Usawa wa jinsia muhimu kwa usalama wa chakula

NI saa 12 alfajiri, Ndigwako tayari yuko shambani eneo la Itunge, wilayani Kyela, kwa ajili ya maandalizi ya shamba la mpunga. Ndigwako mwenye mtoto wa mwaka mmoja na nusu, anaambatana na mtoto wa miaka mitatu ambaye kazi yake kubwa ni kukaa na mtoto chini ya mti wakati mama akiendelea na shughuli za shamba.

Akitoka shambani, Ndigwako (sio jina halisi) anachuma uyoga shambani sambamba na kuokota kuni kwa ajili ya kuandaa chakula cha familia yake.

Akiwa na jembe begani, uyoga mkononi na kuni kichwani, mama huyu na wanawe wanarejea nyumbani majira ya jioni ili kuendelea na shughuli nyingine za kuihudumia familia.

Ndigwako anawakilisha kundi kubwa la wanawake ambalo linaelezwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kiuchumi, ikiwamo kilimo katika mataifa mengi ya Afrika, ikiwamo Tanzania.

Hali hii inatokana na fikra potofu kuwa kilimo ni shughuli duni na hivyo kuachiwa wanawake zaidi, ingawa ni kundi ambalo pia halinufaiki na kilimo chao kutokana na mfumo dume ambao unamtaka mtu mwenye maamuzi katika familia ni mwanaume.

Katika Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 2000, inabainisha kuwa takribani asilimia 90.4 ya wanawake ni wazalishaji mali katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi. Wanawake katika sekta ya kilimo wanakabiliwa na tatizo la nyenzo duni, ukosefu wa mitaji, ujuzi mdogo na kutokuwa na milki ya ardhi.

Takwimu za mwaka 2014 zinaonesha kuwa, kilimo nchini ndio nguzo kuu ya uchumi ikichangia takribani asilimia 30 ya pato la taifa na asilimia 67 ya ajira, huku wanawake wakiwa ndio nguvu kazi kubwa ukilinganisha na wanaume.

Tafiti zinaonesha kwamba wanawake wamekuwa na mzigo mzito katika sekta hii, hasa kwa shughuli za awali kwenye mnyororo wa thamani wa shughuli za kilimo ambazo ni uandaaji wa shamba, upandaji wa mazao, upaliliaji wa shamba, utunzaji, uvunaji, uhifadhi na usindikaji.

Pamoja na wanawake kuwa wahusika wakuu na wanatumia muda mwingi kwenye shughuli za awali za kilimo, mara nyingi wamekuwa hawafaidiki na jasho la kazi zao kutokana na sababu kadhaa ikiwemo zile za tamaduni na mila zisizozingatia jinsia na baada ya sheria ambazo sio rafiki kwa mwanamke.

Hali hii ndiyo iliyofanya Shirika lisilo la kiserikali la Land O’Lakes kuja na mradi wa miaka minne unaohusu ‘Ubunifu katika usawa wa jinsia (IGE) katika kukuza usalama wa chakula’.

Kwenye warsha ya siku moja kuhusu Usawa wa Kijinsia katika Kilimo, Usalama wa Chakula na Lishe, ambayo imeandaliwa na Land O Lakes kwa ufadhili toka Shirika la misaada la marekani (USAID), Mkurugenzi wa Land O Lakes, Dk Rose Kingamkono anasema shirika lake limetekeleza mradi wa kuwawezesha wanawake kunufaika kutokana na sekta ya kilimo, kuongeza usalama wa chakula katika ngazi ya kaya na kuinua afya na lishe ya familia.

Shughuli za uelimishaji na uhamasishaji wa kampeni za Land O' Lakes kuhusu usawa wa kijinsia katika masuala ya kilimo, usalama wa chakula na lishe zinaratibiwa na Shule kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Mwanamke ambaye ndiye mzalishaji mkuu, anaelemewa na majukumu mengi kama ya kubeba mimba, kulea, shughuli za nyumbani na zile za kijamii,” alisema Dk Kingamkono wakati akiuelezea mradi huo unaotekelezwa katika mikoa ya Morogoro Iringa, Songwe na Mbeya.

Anasema mradi huo umetekelezwa katika maeneo hayo kwa kutambua, kusambaza na kukuza teknolojia iliyo rafiki kwa wanawake.

“Hatuwezi kumwambia mwanamke aachane na kazi ya kilimo, lakini tukaona tuje na teknolojia rahisi inayomrahisishisa kazi ili asitumie muda mwingi kwenye kazi hizo,” anasema.

Anasema katika eneo hilo waliweza kutambua na kuwaendeleza watu walioshiriki kubuni teknolojia rafiki kwa mwanamke katika kilimo kupitia shindano.

“Tukifanya shindano, aliyeshinda alikwenda kufanya majaribio ya teknolojia yake kwa wakulima, na kama ilifaa, alisaidiwa mtaji wa kuendeleza na kutafutiwa soko la teknolojia,” anasema.

Kingamkono anaendelea kusema mpaka sasa wametoa mafunzo wa wabunifu wa teknolojia 319 na kati ya hao wanawake ni 169 huku akiainisha kuwepo kwa makundi 148 ya wabunifu.

Alitaja teknolojia iliyobuniwa kuwa ni pampu ya umwagiliaji kwa njia ya mikono, pampu ya umwagiliaji kwa umeme jua, uzalishaji wa uyoga, kutengeneza sabuni, mkaa, kifaa cha kurahisisha upandaji wa mpunga pamoja na kiengulia vifaranga cha ardhini. Anasema wapo wengine waliopata mafunzo ni wabunifu wa kifaa cha kutengeneza tambi, kubangua karanga, mpunga, mahindi, kikausha mboga.

“Walionufaika na mradi huu ni wengi, na mwisho tuna ubunifu ambao umechaguliwa kwa ajili ya kupewa msaada nyongeza ambao ni pampu ya umwagiliaji ya kutumia umeme jua, uzalishaji uyoga, kubangua karanga, kikaushia matunda na mboga za majani, na kitotolesho cha vifaranga cha ardhini,” anasema.

Kingamkono anasema eneo lingine ni kuboresha maarifa ya mwanamke katika masuala muhimu ya kumnyanyua mwanamke, ambapo elimu mbalimbali zilitolewa za kumfanya mwanamke awe kiongozi katika familia yake. Katika mikoa hiyo yote, jumla ya familia 24,423 zimenufaika.

“Tumetoa elimu kwa kuongeza uwelewa na maeneo nyeti na vikwazo vya kijinsia kwenye kilimo, kuibua mjadala na uwelewa miongoni mwa jamii kuhusu umuhimu wa uongozi wa wanawake katika kilimo na maisha na kuwa na maamuzi ya kile wanachokizalisha,” anasema.

“Tulitaka mwanamke aweze kusimama na hata kutetea mambo ambayo ni muhimu, aweze kuwa na maamuzi hata ya mazao anayozalisha mwenywe badala ya kumwachia mwanaume pekee,” anasema. Anasema pia wamepitia na kuangalia mabadiliko ya sera za usawa wa jinsia katika kukuza kilimo.

“Tumeangazia sheria, kanuni, mila, desturi na tamaduni kandamizi zinazopunguza fursa ya mwaname kupata haki za msingi kama vile ardhi, rasilimali fedha, mafunzo na teknolojia sahihi na rahisi za kumsaidia mwanamke kupunguza nguvu na muda mwingi anaotumia katika kilimo na kazi za nyumbani na uzalishaji mali.

“Haya yote humpunguzia mwanamke uwezo wa kufanya shughuli za uzalishaji mali kwa ufanisi na kuchangia ustawi wa familia na jamii kwa ujumla, upungufu wa chakula na lishe duni katika kaya,” anasema.

Anasema pia katika kuhakikisha kunakuwa na programu endelevu katika kumnyanyua mwanamke, wameanzisha Kituo cha Kuendeleza wanawake katika kilimo Tanzania (CAWAT).

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen anasema wanawake wanaojishughulisha katika sekta ya kilimo hasa vijijini hawafaidiki na jasho lao na kuvitaka vyombo vya habari kumulika na kuandika changamoto zinazomgusa mwanamke katika kilimo, ikiwa ni kuangalia ni kwa namna gani sera na sheria zinamsaidia au kumkandamiza mwanamke na mwanaume katika mnyororo wa thamani wa shughuli za kilimo.

“Pia kuangalia imani na mila potofu ambazo zinamkandamiza mwanamke na kumfanya ashindwe kushiriki kikamilifu na upatikanaji wa mikopo kwa wanawake katika sekta ya kilimo.

Anasema vyombo vya habari vitumike kuelimisha jamii kuhusu mgawanyo wa majukumu baina ya wanawake na wanaume katika shughuli za kilimo na shughuli za nyumbani (kaya) na mchango wa wanawake katika usalama wa chakula na lishe kwa familia na namna gani wanaume wanaweza kuchangia kuimarisha hali hii.

“Pamoja na kwamba wanawake ndio wahusika wakuu na wanatumia muda mwingi kwenye shughuli za awali za kilimo, mara nyingi wamekuwa hawafaidiki na jasho la kazi zao kutokana na tamaduni na mila zisizozingatia jinsia,” anasema.