Miaka 40 ya CCM makali yawe yale yale ya 1977

NIANZE kwa kukipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutimiza miaka 40, umri wa mtu mzima tangu kuanzishwa kwake.

Kwa umri huo, chama kinapaswa kuonesha ukomavu, ushupavu na misingi imara katika kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia serikali na kuwasemea wananchi katika utatuzi wa kero zinazowakabili. Kabla sijafika mbali napenda nijulikane mapema kwamba mimi ni mwana-CCM kindakindaki. Historia ya ukombozi wa Tanzania ina uhusiano wa moja kwa moja na Chama Cha Mapinduzi. Hii ni kutokana na chama chetu kurithi mikoba ya vyama vya ukombozi vya Tanganyika na Zanzibar, yaani TANU na ASP.

Swali la kujiuliza ni je, CCM hii ni sawa na ile ya mwaka 1977 iliyotanguliza utu, uwajibikaji, uzalendo na maslahi ya umma wa wakulima na wafanyakazi? Je, chama kinaisimamia serikali kwa dhati na kwa maslahi ya taifa kama CCM ile ya 1977 au chama kinaihujumu serikali katika jitihada madhubuti za kuwaletea wananchi maendeleo? Je, viongozi wa chama na wale wa serikali wote wana nia njema ya kuiendeleza nchi kwa kushirikiana kwa dhati au ni urafiki wa kuviziana kama paka na panya, na unafiki wa kujinufaisha kwa mgongo wa chama?

Hakika ni kwamba, kati ya ‘wanaoisoma namba’ katika utawala wa sasa ni wana CCM kuliko wasio wana CCM. Wizi wa makontena bandarini, biashara za madawa ya kulevya, ujangili, watumishi hewa, vyeti feki, ubovu wa flow mita ya mafuta bandarini, ukwepaji kodi, uporaji ardhi, safari za nje ya nchi za viongozi na kadhalika hakuna ubishi kwamba makada wa CCM walinifaika pia.

Kwa hiyo serikali ya awamu ya tano inapotumbua majipu, wahanga ni wakosaji bila kuangalia ni wafuasi wa chama gani lakini bila shaka wana-CCM waliokuwa wamesahau misingi ya chama hiki ndio waathirika wakubwa zaidi. Rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, kukosekana kwa uwajibikaji na kubebana vilikifanya chama kipoteze mvuto kwa jamii, lakini bila shaka kila mtu anaona kwamba hakuna tena mchezo mchezo ndani ya serikali na kwenye chama chenyewe.

Mwaka mmoja baada ya uchaguzi, tusipuuze yaliyotukumba mwaka 2015 katika uchaguzi ule. Pongezi kwa Mwenyekiti wa sasa chama chetu kwa kujipambanua kwamba yeye ni mzalendo, muadilifu na mwajibikaji. Swali linabaki kwamba, sisi wanachama tuko tayari kubadilika na kukitumikia chama na rasilimali zake kwa manufaa ya umma na si matumbo yetu?

Napendekeza tuyatumie maadhimisho ya mwaka huu kwa kuunga mkono juhudi za Mwenyekiti wetu, John Magufuri kuiunda CCM iwe ile inayotetea maslahi ya wakulima na wafanyakazi wa nchi hii. Ni wakati wa kukijenga chama chetu kinachokubalika kwa watanzania hasa wa kada za chini, wakulima na wafanyakazi. Baada ya uchaguzi wa 2015, na kupata ushindi tusijisahau bali uchaguzi wa mwaka huu ndani ya chama ulenge kubadilisha taswira ya chama chetu zaidi kwa kuwafanya wananchi wakione ni mali yao.

Mshairi mashuhuri nchini Tanzania, Mzee Charles Mloka katika kitabu ‘Diwani ya Mloka’ mnamo tarehe 18/06/1982, aliwakumbusha wana-CCM kukijenga chama imara kwa kuondoa viongozi wala rushwa, wabadhirifu na wahujumu uchumi kwa manufaa ya umma.

Maudhui ya shairi hilo yalinukuu wito wa Mwalimu Julius Nyerere alioutoa jijini Arusha kwa wana CCM. Shairi hilo liitwalo Wito Wake Mwenyekiti’ linasadifu kwa sasa wito wa Mwenyekiti mpya wa CCM, John Magufuli mwenye dhamira ya dhati kuitakasa CCM ili ichochee maendeleo ya Tanzania. Tujikumbushe kwa kulisoma na kuyazingatia maudhui ya shairi hilo ili kukidhi matakwa ya siasa kwa sasa.

1. Rejeeni ya mwalimu, aliyosema Arusha, Viongozi wahujumu, acheni kuwapitisha, Uchaguzi ukitimu, wambieni wamekwisha, Wito wake Mwenyekiti, mikoani mtimize.

2. Naanza na Morogoro, nafika hadi Kinole, Kilosa na Kilombero, Matombo hamuwasile, Waluguru wapogoro, viongozi Msagule, Wito wake Mwenyekiti, mikoani mtimize.

3. Ndugu zangu Wazaramo, Pwani hamsindile, Endelezeni kilimo, lakini kuno mulole, Viongozi wa milomo, kura msiwagolele, Wito wake Mwenyekiti, mikoani mtimize.

4. Jirani zangu Dodoma, Wayangu mliwaswano, Japo shida zawakama, tuonesheni mfano, Ya kwamba mtawalima, viongozi wa maneno, Wito wake mwenyekiti, mikoani mtimize.

5. Kamwene hapo Iringa, mliwanofu salamu, Na mbeya sikuwatenga, mgonile wasalamu, Kura zenu mkifunga, msiwape wadhalimu, Wito wake mwenyekiti, mikoani mtimize.

6.Mnapilika Mtwara, habari ya kuliyamba, Kusini tuwe imara, wito huu kuupamba, Warushaji kwetu dhara, wala tusiwape namba Wito wake Mwenyekiti mikoani mtimize.

7. Na somo tulio Lindi, twende twende wajamaa Waliokishiba Lindi, lazima kuwakataa, Tuwape wale ushindi, chama wasokihadaa, Wito wake Mwenyekiti, mikoani mtimize.

8. Wangoni huko Ruvuma, tuwaone kina Bambo, Japo mngali mwalima, Mloka nawapa fumbo, Kura zenu mkituma, msiwape shiba tumbo, Wito wake Mwenyekiti, mikoani mtimize.

9. Mashujaa wa Kagera, Mloka niwagambile, Iwe msiwape kura, viongozi ‘ija tule’ Wachagueni imara, matunda yao tuyale, Wito wake mwenyekiti, mikoani mtimize.

10. Nakwenu huko Kigoma, Rukwa na hata Tabora, Singida narudi nyuma, Kilimanjaro na Mara, Viongozi wenye njama, msiwape zenu kura, Wito wake Mwenyekiti, mikoani mtimize.

11. Kaditamati Arusha, Mwanza na kule Shinyanga, Unguja najumuisha, na Tanga naweka nanga, Viongozi rusha rusha, kura wapigeni chenga, Wito wake Mwenyekiti, mikoani mtimize.

Mwandishi wa makala haya aliyemalizia kwa shairi la Charles Mloka ni Mwalimu wa Lugha, Fasihi na Uraia wa shule ya sekondari Kibaha. Mawasiliano yake ni 0718 495949 au shageofrey@yahoo. com