OLD BOMA: Ngome ya Wajerumani iliyogeuka kivutio cha utalii Mtwara

MJI mkongwe wa Mikindani, Manispaa ya Mtwara una vivutio lukuki vya utalii wa malikale na utamaduni ambavyo vinamwezesha yeyote kujifunza mengi katika historia ya Tanzania.

Katika eneo la Mikindani kuna jengo kongwe la Old Boma lililokuwa makao makuu ya serikali ya Wajerumani, kanda ya kusini. Historia inaonesha kuwa jengo la Old Boma lilijengwa na wakoloni hao mwaka 1895 na kwamba ujenzi wa jengo hilo lenye ghorofa iliyojengwa bila nondo isipokuwa kwa kutumia mawe matupu yaliyokuwa yanaokotwa baharini ulianza rasmi mwaka1890.

Taarifa zinaonesha kwamba Wajerumani walianza kulitumia rasmi jengo hilo mwaka 1895 na lilitumika kwa matumizi manne; utawala, kwa ajili ya chakula na kulala, kwa ajili ya ulinzi na pia kama mahakama. Kwa ujumla jengo la Old Boma lilitumika katika kipindi chote cha utawala wa Wajerumani hadi mwaka 1916 walipofika watawala wengine ambao ni Waingereza ambao waliendelea kulitumia kwa madhumuni yale yale manne kama ilivyokuwa kwa Wajerumani.

Kulingana na historia ya jengo hilo, ilipofika mwaka 1947 Waingereza waliamua kuhamisha makao makuu kutoka Mji Mkongwe wa Mikindani na kuyapeleka katika bandari ya Mtwara Mjini ambayo ina kina kirefu cha bahari cha asili, hivyo kuwezesha meli za ukubwa wowote kuingia ukilinganisha na mji wa Mikindani ambao ulikuwa shida kuingia meli kubwa. Jirani ya jengo la Old Boma kuna jengo alilofikia Mpelelezi mashuhuri, Dk David Livingstone na kuishi hapo kuanzia Machi 24 hadi Aprili 7 mwaka 1866.

Mpelelezi Dk Livingstone aliwahi kunukuliwa katika kumbukumbu zake akisema kuwa mji wa Mikindani ni moja ya zilizokuwa bandari nzuri katika mwambao wa pwani, kabla ya kujaa mchanga hivyo kushindwa kuendelea kutumika kwa shughuli za kibandari. Ujenzi wa bandari ya Mtwara ulikamilika mwaka 1957 hivyo Waingereza walihamisha serikali kutoka mji wa Mikindani na kuhamia katika bandari ya Mtwara na kuanzia hapo matumizi ya jengo la Old Boma yalianza kupungua umuhimu na umaarufu wake.

Baada ya kupata uhuru mwaka 1961 jengo la Old Boma lilikabidhiwa serikalini na kutumika kama Kituo cha kwanza cha polisi. Wajerumani walipoamua kujenga jengo la Old Boma waliamua mahali hapo pawe ndiyo Makao Makuu yao ya Kanda ya Kusini hasa kutokana na mahali hapo kuwa juu hivyo kufaa kwa ulinzi na usalama.

Hata hivyo, wakati jengo hilo linatumika kama Makao Makuu ya Polisi lilianza kuharibika kutokana na kukosa kufanyiwa ukarabati hatimaye mwishoni mwa miaka ya 1980 serikali iliacha kulitumia kwa kuhofia usalama wake, hali iliyosababisha jengo hilo kubakia kama gofu. Mwaka 1997 Muingereza mmoja anayeitwa Barayan Carl alifanya mradi unaoitwa Trade Aid Tanzania na kuamua kukarabati jengo hilo.

Muingereza huyo akiwa katika safari zake za kitalii alifika katika eneo hilo la Mikindani na kutembelea jengo la Old Boma, baada ya kupata historia yake na kuona jengo limechakaa alipendezwa na historia yake hivyo aliamua kulifanyia ukarabati jengo hilo. Lengo la muingereza huyo baada ya kumaliza ukarabati ni kulitumia kwa lengo la kuinua utalii katika mji mkongwe wa Mikindani baada ya kupata historia kuwa serikali ya kwanza ilitokea katika jengo hilo.

Barayan alifanya taratibu zote za kuingia mkataba wa ukarabati wa jengo hilo na serikali kwa kipindi cha miaka 20 kati Tanzania na Trade Aid ambapo ukarabati huo ulimalizika mwaka 2000 na jengo hilo kuanza kutumika kama hoteli ya utalii na kujifunzia historia. Msimamizi na Meneja wa hoteli ya Old Boma, John Zomali anasema lengo la hoteli hiyo ni kuhakikisha kuwa wanajamii wa Mikindani wanapewa kipaumbele kwa kunufaika na hoteli hiyo ambapo baadhi ya wafanyakazi wa hoteli hiyo wametoka katika jamii ya Mikindani.

“Hoteli hii inategemea zaidi wageni ambao ni watalii kutokana na mazingira na asilia ya jengo la Old Boma ambalo limejengwa na Wajerumani, hivyo watalii wanapofika wanapenda sana kushangaa jengo hilo la ghorafa lililojengwa miaka mingi kwa mawe ya kuokota baharini, chokaa na udongo, tena bila kutumia nondo na ubora wake upo vilevile,’’ anasisitiza Zomali. Zomali anabainisha kuwa wageni wengi wanaofika katika hoteli hiyo ni watalii ambao wanaweza kumudu bei na kwamba kwa wastani Old Boma inapokea watalii wengi kuanzia mwezi wa Juni, Julai, Agosti, Septemba na Desemba.

Wananchi wa Mikindani wanafurahia uboreshaji wa mji huo kuwa sehemu ya utalii kutokana na kunufaika na mambo mbalimbali ikiwemo ajira, kufanya biashara na pia wanapata marafiki ambao baadhi yao huwachukua kwenda Ulaya na kwamba baadhi ya wanafunzi wa Mikindani wanapata ufadhili wa kwenda kusoma. Zomali anasema jamii ya Mikindani pia inanufaika na mradi wa kufundisha lugha ya Kiingereza bure na kutoa mikopo midogo kwa wafanyabiashara wa eneo hilo.

Katika kuhakikisha kuwa utalii wa mji mkongwe wa Mikindani unatan gazwa duniani kote tayari Old Boma imefungua tovuti yake inayoitwa www.mikindani.com ambayo imeutangaza kikamilifu mji huo na mkoa wa Mtwara kwa ujumla. Amevitaja baadhi ya vivutio ambavyo vimewekwa katika tovuti hiyo kuwa ni pamoja na maeneo mazuri ya kuogelea kama Msimbati, mto Ruvuma ulioko mpakani ambako watalii wanaweza kuangalia wanyama kama viboko ambao ni kivutio kikubwa cha utalii.

Ukiacha jengo hilo la Old Boma, jirani na jengo hilo kuna majengo mengine yenye historia ya kipekee kusini mwa Tanzania yakiwemo soko la watumwa, ambalo hivi sasa limekarabatiwa na baadhi ya maeneo kukatwa vyumba na kuwapatia wanajamii wa Mikindani wanaofanya biashara ndogo ndogo katika soko hilo.

Wananchi hao wanalipa pesa kidogo kama mchango wao hata hivyo wao ndiyo wanaonufaika kufanya biashara ndogo ndogo na kuendeleza maisha yao katika eneo hilo lenye kivutio cha kipekee kwa utalii hasa katika kipindi hiki cha ugunduzi wa gesi asilia mkoani Mtwara. Hamisi Salum (75), mkazi wa mji mkongwe Mikindani anasema baada ya kukarabatiwa jengo la Old Boma limekuwa na hadhi ambayo inavutia watalii wengi kufika hivyo kuongeza mapato na fedha za kigeni ambazo zinachochea maendeleo.

Mji wa Mikindani unafahamika na wengi kutokana na historia mji huo ilikuwa ni bandari ya kwanza ya mwambao wa kusini mwa Tanzania na unabaki kuwa mji mkongwe kama ilivyo Kilwa, Bagamoyo, Pangani, Lindi na Mafia. Unapofika katika mji wa Mikindani unaona fukwe nzuri pamoja na nyumba zilizojengwa na mawe yaliyookotwa toka baharini. Mji huo ulikuwa ni muhimu kibiashara kuanzia karne ya 15.

Isa Ramadhani (86), mwenyeji wa mji huu anasema ujenzi wa kutumia mawe katika majengo ya zamani kwenye eneo hili yanathibitisha utamaduni wa ujenzi wa Kiarabu. “Hapo ndipo ilipokuwa ngome ya Wajerumani na sasa inajulikana kama Hoteli ya Old Boma, kwa ujumla ghuba ya Mikindani ni kubwa. Ni bandari ambayo imetunzwa vizuri katika ukanda wa kusini, ni rahisi pia kuzifikia fukwe bora na hifadhi za viumbe wa baharini,’’ anasema.

Serikali ya awamu ya tano Januari mwaka huu imeuagiza uongozi wa Mkoa wa Mtwara kuhakikisha kwamba inawaondoa watu wote wanaoishi katika magofu ya kale ya mji wa Mikindani. Utafiti umebaini kuwa majengo hayo yanaonekana kuwa ni hatarishi kwa maisha yao ambapo hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wote ambao wamekaidi maagizo ya serikali ya kuhifadhi maeneo ya kale hususani kuendesha ujenzi bila vibali halali ndani ya mji huo.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani amekagua Mji mkongwe wa Mikindani na kubaini kuharibika kwa baadhi ya majengo yenye utajiri wa utalii wa kiutamaduni na mambokale. “Kuna haja ya serikali kuchukua hatua za makusudi ili kunusuru majengo hayo ambayo ni moja ya kivutio cha watalii hususani katika maeneo ya kusini,’’ anasisitiza.

Milango ya utalii katika Mkoa wa Mtwara hivi sasa imefunguka hasa baada ya ugunduzi wa gesi asilia. Mkoa huo una wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi ambao watatembelea vivutio vya utalii kama Old Boma na kuongeza kipato na fedha za kigeni. Mwandishi wa makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili mawasiliano baruapepe:albano.midelo@ gmail.com. Simu 0784765917