Wambura: Wananchi someni HabariLeo mpate mambo halisi

“HABARILEO ni gazeti ambalo nalipenda sana. Ni gazeti zuri ambalo kimsingi linatoa habari za uhakika na za ukweli,” hii ni kauli ya Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura.

Anaendelea: “Kwa watanzania, ni gazeti linalowaletea matumaini kutokana na jinsi ambavyo linatoa habari za uhakika na za ukweli. Mtanzania yeyote anapilisoma gazeti hili anajisikia vizuri, anasikia amani moyoni. “Ni gazeti zuri na linapendwa na wananchi. Kama mtu unataka kutulia, unataka kupata habari makini na sahihi na ukiwa na amani moyoni basi soma gazeti la HabariLeo.”

Akizungumza katika mahojiano kuhusu maadhimisho ya miaka 10 ya HabariLeo, Naibu Waziri huyo anasema HabariLeo limekuwa ni gazeti ambalo limekuwa likiunganisha wananchi na serikali yao au serikali na wananchi wake kwa kuibua kero zinazoikabili jamii. Anafafanua kwamba yale masuala ambayo ni kero kwa wananchi mengi unaweza kuyaona kwenye gazeti hili na kuyafanyia kazi.

Anaongeza: “Kwa upande wa serikali masuala yote ya maendeleo ambayo yanafanyika serikalini yamekuwa yakiwafikia wananchi kwa usahihi zaidi kupitia Habari- Leo.” Wambura anatolea mfano wa kero ya nyaya za umeme ambayo ilikisumbua kijiji kimoja mkoani Tanga kwa miaka miwili, lakini baada ya HabariLeo kuandika kero hiyo, Shirika la Umeme nchini (Tanesco) ililiishughulikia kwa muda mfupi.

“Nimesoma pia habari ambayo mwananchi anashukuru baada ya Tanesco kutatua kero ya nyanya ambazo zilihatarisha maisha yao kwa miaka miwili, HabariLeo ndio iliyoibua tatizo hilo, na hii inaonesha kwamba gazeti hili linafanya kazi nzuri,” anasema. Anasema jambo ambalo anavutiwa nalo ndani ya gazeti la Habari- Leo ni matumizi ya lugha zenye staha na pia kupambwa na vichwa vya habari vyenye uhalisia na siyo vilivyoongezewa chumvi.

Kuhusu kwenda na ushindani, Wambura anautaka uongozi kuhakikisha HabariLeo linakuwa na habari nyingi zinazogusa maeneo mengi ya nchi pamoja na kuhakikisha kuwa linawafikia wananchi katika pande zote za nchi kwa haraka na kwa wakati.

“Vyombo vya habari ni vingi, lakini mmekuwa mkijitahidi kwa kadiri mnavyoweza. Najua mna changamoto kadhaa (ikiwemo ya ushindani sokoni), ingawa mnajitahidi pamoja na hali iliyopo. Ningeomba mjitahidi kuhakikisha mnakuwa na habari mpya kila siku na si mtu ategemee kuona habari mpya kutoka magazeti mengine.” “Lakini pia kuwa na uhakika wa ushindani ni pale ambapo mtakapowafikia wananchi kwa wakati. Siyo wenzenu wanapeleka gazeti saa tisa usiku na watu wanakuwa wameshapata habari za siku hiyo ninyi mnafika sokoni saa tatu asubuhi. Hakikisheni wenzenu wasiwatangulie katika habari kwani mnapopungukiwa habari watu watakimbilia magazeti mengine.”

Anaushauri pia uongozi kuhakikisha gazeti linafika pembe zote za nchi kwa wakati na kuibua matatizo yanayokabili jamii ya watanzania ili yaweze kufanyiwa kazi. “Magazeti mengine yanarahisisha kazi kwa kuwa na habari za mjini mjini tu, lakini mkiweza kufika vijijini, huko kuna mambo mengi si ya hatari tu (mabaya) bali pia yapo ya maendeleo na utamaduni ambayo yanaweza kuchochea maendeleo zaidi vijijini.

“Sasa mkiweza kufika vijijini mtaibua tamaduni ambazo zinachochea maendeleo, lakini pia ziko tamaduni ambazo wakati mwingine zinakwenda kinyume na mahitaji ya maendeleo au tuseme masuala ambayo ni hasi yanafanyika kule. Haya tuyakemee kwa nguvu zote.” Anatolea mfano wa masuala ya vifo vya mama akisema: “Kila siku tunasema mbona havishuki? Kumbe utakuta kule vijijini kuna desturi mbaya kama mama mjauzito kupigwa hovyo, siku mbili tatu anajifungua mtoto ameshafariki au hata yeye mwenyewe wakati anaenda kujifungua anapata matatizo kwa sababu alipigwa na kuumizwa.”

Anasema kuna masuala ya ukeketaji ambayo yanaendelea kwa siri katika baadhi ya maeneo hivyo analishauri HabariLeo kukayaibua kwa kuyaandika. “Masuala ya mila na utamaduni yana mchango mkubwa sana katika kuleta maendeleo, lakini utamaduni hasi unarudisha nyuma maendeleo,” anasema. Akizungumzia matazamio yake ya HabariLeo la miaka 10 ijayo, Wambura anasema anatamani kuona likiwa ni gazeti linaloongoza kwa kusomwa na wananchi wengi kuliko gazeti lingine nchini.

“Napenda kuiona HabariLeo ya miaka 10 ijayo ikiwa inaongoza kwa kusomwa na wananchi wengi, lakini ningependa muongeze vitu pia ndani ya gazeti. Ningependa masuala ya masomo ambayo yanaonekana ni tatizo katika jamii yaonekane katika HabariLeo. “Pia somo la Kiswahili. Kuna mambo madogo madogo ambayo ni makosa ya kawaida katika matumizi ya lugha ya Kiswahili yanayojitokeza wakati wa mazungumzo ya kawaida. Hata kwa waandishi wa habari na viongozi wanafanya makosa hayo. Ninataka HabariLeo lisahihishe jamii.

“Hivyo muwe na ushirikiano wa karibu na Bakita (Baraza la Kiswahili la Taifa). Naamini kwa kufanya hivyo mnaweza kuwasaidia wageni pia kusoma ili kupata kuelewa matumizi sahihi ya maneno na lugha ya Kiswahili, na hili litawasaidia hata wananchi wa kawaida. Wambura anasema anatamani kuona HabariLeo lijalo linaibua viwanda vidogo kwa lengo la kuinua uchumi ili kufikia azma ya serikali ya kuwa Tanzania ya viwanda.

“Unapozungumzia dhana ya viwanda kwa wananchi wengi wanadhani ni vile viwanda vikubwa sana, vinavyogharimu mitaji mikubwa. Kwa hiyo pengine uelewa wa wananchi kuhusu viwanda bado uko chini. “Ni wajibu sasa wa kuviibua viko wapi, vina changamoto gani, kwa sababu ziko changamoto zinazowakabili. Kwa kufanya hivyo tutaweza kuwasaidia kuongeza thamani ya bidhaa zao na thamani ya mazao ya kilimo,” anasema.

Aidha, Wambura anatumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania kusoma gazeti la HabariLeo kwa kuwa lina habari za uhakika na za kweli. “Sijawahi kusikia habari yoyote ya uchochezi, sijawahi kuona habari ambayo mtu akisoma anajenga uhasama na mtu fulani au na serikali yake. Ni habari ambazo tuseme ziko kati kati, haziegemei upande wowote na zina uhalisia wake. “Kimsingi mimi niwaombe wananchi wasome gazeti la Habari- Leo, kwa sababu linatoa mambo halisi,” anasema Naibu Waziri huyo mwenye dhamana ya michezo, habari, utamaduni na sanaa.