Mageuzi ya kiuchumi, kijamii Z'bar kuwa kweli 2020?

TANGU Wazanzibari walivyojiondoa kwenye minyororo ya utumwa wa kikoloni kwa kupindua utawala wa sultani Januari 12, 1964, wakiongozwa na Mzee Abeid Amaan Karume, wamewathibitishia Waarabu kwamba kulikuwa hakuna sababu ya kutawaliwa abadani.

Wakiwa katika umoja wao, Wazanzibari wamefanya kazi kwa bidii katika kuboresha uchumi na kubadilisha kwa kiwango kikubwa hali duni waliokuwa nayo wakati wakitawaliwa na mkoloni kwa mgongo wa sultani.

Serikali ya Mapinduzi ikiwa inafahamu inatakiwa kuimarisha zaidi hali ya kijamii na kiuchumi kwa watu wake, ilikuja na Dira ya Maendeleo ya 2020 ikilenga kukuza uchumi wa taifa na kuondoa umaskini kwa watu wake.

"Serikali ya Mapinduzi ilianzisha Dira 2020 ikilenga kukuza uchumi pamoja na kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa," anasema mmoja wa maofisa waandamizi wa serikali kutoka Wizara ya Kilimo.

Ofisa huyo pia anadokeza kuwa kuutokomeza umaskini kunahitaji, pamoja na mambo mengine, sera thabiti za uchumi zitakazosaidia kujenga fursa zaidi za ajira; elimu na mafunzo ambayo yatakuza uelewa wa wananchi katika ajira watakazochagua, uzalishaji, kazi na huduma muhimu za kijamii, ikiwa ni pamoja na afya.

Ofisa huyo anasema watu wanaoishi katika umaskini wanapaswa kupewa uwezo kupitia ushiriki watakaouchagua kwa uhuru wao katika nyanja zote za maisha; iwe ni kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Anataja mambo mengine muhimu katika kuondoa umaskini kuwa ni pamoja na kuwa na sera zinazolenga katika kupunguza tofauti ya walio nacho na wasio nacho na kuongeza fursa katika kuzifikia rasilimali.

"Dira pia inalenga katika kukuza maendeleo vijijini na kupeleka kila hatua zinazoboresha hali ya kiuchumi, kijamii na kimazingira kwa wananchi," anasema ofisa huyo.

Dira pia ina lengo la kutoa ulinzi wa kijamii kwa wale ambao hawawezi kujisaidia wenyewe; kutambua mahitaji na ujuzi wa wanawake; kuendeleza rasilimali watu na kuboresha miundombinu, ikiwa ni pamoja na vifaa vya mawasiliano.

"Zaidi ya yote, Dira 2020 imejielekeza katika kukuza sera za ndani ili kukidhi mahitaji ya msingi ya watu wote wa Zanzibar," anasisitiza ofisa huyo.

Anasema pengine kinachoweza kukwamisha Dira ni ukosefu wa hatua zinazofaa katika kushughulikia matatizo mbalimbali yaliyopo.

"Zinatakiwa hatua madhubuti ambazo zitabadilisha uchumi, kwa mfano, kutoka kilimo cha kujikimu hadi kilimo kikubwa cha kibiashara na ambacho ni cha kisasa," anasema mtaalamu huyo wa kilimo.

Kimsingi, Dira inajielekeza katika kutumia rasilimali watu ipasavyo katika kujiletea maendeleo kwa Wazanzibari. Dira ya Maendeleo Zanzibar 2020 inalenga kuboresha kiwango cha elimu ili kuiwezesha nchi kuhimili changamoto za karne ya 21 na wakati huo huo kuboresha ushirikishwaji wa sekta binafsi.

Chini ya dira hii, fursa zinatakiwa kuelekezwa pia kwa wanawake, kujenga fursa sawa kwa wote ikiwa ni pamoja na yatima, walemavu, wagonjwa na makundi mengine yenye matatizo sambamba na kutoa mwongozo juu ya mila na desturi za Zanzibar ili kukabiliana na wimbi la mabadiliko wakati wa mchakato wa maendeleo.

Muhimu zaidi, dira inasisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa mila na desturi za Zanzibar zinaendelea kuenziwa kwa vizazi vijavyo na kuhakikisha amani, utulivu wa kisiasa na uvumilivu wa kidini unaendelea kuwepo wakati wote.

Kwa ujumla, lengo kuu la Dira hii ni kwa Zanzibar kujiondoa katika umaskini na kujiletea maendeleo endelevu ya binadamu ifikapo mwaka 2020.

Hivyo inatarajiwa kwamba ifikapo mwaka 2020 jamii ya Zanzibar itakuwa imefikia malengo hayo kwa kiwango kikubwa na hasa kama itatalia manani mambo kadhaa yakiwemo haya yafuatayo: Kutokomeza umaskini uliokithiri; kuendeleza kilimo cha kisasa, viwanda, utalii na sekta za uzalishaji ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya soko na hali ya kiteknolojia.

Lingine ni kuiwezesha Zanzibar kuwa taifa la kiwango cha juu cha ubunifu, kujiamini na kujithamini, na zaidi ya yote, kuhakikisha kwamba Zanzibar inakuwa nchi ya amani, yenye utulivu wa kisiasa, utawala bora, uadilifu, umoja wa kitaifa na mshikamano wa jamii.

Kwa mujibu wa Dira ya 2020, Serikali ya Mapinduzi anataka kuwa na Zanzibar tofauti inayoendesha uzalishaji wa kisasa wa bidhaa na huduma ili kukidhi mahitaji ya msingi ya jamii na kufikia ushindani wa kimataifa katika sekta nyingi. Serikali ya Mapinduzi inalenga pia kuvutia zaidi wawekezaji wa moja kwa moja kutoka nje kwa lengo la kuwa na mtaji mkubwa, ambao utasaidia kuxalisha ajira.

Aidha, Dira hiyo ambayo utekelezaji wake ni wa kipindi cha miaka saba, inalenga katika kuongeza ukuaji wa uchumi wa Zanzibar kwa wastani wa asilimia 9 hadi10 ifikapo mwaka 2020 kutoka ukuaji wa asilimia 4.5 wakati Dira inaandaliwa.

Serikali ya Mapinduzi pia inatamani kuona Zanzibar ikiwa na kiwango cha juu cha ajira katika sekta ya kisasa. Dira pia inalenga kwamba asilimia 50 ya nguvu kazi ifikapo mwaka 2020 iwe imeajiriwa katika sekta ya utalii na maeneo huru ya kiuchumi, asilimia 20 katika kilimo na asilimia 30 katika sekta zilizobaki.

Kadhalika ina lengo la kuongeza pato la kila mwananchi hadi kufikia uchumi wa kipato cha kati, na hivyo kutokomeza umaskini uliokithiri.

Inatarajiwa pia kwamba uchumi mseto utakaotokana na kuanzishwa kwa viwanda vingi, utalii, biashara na ujenzi vitaongeza kwa kiwango kikubwa pato la taifa.

Kadhalika imedhamiriwa kwamba hadi mwisho wa kutekeleza dira hiyo, kiwango cha Mzanzibari kuishi kiwe kimeongezeka kutoka miaka 48 ya wakati dira inatayarishwa hadi 65.

Dira hiyo ina mambo mengi ikiwa ni pamoja na watu kupata maji safi, huduma za afya na kadhalika lakini kubwa ambalo wengi wanajiuliza ni kama sherehe za miaka 53 ya Mapinduzi leo zitazidi kuwa kichocheo cha kuhakikisha kuwa dira hiyo inatekelezwa ifikapo mwaka 2020.