Upandaji miti utatuokoa na mabadiliko ya tabianchi

WATAALAMU wanasema mabadiliko ya tabianchi ambayo yana athari nyingi ikiwemo tunayoshuhudia sasa ya ukosefu wa mvua, yanasababishwa kwa kiwango kikubwa na binadamu mwenyewe.

Moja ya tabia ya binadamu inayosababisha hali hii ni watu kukata miti hovyo na kuiacha ardhi ikiwa haina uoto. Hali hii huongeza hewa chafu ya ukaa angani ambayo inaleta athari kubwa kwa viumbehai wote ambao wanakuwa katika hatari ya kutoweka katika uso wa dunia.

Wanasayansi wanatahadharisha kuwa dunia hivi sasa inapita katika tatizo kubwa la kubadilika kwa misimu ya mvua, kuongezeka kwa joto, ukame, mafuriko, kuongezeka kwa baridi, kuyeyuka kwa barafu kwenye maeneo kama Mlima Kilimanjaro kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira tunaoufanya. Utafiti umebaini kuwa viumbehai wa kuvutia kama ndege, mimea na wanyama siku moja wanaweza kufutika kabisa katika uso wa dunia kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa na binadamu ambao hivi sasa umeleta mabadiliko ya tabia nchi.

Aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Dk Teresia Huvisa aliwahi kuwaasa watanzania wote kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na hewa ukaa angani. Akasisitiza kuwa uharibifu wa mazingira ni janga la duniani ambalo linaviweka viumbehai njia panda. “Mimi kama Mwanamazingira nina wajibu wa kutoa tahadhari, siyo tu kwa watanzania bali Afrika nzima na duniani kote kwa ujumla.

Siku moja dunia inaweza kuangamia kama sisi sote hatutafanya juhudi za makusudi kupambana na mabadiliko ya tabianchi hasa kupanda miti kwa wingi,’’ alisisitiza Dk Huvisa. Kwa mujibu wa wanasayansi, shughuli mbalimbali za kibinadamu zimesababisha kuongezeka kwa joto la Dunia kwa asilimia 0.7 na kusababisha madhara yote yanayotokea hivi sasa duniani yakiwemo ukame, mafuriko na ongezeko la joto.

Hata hivyo, wanasayansi wanatahadharisha kuwa iwapo joto duniani litaongezeka hadi kufikia asilimia 1.5 ambalo ni ongezeko la asilimia 0.8, viumbehai wote waliopo duniani hawataweza kumudu kuishi. Utafiti wa wanasayansi unaonesha kuwa mwaka 2012 ongezeko la joto duniani lilikuwa 0.7, mwaka 2013 kiwango cha joto kilifikia 0.8 na kwamba kiwango cha joto kimeendelea kuongezeka na kufikia nyuzi 0.85c hadi kufikia mwaka 2015.

Kulingana na wataalamu wa mazingira, njia pekee ambayo inaweza kuinusuru dunia katika janga la mabadiliko ya tabianchi kwa upande wa nchi za huku kwetu ni kupanda miti ya kutosha kila mwaka na kupambana na watu wote wanaokata miti hovyo. Kampeni ya Kitaifa ya Upandaji Miti inaagiza kila halmashauri nchini kupanda miti 1,500,000 kila mwaka ili kupambana na ukataji miti hovyo ambao unafanyika katika maeneo mengi nchini.

Kwa kipindi cha mwaka 2005 hadi 2015 Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, ilipokea taarifa za upandaji miti kutoka mikoani, ambazo zilionesha kuwa miti 1,491,870,192 ilipandwa na kati ya hiyo miti 1,139,473,928 ilistawi, sawa na asilimia 76.2. Athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zinatokana na uharibifu wa mazingira zimeanza kujitokeza katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mtaalamu wa mazingira, Bugingo Bugingo anasema chanzo kikuu cha mabadiliko ya tabia nchi ni kuongezeka kwa hewa ukaa ambayo hutoboa blanketi lililoko angani (ozone layer) linalorekebisha mionzi ya jua kufika duniani. Anabainisha kuwa kutokana na kuharibika kwa tabaka hilo mionzi mingi zaidi inafika duniani na kurudi angani mara moja kuliko ilivyo kawaida, hali inayosababisha mabadiliko ya tabianchi yasiyotarajiwa ambayo yanaleta madhara kwa viumbe waishio duniani.

“Hewa ukaa inazalishwa kutokana na shughuli za kibinadamu katika viwanda vikubwa katika nchi zinazoendelea, usafiri na usafirishaji, shughuli za mashambani zinazohusiana na uharibifu wa mazingira kama vile ukataji wa miti hovyo na uchomaji moto,’’ anasema Bugingo. Moja ya athari za tabianchi ambazo zimejitokeza hapa nchini ni kuwepo kwa mvua za mawe ambazo zinaleta mafuriko ambayo yanasababisha vifo na kupotea kwa rasilimali nyingi na magonjwa.

Baadhi ya mikoa ambayo imeathirika na mabadiliko ya tabianchi ni Dodoma, Arusha, Manyara, Shinyanga, Simiyu, Kagera, Songwe na Mbeya. Kwa mfano katika Mkoa wa Songwe Tarafa ya Songwe, kuna majira fulani ya mwaka kunatokea giza kubwa linaloambatana na upepo wa vumbi zito mfano wa wingu la mvua ambalo linaendelea kuua ardhi mwaka hadi mwaka na kusababisha eneo hilo kugeuka kuwa nusu jangwa.

Katika Mkoa wa Shinyanga, mwaka juzi kulitokea mvua ya mawe iliyoambatana na upepo mkali ambao ulileta madhara makubwa kwa wananchi na kusababisha vifo vya watu 47 na kuharibu kaya za watu zaidi ya 400 ambao walipoteza kila kitu katika maafa hayo. Kwa mujibu wa sera ya Taifa ya misitu ya mwaka 1998, Tanzania ina karibu hekta milioni 33.5 za misitu ambapo theluthi mbili ya hekta hizo ipo mashakani kutoweka kutokana na ukosefu wa usimamizi mzuri, hali inayosababisha watu kuvamia na kuharibu misitu kwa ajili ya kilimo, malisho ya mifugo, kuni, mkaa, uchimbaji madini, ujenzi na shughuli nyingine.

Licha ya kwamba hakuna takwimu za kuaminika kuhusu kasi ya kutoweka kwa misitu, inakadiriwa kuwa hapa nchini ni kati ya hekta 130,000 hadi 500,000 za misitu zinazofyekwa kila mwaka, hali inayokatisha tamaa jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanahitaji miti ili kupunguza hewa ukaa.

Kulingana na wataalamu, moja ya sababu kuu zinazochangia kuendelea kuongezeka kwa hewa ya ukaa angani ni maendeleo ya viwanda ambavyo vinatoa moshi ambao unasambaa angani na kufanya uchafuzi mkubwa wa mazingira ya anga na moshi mwingi wa magari ambayo hayana viwango husababisha gesi ya ukaa kwenda moja kwa moja angani. Katika nchi ambazo zimeendelea magari yote ambayo yanatoa moshi mwingi kupita viwango, yanatozwa kodi kubwa, hali ambayo inasababisha wamiliki kushindwa kumudu kulifanya gari hilo kuendelea kutembea barabarani.

Hapa Tanzania hali ni tofauti kwa kuwa ni jambo la kawaida kuona magari mabovu ambayo yanatoa moshi mwingi yakitembea barabarani. Wataalamu wa mazingira wanaeleza kuwa misitu husaidia kufyonza hewa ya ukaa na hivyo inapokatwa husababisha kushindwa kunaswa na kufyonza kwa hewa hiyo chafu, hali ambayo inasababisha hewa hiyo kwenda angani na kuleta athari za kimazingira.

Mwanamazingira mahiri hapa nchini, Charles Meshark anasema misitu au miti ina nafasi kubwa zaidi katika kupunguza hewa ya ukaa angani. Kwa mujibu wa Meshark, misitu inapovunwa au kuharibiwa inachangia kwa asilimia kati ya 20 hadi 25 katika ongezeko la hewa chafu ya ukaa. Anasema misitu au miti inapovunwa au kukatwa, hewa chafu inakuwa haina pa kwenda zaidi ya kwenda angani na kusababisha athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia ya nchi.

Misitu ndiyo njia mwafaka katika kukabiliana na ongezeko la hewa chafu ya ukaa ambayo inaleta mabadiliko ya tabianchi na kuleta athari mbalimbali za kimazingira. Jambo muhimu ni watanzania kuhamasishwa kupanda miti kwa wingi kila mwaka, kuihifadhi na kuilinda miti na misitu, hali ambayo itawezesha Tanzania na dunia kwa ujumla kuwa mahali salama pa kuishi kwa kizazi cha sasa na kijacho. Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili mawasiliano baruapepe:albano.midelo@gmail. com,simu 0784765917