Jamii inachangia migogoro ya walimu na wanafunzi

WAKATI nasoma shule za msingi na baadaye sekondari, mimi na wanafunzi wenzangu tuliwaheshimu sana walimu wakati mwingine kuliko hata wazazi wetu.

Nakumbuka, kuna siku mama alinizuia nisiende shule, na badala yake niende shambani kupalilia, lakini sikutekeleza agizo lake kwani nilitoroka na kwenda shule. Sikuwa tayari kukosa masomo lakini pia kukorofishana na walimu! Kwa kujua namna nilivyokuwa ninawaheshimu walimu, ilifikia mahala hata pale nilipofanya kosa nyumbani, wazazi wangu, hususani mama, alinitishia kunishitakia kwa walimu wangu.

Kusema hivi si kwamba nilikuwa siwaheshimu wazazi wangu, la hasha, bali nilikuwa nina hofu zaidi kuwakosea adabu walimu! Walimu wa miaka hiyo, walibeba dhima halisi ya uzazi hata kama kuna maneo walizidisha ukali na kuwafanya wanafunzi kuwa nao mbali, lakini ni ukweli pia kwamba mwanafunzi uliona fahari kumfanyia kazi mwalimu nyumbani kwake bila hata ya kushurutishwa wala kusukumwa.

Siyo wanafunzi pekee, bali jamii nzima, hususani maeneo ya vijijini, ilijenga utamaduni wa kuwasaidia walimu katika shughuli za shamba na nyingine kwani kutokana na kuwa mlezi muhimu, jamii ilimuona mwalimu anastahili kupata huduma hizo. Ingawa walikuwepo wachache wasio na maadili, lakini idadi kubwa ya walimu walikuwa ni wenye nidhamu ya hali ya juu, huku wakijituma vyema katika majukumu yao ya kufundisha na ulezi.

Wakiwa kiigizo kizuri kwetu, wanafunzi siyo tu kwamba tuliiga hata namna ya kuzungumza au kuvaa bali pia mambo mazuri waliokuwa wanafanya walimu. Hali hiyo ilitufanya miongoni mwetu tutamani pia kuwa walimu baada ya kuhitimu elimu zetu. Ninachokumbuka pia ni kwamba wazazi walikuwa wanajitokeza kwa wingi kuhudhuria mikutano ya wazazi inayoitishwa na shule kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo ya kielimu na hata nidhamu za wanafunzi.

Kwani zama zetu wanafunzi watoro pia walikuwepo na hata wakorofi lakini si kwa kiwango cha kupigana na mwalimu! Uchunguzi wangu unaonesha kwamba katika miaka ya karibuni hali imekuwa tofauti kabisa. Idadi kubwa ya waalimu hawaheshimiki na wanafunzi na hata wazazi na kama ambavyo wanafunzi hawavutiwi kuwa walimu, hata jamii pia haiwathamini waalimu. Jamii inaiona taaluma ya ualimu kama ajira mbadala baada ya mtu kukosa ajira zinazodhaniwa kuwa nzuri zaidi.

Kuna hii siku nilikuwa kwenye daladala naelekea kwenye kituo changu cha kazi jijini Mwanza, nikamsikia mwanamke mmoja aliyekuwa anaongea na ndugu yake kwa njia ya simu, akimlalamikia kuhusu kijana wake aliyehitimu elimu chuo kikuu kukosa ajira. Mwanamke yule alisema: “Yupo tu nyumbani, amekosa hata kazi ya ualimu”, hali inayoonesha kuwa jamii inaiona taaluma ya ualimu kama ajira mbadala.

Mimi ninayeandika makala haya na wewe unayesoma na yeyote tunayedhani kwamba amepata mafanikio baada ya kupita katika mfumo wa elimu, ni walimu ndio waliotufikisha tuliko leo. Kimsingi, waalimu ndio mambo yote kwani ndio wapishi wa kila taaluma. Mataifa makubwa, yamefanikiwa kufika yaliko leo kutokana na kuwekeza vya kutosha katika akili za vijana wao, kwa maana ya elimu.

Je, kwa nini ualimu unadharauliwa siku hizi kiasi hiki? Je, ni walimu wenyewe wamechangia au jamii? Je, ni kutokana na mshahara wanaolipwa labda ni duni kulinganisha na kada zingine? Je, ni kwa sababu ufisadi ulikuwa umetamalaki katika jamii kiasi cha kazi zisizo na rushwa kama ualimu kuonekana za hovyo? Nikirudi katika hadhi ya walimu, nimekuwa nikisikia na hata kushuhudia namna nidhamu waalimu wao ilivyoshuka kiasi cha kutisha.

Siku hizi kuna taarifa za wanafunzi kupigana na waalimu wao, wanafunzi kugomea adhabu na mbaya zaidi kuna taarifa pia za wazazi kuwajia juu waalimu kwa nini wanawaadhibu au ‘kuwafuatafuata’ watoto wao! Taarifa hizi za kuudhi zina upande wa pili wa shilingi wa mwalimu kumuonea mwanafunzi kwa kipigo kisichostahili, mwalimu kumpa mimba mwanafunzi, mwalimu kutotekeleza wajibu wake huku wengine wakijihusisha na biashara ikiwemo kuendesha bodaboda wakati wa kazi na kadhalika na kadhalika!

Nini hasa kimetufikisha hapa? Je, kuna kushuka kwa taaluma katika vyuo vya ualimu? Ni jamii imeoza au utandawazi umetuharibu na kuacha misingi mizuri ya mahusiano baina ya mwalimu na mwanafunzi na mwalimu na jamii yake? Tukio la mwaka jana la wanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Usevya iliyoko mkoani Katavi la kumshambulia mwalimu mkuu msaidizi wa shule hiyo, Makonda Ng’oka ni tukio linaloonesha matatizo yanayoikumba elimu.

Aidha tukio la hivi karibuni la wazazi katika wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa kumdhalllisha mwalimu Musa Mkalambosa wa Shule ya Msingi Kipanga kwa kumcharaza fimbo mbele ya wanafunzi wakimtuhumu kuwaadhibu watoto kwa kuwabebesha matofali ni tukio la udhalilishaji pia kwa walimu. Nimpongeze Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura kwa kutoa agizo la kukamatwa kwa wazazi hao ili wafikishwe mahakamani na kuagiza mwalimu aliyefanyiwa ukatili ahamishiwe kituo kingine cha kazi.

Katika tukio la Mwalimu Makonda ambapo pia walimu wengine walijeruhiwa baada ya kuvamiwa na wanafunzi wao, tuliona mamlaka zinazohusika na elimu zikichelewa sana kuchukua hatua. Pengine sasa ni wakati mwafaka kwa serikali kuimulika upya elimu yetu. Je, vyuo vyetu vinamjenga vyema mwalimu kimaadili kama mzazi na mtoa elimu na kumtengeneza kuwa mtu wa kuheshimika, siyo tu na wanafunzi, bali pia na jamii kwa ujumla?

Jamii pia inapaswa kumulikwa na kuona namna ya kuitengeneza iwaheshimu waalimu kama wazazi wenzao ambao ndio wanaokaa na watoto wao muda mwingi zaidi na kurejesha heshima ambayo miaka ile ilikuwepo. Wazazi wanaoshindwa kulea watoto katika maadili na wanaoungana na watoto wao katika maovu dhidi ya walimu ni muhimu washikishwe adabu na kila mtu ajue ili asije akarudia makosa. Mwalimu anapaswa kujijua kama mzazi wa pili na mzazi anapaswa pia kutambua hilo kwa asilimia 100.

Ni vyema pia bodi na kamati za shule ziongozwe na watu makini na wenye weledi ambao hawachaguliwi kutokana na umaarufu wao bali uwezo na ikiwezekana suala la elimu pia lizingatiwe. Katika zama hizi, labda kama amekosekana kabisa lakini nashauri ni vyema Mwenyekiti wa Bodi ya shule ya sekondari asiwe mhitimu wa darasa la VII. Nasema hivyo, kwa sababu mwenyekiti ‘msomi’ anaweza kutatua migogoro mingi ya shule kama vile wanafunzi wanapogomea mtihani wa majaribio ulio nje ya mitaala ya elimu au kugoma kufundishwa na mwalimu asiye na uwezo!

Taaluma ya ualimu ni taaluma nyeti na muhimu sana. Upatikanaji wa elimu bora unategemea mambo mengi ikiwa ni pamoja na mitaala bora, miundombinu imara, ikama inayotosheleza ya walimu, wanafunzi na utayari wa jamii wa kumruhusu mtoto kupata elimu. Lakini suala zima la maadili na mahusiano mazuri baina ya walimu na wafunzi pamoja na jamii, ni muhimu sana wakati wote.