekuwa na utamaduni wa maana, vyombo vya habari vingelieleza wazi vinamshabikia nani.

Lakini si kwa kusema kwamba wao wanaripoti kitaaluma wakati watu wenye akili wanaona nguvu kubwa inayotumika kuwapa taarifa wananchi ubaya wa serikali na chama chake tawala na kwamba wasiichague.

HabariLeo walifanya kazi yao na wapo watakaosema kwamba wameifanya kuitetea serikali, lakini pamoja na hayo yote, wangelifanya nini? Je, walifanikiwa kitaaluma HabariLeo wakashindwa kisiasa?

Naamini kabisa kitaaluma walifanikiwa lakini kama ilivyo kawaida, ada ya mja hunena muungwana ni vitendo, HabariLeo iliendelea kusema kuhusu serikali kwa kuzingatia misingi ya taaluma bila chumvi.

Ni kweli kazi ambayo imefanywa na Habaarileo ni kutoa taarifa za kweli za kina na zenye uhakika kutoka vyanzo vya uhakika wananchi waweze kuchambua na mwishoni wafikie dhima yao wanayoitaka.

HabariLeo ilitambua wajibu wake, ilitambua dhima yake, ikatambua mahitaji ya wananchi ikawapa elimu inayostahili kuhusu uchaguzi na kueleza kwa ufasaha kwa kila mgombea kwa staha ya aina yake bila kusababisha mitafaruku isiyokuwa na maana katika jamii. Ule usemi wa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete wa tunajenga nyumba moja kwa nini tugombee fito, ulitawala hisia za waandishi na wahariri wa Habari- Leo.

Bila kujitambua wakatekeleza kazi yao kwa umahiri mkubwa wakijali amani zaidi na taifa, mauzo kesho. Waliwatumikia wale wasiokuwa na sauti, wakaelewa nini maana yake. Kwangu mimi niliona kwamba nadharia tisa za uandishi wa habari uliotukuka ulibaki zaidi katika chumba cha habari cha HabariLeo wakiachana na ushabiki uliokuwa ukiendekezwa na vyombo vingine ikiwamo mitandao ya kijamii.

Mfano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ni rahisi kuingia kichwani, lakini kiukweli gazeti hili tangu limeanza ugomvi wake mkubwa ni usahihi na ukweli wa habari kwa mahitaji ya wananchi. Na katika hili mnara mkubwa wa kwanza ulikuwa unatekelezwa.

Kwangu niliona kwamba gazeti linasaidia kuimarisha demokrasia kwa kuandika habari za uhakika zenye maana kwa kuwa haikuwa suala la usahihi na ukweli pekeekwa manufaa ya falsafa bali katika ukweli wa uhalisia wa mahitaji ya wananchi katika habari zenye ukweli na sahihi ili kukuza uelewa na kushiriki vyema katika maendeleo ya taifa lao kwa kutengenezewa uwezo wa kuhoji.

Wananchi walikuwa wanamezeshwa habari za aina moja, lakini HabariLeo ikijitambua kama daraja ilikuwa na kazi kubwa ya kuwa karibu na wananchi ikiwaeleza kutambua fursa.

HabariLeo haikushughulika na matangazo ya walipa fedha, wanaonunua karibu main stream yote, lakini pia ilitengeneza muundo wa utoaji habari ambao ulizingatia zaidi kuliwekea heshima gazeti hili kwa kuwa na habari ambazo hazina urafiki bali za kuonesha fursa zilizopo.

Kitu kilichonipa raha zaidi katika miaka 10 ya gazeti hili, ni ile ari ya nidhamu ya kutafuta usahihi wa habari. Yaani kuhakiki taarifa ambazo unazo mkononi na nyuma ya pazia kuangalia nini maana yake nini.

Ni katika hili , wameliepusha gazeti hili na mabalaa ya kulaumiwa kila mara, na kubaki gazeti la kupongezwa kutokana na uhakiki wake wa habari.

Sio kwamba hawajaingizwa chaka, lakini machaka yaliyoingizwa yamesaidia sana kutengeneza uwezo wa kutambua maana halisi ya uhakiki wa taarifa si wa vyanzo vilivyotoa bali pia katika vyanzo vinavyofanana nayo. Pamoja na kazi hiyo, muundo uliokuwepo awali ulisaidia kutoa nafasi ya uhakiki wa habari na ubora wa tafsiri ya mwandishi katika hoja mbadala.

Aidha taratibu waandishi walianza kuona haja ya kuwa huru, kutokana na mhariri wa habari kuwa mkali. Katika hili umbogo, mathalani wa Mhariri Kingoba Mgaya.

Swali ambalo watu wengi wanaweza kujiuliza katika kufikia hitimisho ni kama gazeti linaandika habari zinazogusa wanyonge au la na kama linatumika watu kuonesha hasira zao kwa kupewa nafasi ya kujieleza, watendaji kutumia busara zao kuliendesha na kama kweli linatumika kama mhimili wa nne wa dola.

Haya ni maswali yatakayoendelea kuulizwa na kila msomaji na mtafiti, lakini kama huna mwegemo utajua kwamba HabriLeo litaendelea kuwapo kutokana na kufuata taaluma inavyohitaji na kumjua mwajiri anataka nini katika kumsaidia kukutana na wateja wake ambao ni wananchi.

Kwa taaluma napenda kutambua uwapo wa HabariLeo kama moja ya chombo ambacho kwa miaka yote udaku ni marufuku lakini taarifa za kina kuhusu uzalendo wetu zikiendelea kutolewa hoja.