Mkakati wa China kukujenga viwanda Tanzania

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Tanzania itaendeleza ushirikiano na Serikali ya China katika nyanja mbalimbali kupitia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda, nishati na miundombinu. Hii ni kauli aliyoitoa hivi karibuni, alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, kwa niaba ya Rais John Magufuli, jijini Dar es Salaam.

Majaliwa anataja ushirikiano wa Tanzania na China kuwa ni wa kihistoria ambao utaendelezwa kwa manufaa ya wananchi wa pande zote.

Anawakaribisha wawekezaji kutoka China kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini hususani kwenye miundombinu, viwanda, kilimo na nishati.

“Tanzania iko tayari kupokea kampuni zaidi za China kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali nchini,” anasema waziri mkuu akisisitiza kuwa, nchi iko tayari kupokea viwanda kati ya 200 hadi 700 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Waziri huyo wa China, Wang Yi anapongeza utendaji kazi wa Rais Magufuli pamoja na viongozi wengine hususan katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi ambayo matunda yameanza kuonekana.

“Serikali ya China kwa sasa iko katika mkakati wa kuhamishia viwanda vyake vingi barani Afrika. Iliamua kuichagua Tanzania kuwa moja kati ya nchi watakazohamishia viwanda hivyo kutokana na kuridhishwa na dhamira inayoonyeshwa na serikali katika kuleta maendeleo,” anasema waziri huyo.

Wang alisema China inatambua mchango mkubwa wa Tanzania katika harakati za kujikomboa hivyo itaendelea kuiunga mkono kuhakikisha inafikia uchumi mzuri.

Lakini pia, nchi hiyo inasisitiza kuendeleza ushirikiano wake na Tanzania kwa kuboresha miundombinu ikiwemo kujenga uwanja wa ndege na bandari Zanzibar.

Pia itajenga jengo la wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mjini Dodoma kuwezesha ihamie mjini humo kama ilivyoelekezwa.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga anasema msaada huo wa China ni mwendelezo wa ushirikiano ulioanzishwa na waasisi wa mataifa hayo Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mao tse tung. Balozi Mahiga anasema, miradi mingine itakayotekelezwa ni pamoja na bandari ya Bagamoyo na reli ya Mamlaka ya Reli Tanzania na Tambia (Tazara).

Kwa mujibu wa waziri Mahiga, kwa sasa wanaangalia hali ilivyo na fursa zilizopo pamoja na kutazama maeneo mapya ya kiuchumi na kuyaendeleza.

Mkakati wa China wa kuhamishia viwanda Afrika, hususani Tanzania, unatoa changamoto kwa serikali na wadau wengine kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri yatakayofanikisha lengo hilo.

Hii ni pamoja na kuhakikisha, nchi inakuwa na miundombinu rafiki itakayofanikisha lengo la usafirishaji wa malighafi na huduma nyingine kwa ajili ya viwanda.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa anasema ndiyo maana serikali imeelekeza bajeti kubwa kwenye miundombinu kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa viwanda.

"Tumesikia katika semina hii kwamba wenzetu Wachina wameichagua Tanzania kuwa nchi ya kwanza kutekeleza mpango wake wa kuhamishia viwanda barani Afrika, hii ni fursa nzuri kwetu ambapo kama serikali tumeamua kutenga zaidi ya asilimia arobaini ya bejeti kwenda kwenye miundombinu kwa ajili ya kuchochea kasi ya uanzishaji wa viwanda," ni kauli ya Profesa Mbarawa aliyoitoa mwaka jana katika semina ya kimataifa, iliyoandaliwa na ubalozi wa China nchini.

Kupitia miundombinu bora, kutakuwa na kasi ya uanzishwaji wa viwanda kwani wakulima watapata urahisi wa kusafirisha mazao yao sambamba na kuwa na uhakika wa bidhaa kufika sokoni na hivyo hivyo kwa malighafi kwenda viwandani.

Lakini pia nishati ya umeme yenye uhakika, ni eneo lingine linalohitaji kufanyiwa kazi ipasavyo katika mchakato wa kukaribisha viwanda hivyo. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amekuwa akisisitiza juu ya hilo kwa kusema, ili Tanzania iweze kuwa nchi ya viwanda, nishati ya uhakika inahitajika.

Kutokana na fursa ya gesi nchini, Waziri Muhongo amekuwa akihimiza kampuni kuwekeza katika uzalishaji wa umeme unaotokana na gesi.

Miongoni mwa maeneo yanayohitaji uwekezaji katika kuzalisha umeme kwa kutumia gesi ni pamoja na Mtwara, Lindi, Somanga Fungu, na Mkuranga.

Msimamo wa Profesa Muhongo ni kwamba, hakuna nchi duniani iliyopiga hatua kimaendeleo bila kuwa na nishati ya uhakika ya umeme.

Hatua ya hivi karibuni ya Waziri Muhongo kuzuia Shirika la Umeme (Tanesco) kupandishwa kwa bei ya umeme, ni uthibitisho wa nia ya serikali kuhakikisha mikakati ya kujenga viwanda inatekelezeka. Rais John Magufuli ambaye amepongeza hatua hiyo ya kusitisha kupanda kwa bei ya umeme, anafafanua zaidi akisema, haiwezekani kupanga mikakati ya kujenga viwanda wakati umeme ukipanda.

“Namshukuru sana Waziri wa Nishati na Madini kwa maamuzi ya kusitisha hayo, kwa hiyo umeme hakuna kupanda bei,haiwezekani unapanga mikakati ya kujenga viwanda…,” Rais Magufuli alisema hayo kwenye ibada ya mwaka mpya, katika kanisa kanisa la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma, Kanisa Kuu Jimbo Katoliki la Bukoba, mkoani Kagera.

Ikiachwa viwanda ambavyo China itavielekeza nchini, pia vipo vinavyohitaji kufufuliwa ambavyo ukuaji na ustawi wake unategemea kwa kiwango kikubwa uwapo wa miundombinu pamoja na nishati ya uhakika ya umeme.