Ukifuga nyuki unatajirika

“TANZANIA imekuwa ikipoteza mamia ya tani za asali kila mwaka kutokana na kutotumia vyema rasilimali ya misitu lakini sasa tumeamua kutumia fursa hiyo vizuri ili kuendeleza sekta ya ufugaji nyuki Tanzania.“ Kauli hiyo inatolewa na Philemon Kiemi kutoka Kampuni ya Youth Interpreneurs and Consultant Society (SYECCOS) ya mkoani Singida ambayo ni mdau mkubwa wa biashara ya asali nchini.

Kiemi anasema sekta ya nyuki ikisimamiwa vyema inaweza kuingiza mapato mengi na kusaidia sana katika uchumi wa taifa ikizingatiwa kuwa Tanzania ina misitu mingi, maua yako kila mahali. Hata hivyo anasema, hawajatambua fursa kubwa iliyopo katika ufugaji nyuki.

Anabainisha kuwa, nyuki wakishawekewa misingi wanajitengenezea chakula wenyewe.

“Nyuki ni mdudu anayetoa mazao saba kwa wakati mmoja, lakini hali inaonesha ufugaji wa nyuki haujafanyika kama inavyotakiwa,” anasema.

Anaelezea asali imekuwa ikizalishwa ndani ya magome ya miti, kwenye mashimo na ukitengeneza mizinga kitaalamu utaweza kuzalisha zaidi.

“Asali inaweza kukaa bila kuoza kwa muda mrefu hata kwa zaidi ya miaka 30. Ukiangalia zao ambalo linaweza kukaa muda mrefu stoo basi ni asali,” anasema.

Anasema nyuki hutengeneza asali kama chakula chake ambayo hutumiwa na binadamu kwa chakula, na kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwamo dawa. Pia masega huzalisha nta.

Bidhaa zitokanazo na nta ni pamoja na mishumaa. Mdau huyu anaelezea kuwa ufugaji nyuki kwenye mizinga nchini ulianza tangu karne ya 16, wakati Wareno walipofika pwani ya Afrika Mashariki kisha Wajerumani na Waingereza. Kwa mujibu wa Kiemi ambaye ananukuu taarifa za historia ya ufugaji nyuki, Wajerumani walioanzisha ufugaji huo kwenye mizinga ya mbao hapa nchini.

Lakini ni mpaka mwaka 1949, wakati wa utawala wa Waingereza, ndipo sekta ya ufugaji wa nyuki ilipoundiwa idara yake chini ya Wizara ya Kilimo.

Hata hivyo, baada ya nchi kupata uhuru mwaka 1961, sekta ya ufugaji wa nyuki iliendelea kuwekwa chini ya idara za misitu na wanyamapori kwa nyakati tofauti. Kuanzia mwaka 1980 hadi 1984 sekta ya ufugaji nyuki ilipewa idara inayojitegemea kwenye wizara.

Kwa kutambua umuhimu wa ufugaji nyuki kitaifa, kwa kujenga na kukuza uchumi, kuondoa umasikini katika jamii, kulinda na kutunza mazingira, taifa lilitayarisha na kupitisha sera ya ufugaji nyuki ya mwaka 1998, ambayo ndiyo inayotumika mpaka sasa.

Inakadiriwa hapa nchini kuna himaya za nyuki zipatazo milioni 10 ambazo zina uwezo wa kuzalisha tani za asali 140,000, yenye thamani ya dola za Marekani milioni 140, na kupatikana nta tani 10,000 zenye thamani ya dola za Marekani milioni 19.

Mahitaji ya sasa ya asali na nta yanazidi kupanuka kwa kasi kubwa kutokana na wawekezaji wa viwanda kuhitaji asali kwa wingi hasa wenye kutengeneza bidhaa za vyakula na madawa.

Takribani asilimia 50 ya inayozalishwa, inatumiwa hapa nchini katika kutengeneza pombe za kienyeji na mvinyo. Aidha asilimia 10 inatumika katika viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu na pia kwenye viwanda vyenye tanuru za kuoka mikate na biskuti. Kiasi kidogo kinachobaki huuzwa nchi za jirani za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Wanunuzi wengine wa asali ya Tanzania ni nchi za Umoja wa Ulaya na hasa Uingereza, Ujerumani na Uholanzi. Wengine ni Umoja wa Falme za Kiarabu- Emirate na Omani.

Wanunuzi wakubwa wa nta ni Japan, Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya. Pamoja na kwamba asali na nta ya Tanzania vinatajwa kuwa na soko la uhakika na la kudumu, lakini uzalishaji wake wa asilimia 6.5 bado ni wa kiwango kidogo kwa kulinganisha na ukubwa wa eneo la nchi Idadi ya mizinga na idadi ya wadau milioni mbili wanaojishughulisha na ufugaji wa nyuki, bado ni ndogo sana wakati kazi hii ya ufugaji nyuki siyo ya suluba kama zilivyo kazi ngumu za migodini na uvuvi wa baharini.

“Miundombinu, uhaba wa vifaa na tekinolojia ya kisasa ya kufuga nyuki, vifaa muhimu vya kurina asali, kutunza, uchakataji na kufunga asali kwa kuuzwa nje ndiyo vinavyodumaza sekta ya ufugaji nyuki nchini,” anaelezea zaidi.

Mdau huyu anasema: Sisi tulipata msaada kutoka Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambao ulituwezesha kununua mtambo wa kisasa wa kuchakata asali ambao una uwezo wa kukamua tani moja kwa saa.

Anasema mwanzo walikuwa wanachakata katika ndoo lakini baada ya kupokea fedha kutoka ILO, walinunua mtambo wa kisasa ambao unakamua asali tani moja jambo linalowawezesha kuwa na uwezo wa kuuza asali mahali popote duniani. Anasisitiza kuwa, sasa wako tayari kutoa elimu hiyo kwa makundi mbalimbali ili watu wengi zaidi wanufaike na fursa hiyo.

Anasema kama kikundi, wanaona jinsi nyuki wanavyowapeleka mbali. “Tuna misitu ya kutosha lakini kila mwaka tunapoteza mamia ya tani za asali kutokana na kushindwa kutumia fursa ya ufugaji nyuki vizuri,” anasema.

Singu Mayaya ni Ofisa Nyuki katika shamba la Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda. Anasema sekta ya ufugaji nyuki ikisimamiwa vizuri itatoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi. Anasema uendeshaji wa kilimo na ufugaji nyuki umekuwa na tija kubwa kutokana na uwekezaji kufanyika kwenye eneo dogo.

“Hapa tulipo kuna miembe lakini kuna vibanda vya mizinga ya nyuki, utavuna maembe na mizinga itaendelea kuwepo, ukivuna asali miembe itakuwepo pia, unaweza kuwa na shamba la kawaida lakini ukafanya shughuli zako hapo bila kuathiri chochote,” anasema.

Anashauri katika suala zima la ufugaji nyuki wa kisasa ni vyema mizinga ikajengewa kichanja ili iwe rahisi kuikagua tofauti na kuweka juu ya miti ambako nguvu nyingi hutumika kuishusha na kufanya ukaguzi. Pia anasema ni vyema banda la nyuki likaezekwa kwa kutumia majani kwani linapoezekwa kwa bati, joto linapozidi nyuki atahitaji kutafuta maji ili apooze mzinga wake.

“Kama banda lina unyevunyevu nyuki atalazimika kutengeneza joto,” anasema.

“Kwenye miti kuna maadui wengi wa nyuki ambao huvamia mizinga huwa hamna namna nyingine ya kuwaondoa zaidi ya kuishusha mizinga,” anasema.

Ofisa nyuki huyo anaelezea tabia ya nyuki akisema, wamekuwa hawapendi manukato au harufu ya pombe na kwamba, mtu wa namna hiyo akipita karibu lazima atashambuliwa.

Mshauri katika shamba la Waziri Mkuu, David Kamara anasema lengo kubwa la kiongozi huyo mstaafu kuanzisha shamba hilo ni kuona kilimo kitabadilishaje maisha ya watu.

“Watu wengi wanakuja kuangalia shughuli zinazofanyika hapa kutoka ndani na nje ya nchi, vijana kama wataweza kutambua uchumi wa asili wanaweza kuleta mabadiliko makubwa,” anasema.

Anasema nyuki wamekuwa na faida kubwa na wanapofugwa kwa kufuata utaalam ni chanzo kikubwa cha kipato.

“Ukiwa na shamba fikiria namna ya kuweka mizinga hapo kuna faida kubwa sana, huhitaji hata kuajiriwa kama unataka fedha basi ipo kwenye asali,” anasema.

Pia anasema ni vyema serikali ikawekeza kwa vijana kwenye mafunzo ya vitendo na si kwa fedha nyingi kuishia kwenye mikutano na makongamano bila vijana hao kujua uhalisia wa kile wanachotakiwa kukifanya.

“Vijana wawe na tabia ya kupenda kujifunza bila kujali una elimu kiasi gani kuna watu wamemaliza vyuo vikuu lakini wamejiajiri kwenye miradi ya kufuga nyuki na wanapata faida kubwa,” anahimiza vijana.

Pinda amekuwa akihimiza umuhimu wa kuwekeza katika kuzalisha asali ili sekta hiyo itoe mchango unaostahili katika uchumi. Anasema, iwapo sekta ya ufugaji nyuki itapewa kipaumbele, uzalishaji utaongezeka na hivyo kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.

“Sekta ya ufugaji nyuki imeajiri zaidi ya watu milioni mbili. Si sekta ndogo kwa maana ya mchango wake katika uchumi wa taifa,” anasema.

Pia anasema takwimu za wachambuzi wa biashara ya mazao ya nyuki kimataifa zinaonesha soko la asali ulimwenguni linategemea kuongezeka hadi kufikia tani milioni 1.9 zenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 12 kwa mwaka huu wa 2015 “Mazao ya nyuki yana bei nzuri ndani na nje ya nchi na kinachotakiwa ni kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao ya nyuki kwa kuzitumia taasisi zilizo za kiserikali na zisizo za kiserikali. Pinda anasema asali ya Tanzania ni miongoni mwa asali bora na nzuri sana ulimwenguni.

“Hii inatokana na ukweli kwamba asali ya Tanzania asali nyingi inayozalishwa Tanzania inatokana na misitu ya asili ambayo ipo huru na kemikali zinazohusu shughuli za kilimo.”

Pia anasema kuna asali inayotokana na karafuu eneo la Pemba, vichaka vya Itigi, migunga (acacia) maeneo ya Katavi, Ludewa (Njombe) na Igunga (Tabora) inaweza kuongeza thamani ya asali na vile vile kuwa na viini lishe na tiba tofauti za asali nyingine za kawaida.

“Kuna umuhimu wa kufanya utafiti wa kina wa asali hizo ili kubaini viini lishe na tiba sahihi kwenye asali hizo na hiyo itasaidia kuongeza thamani katika soko la dunia,” anasema.

Waziri Mkuu mstaafu anataja takwimu kuwa zinaonesha Tanzania ni nchi ya pili Afrika kwa uzalishaji wa asali. Huzalisha tani 34,000 kwa mwaka huku Ethiopia ikiwa ya kwanza kwa kuzalisha tani 54,000 kwa mwaka.

Wazalishaji wakubwa wa asali duniani ni China, Urusi, Marekani, Mexico, Argentina, Canada, Brazil na Australia. China inaongoza kwa kuuza asilimia 40 ya asali yote inayozalishwa katika soko la dunia.