HabariLeo limeleta matumaini Ruanda

UKIENDA katika vijiji vinavyounda kata ya Ruanda hususani kijiji cha Ntunduwaro, wilayani Mbinga, ukaulizia kuhusu gazeti la HabariLeo, lazima utapata mwitikio wa watu wengi wanaolifahamu. Hata kama si wote waliowahi kulisoma moja kwa moja, lakini wana ushuhuda juu ya umuhimu wa gazeti hili katika maisha yao.

Ushuhuda huo unajikita kwenye suala zima la kupatikana kwa ufumbuzi wa kilio chao juu ya changamoto zilizowakabili kwa muda mrefu tangu mwaka 2011 bila kupatiwa ufumbuzi.

Wananchi hawa wapatao 2,400 wamekabiliwa na athari za kiafya na kimazingira ambazo zimekuwa zinawasumbua kwa muda mrefu kutokana na uchimbaji wa madini tangu mwaka 2011 kwa kuwa kipo ndani ya eneo la mgodi.

Kwa mujibu wa sensa ya makazi ya mwaka 2012, vijiji vinavyounda Kata ya Ruanda vina jumla ya wakazi 7374 ambao wanatoka katika vijiji vya Ukombozi, Ntunduwaro, Paradiso na Ruanda.

Wakazi wa vijiji hivyo walilalamikia muda mrefu kuwa wanapata athari ya vumbi kutoka kwenye magari yanayobeba makaa wa mawe hadi bandari ya nchi kavu ya Kitai. Awali changamoto hizo hazikuibuliwa kiasi cha kujulikana kwa mamlaka zenye uamuzi na utoaji suluhu.

Lakini gazeti la HabariLeo liliwafikia wakazi hawa, likatafiti katika vijiji vya kata ya Ruanda juu ya athari hizo za kiafya na kimazingira zinazotokana na uchimbaji wa makaa ya mawe unaofanywa na Kampuni ya Tancoal.

Ilikuwa Julai hadi Septemba, 2016 nilipoamua mwandishi wa makala haya alipoamua kujikita kufuatilia kero hiyo inayowakumba wakazi wa kata hiyo. Julai 5, 2016, mwandishi wa makala haya alipokwenda kijiji cha Ntunduwaro akiwa na Mkemia wa Maji wa Maabara ya serikali, Dk Philemoni Kinyangadzi.

Alikwenda kupima ubora wa maji hayo baada ya kuwapo malalamiko ya wananchi wa Ntunduwaro wakidai kuugua magonjwa yanayosababishwa na kula, kunywa uchafu. Wakazi wakalalamikia pia baadhi yao kukabiliwa na tatizo la vifua visipona.

Matokeo ya vipimo vya kibayolojia vya ubora wa maji katika maabara ya Serikali Kanda ya Songea vilivyochukuliwa kwenye vyanzo vya maji ya visima vya asili, mito na bomba katika maeneo ya mgodi. Vikaonesha kuwa vyanzo vya maji vimechafuliwa katika kiwango ambacho hakifai kwa matumizi ya binadamu.

Dk Kinyangadzi akasema uchafuzi huo umetokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu zinazofanywa kuzunguka vijiji vilivyopo eneo la mgodi ikiwemo ufugaji holela, uchimbaji wa madini na utupaji wa taka kwenye vyanzo vya maji.

Hata hivyo, alisema sampuli za vipimo vya kikemikali ambavyo vimechukuliwa kwenye mito na visima vinaonesha maji hayo bado yanakidhi viwango vya Tanzania.

Alihadharisha akisema, baadhi ya sampuli zimeonesha hewa ya oksijeni imepungua kwenye maji hivyo kuathiri viumbe hai wa majini kama samaki.

Mkemia huyo wa maji akaishauri serikali kuangalia uwezekano wa kutafuta maji katika vyanzo vingine vya mbali ambavyo havijachafuliwa ili kuwaokoa wananchi wa eneo hilo ambao baadhi yao tayari wanadai kuugua magonjwa ya matumbo.

Katika makala iliyoandikwa na gazeti hili, ilimkariri Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ntunduwaro akisema, tangu mwaka 2011 wananchi walikuwa wanaugua magonjwa ya matumbo mara kwa mara, bila kujua kuwa maji wanayotumia yalikuwa hayafai kwa matumizi ya binadamu.

Ofisa mtendaji huyo alikiri kuwa, mwandishi wa HabariLeo amekuwa mkombozi wao kwa kuwa sasa wanachukua hadhari kwa kuchemsha maji kabla ya kunywa.

“Kilio kikubwa cha wakazi wa hapa ni kupata maji safi na salama. Tunaomba serikali ituokoe katika hili, tukipata maji safi na salama tutakuwa na afya na kuweza kuwajibika, bado wananchi wanaugua magonjwa ya matumbo kwa kuwa tunaendelea kutumia maji machafu,’’ alisisitiza.

Mwandishi pia alibaini wakazi wa Kata ya Ruanda na vijiji vilivyopo barabarani kutoka mgodi wa makaa ya mawe Ngaka wanapata athari za kimazingira zinazosababishwa na vumbi wakati wa kusafirisha madini hayo kwa njia ya barabara hadi Kitai.

Diwani wa Kata ya Ruanda, Edmund Nditi aliweka wazi kuwa, Desemba 2015 ilifanyika sensa ya kubaini idadi ya nyumba ambazo zilipasuka na kuweka nyufa ambapo nyumba zaidi ya 250 zilibainika kuathirika kutokana na ulipuaji wa miamba unaofanywa na Kampuni ya Tancoal.

Ikabainika kampuni hiyo inatumika teknolojia ya zamani katika uchimbaji wa madini hali ambayo inasababisha athari za milipuko na kupasuka nyumba. Hata hivyo katika makubaliano kwenye mkataba, kampuni ilitakiwa kutumia teknolojia ya kisasa katika uchimbaji wa madini hayo.

Tangu kuchapwa kwa makala hizo katika gazeti la HabariLeo, viongozi wa serikali katika ngazi mbalimbali wamekuwa wanakwenda katika vijiji vilivyopo eneo la mgodi kuzungumza na wananchi na watendaji wa Kampuni ya Tancoal.

Lakini pia, hivi karibuni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekagua shughuli za mgodi wa makaa ya mawe Ngaka na kujionea namna kampuni ya Tancoal Energy Limited ambayo ni kampuni ya ubia kati ya NDC na Kampuni ya Pacific Corporation East Africa ya Australia inavyozalisha madini hayo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Kampuni ya Uchimbaji madini ya makaa ya mawe ya Tancoal kuhakikisha wanatekeleza haraka jukumu la kupeleka maji safi na salama kwa wananchi wanaoishi katika Kijiji cha Ntunduwaro Kata ya Ruanda Mkoa wa Ruvuma.

Amesema vyanzo vya maji vinavyozunguka mgodi wa Ngaka vimechafuliwa na kuleta madhara kwa wananchi hivyo wananchi wanaoishi karibu na mgodi huo hawana maji safi na salama hivyo ni jukumu la kampuni kuwasambazia maji safi na salama kama ilivyoelekezwa kwenye mikataba kabla ya kuanza mradi huo.

Kampuni ya Tancoal kwa kushirikiana na serikali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, wamepata chanzo cha maji safi na salama cha Kindimbajuu ambacho kitatumika kuleta maji safi na salama kwa wananchi wanaoishi eneo la mgodi kijiji cha Ntunduwaro na vijiji vya kata ya Ruanda.

Waziri Mkuu amesema hadi sasa, Tancoal haijatekeleza makubaliano yaliyofikiwa katika mikataba ikiwemo ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kitai ambayo ni bandari ya nchi kavu hadi mgodini hali ambayo inasababisha vumbi la makaa ya mawe kuwaathiri wananchi wanaoishi kando kando mwa barabara hiyo.

Ameagiza kujengwa haraka barabara ya lami kutoka mgodini hadi Kitai ili kuwaondolea adha ya vumbi wananchi wa kata ya Ruanda na kuwasababisha hatari ya kupata athari za kiafya na kimazingira.

Ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara isimamie kikamilifu utendaji wa NDC na kampuni ya Tancoal ili kuhakikisha makubaliano yaliofikiwa katika mkataba yanatekelezwa haraka.

“Watendaji wote waliopewa dhamana ya kuongoza mashirika ya umma ni lazima wahakikishe kuwa wanalinda maslahi ya taifa badala ya kukaa kimya hata wakati kuna ukiukwaji unaendelea kama ambayo imejitokeza katika mradi wa mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka,’’ anasisitiza Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amemuagiza Mbunge wa Mbinga Vijijini, Martin Msuha kufuatilia masuala yaliyomo kwenye mkataba yanayotakiwa kutekelezwa na kampuni hiyo kwa wananchi wa Kijiji cha Ntunduwaro na Kata ya Ruanda ili kuwaondolea kero na malalamiko wananchi hao.

Akizungumzia uzalishaji wa madini ya makaa ya mawe ambayo yanafanywa na Kampuni ya Tancoal, Majaliwa alisema baada ya kukagua mgodi huo, amebaini upungufu mwingi ikiwamo NDC kutolipwa gawio na kampuni hiyo tangu kuanza kwa uzalishaji mwaka 2011.

Mwandishi ni mchangiaji wa gazeti hili mawasiliano baruapepe:Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.,simu 0784765919