Wafungaji bora haoo! Wanavutana mashati

LIGI msimu huu si mchezo. Wakati timu mbili zikipambana kwa pointi kuongoza usukani kwenye msimamo wa ligi, washambuliaji nao hukimbizana katika ufungaji wa mabao kuwania kiatu.

Mpaka sasa michezo 20 imechezwa na timu zinaelekea katika mchezo wa 21 mwishoni mwa wiki hii. Kila mechi washambuliaji nao hupambana kuweka rekodi zao za ufungaji na ikiwezekana kuchukua kiatu cha ufungaji bora. Inaonekana dhahiri kuwa mambo ni magumu kwa washambuliaji awamu hii hasa katika klabu za Yanga, Simba na Azam FC ambao wanaongoza katika orodha ya wafungaji bora.

Ugumu wa kushindwa kufunga mabao mengi na kuvutana mashati ni kutokana na timu pinzani msimu huu kuonekana kuwafahamu vizuri wabaya wao na kuwazuia wasipenyeze kwenye nyavu zao. Katika orodha ya wafungaji inaonesha wazi kuwa washambuliaji watatu wanavutana mashati wakifanana kwa idadi ya mabao tisa kila mmoja. Amis Tambwe na Simon Msuva wa Yanga, Shiza Kichuya wa Simba wote wana magoli tisa.

Je, ni nani atakayempon- yoka mwenzake siku zijazo na kuongoza msimamo wao? Bila shaka hakuna anayejua kwa sababu kuna michezo mingi mbele na yeyote anaweza kuibuka. Aidha, wenye magoli nane ni Donald Ngoma wa Yanga na John Bocco wa Azam FC. Wafungaji hao ni kabla ya mechi za kuanzia jana (Ijumaa) na matokeo ya leo na kesho. Bado wachezaji hao wanaweza kushuka au kupanda kutokana na mechi za mwishoni mwa wiki hii au zijazo.

Sijawataja baadhi ya wengine wenye magoli saba pia wapo wengi na wanaweza kupanda wakati wowote. Kutokana na wafungaji hao kutoachana mbali kwa idadi ya magoli mpaka sasa ni vigumu kutabiri nani atakuwa mfungaji bora msimu huu kwani mambo yanaonekana ni magumu kwao. Na ugumu huo unaweza ukawa ni matunda kwasababu ni lazima kila mmoja atapambana kuponyoka alipo na kuingia sehemu nyingine kwa kuhakikisha anafunga zaidi.

Katika baadhi ya mechi za karibuni Bocco anaendelea kupanda kiwango baada ya kufunga mchezo uliopita dhidi ya Simba bao pekee lililowapa pointi tatu. Bocco ni mshambuliaji asiyetabirika. Kuna wakati yuko vizuri na muda mwingine yupo kama hayupo lakini ni mchezaji mwenye uwezo wa kubadilisha matokeo wakati wowote katika timu yake. Kwa baadhi ya wengine kumekuwa na ubutu wa kutofunga mara kwa mara kama Tambwe, Kichuya na Ngoma ambaye hakuwepo kutokana na matatizo ya kifamilia.

Hawajafunga licha ya kupata nafasi za kucheza katika baadhi ya mechi. Hali hiyo inawafanya mashabiki wa soka wajiulize kunani tena kwao? Kidogo kwa Msuva ambaye amekuwa akijitahidi kupambana kwa kila mchezo na kupata bao. Viungo na mawinga wamekuwa wakitengeneza historia nyingine katika ufungaji kwa mfano Deus Kaseke, kiungo mshambuliaji Mohamed Ibrahim wa Simba na wengine ambao sijawataja.

Wapo washambuliaji waliovuma raundi ya kwanza kama Laudit Mavugo, Ibrahim Ajibu, hawajaweza kufumani nyavu kwa muda mrefu kiasi cha kudhaniwa huenda wameshuka kiwango bila kumsahau Antony Matheo ambaye hajafunga muda mrefu. Labda kwa kuwataja baadhi yao kama Matheo na Ajibu ambao hawakupata nafasi ya kucheza mara kwa mara huenda kukawa ni sababu ya kushindwa kufumania nyavu na kuona thamani yao.

Chirwa naye alianza kusahaulika kutokana na kutopata nafasi tangu kuwasili kwa Kocha mpya Mzambia George Lwandamina. Lakini baada ya kukaa nje muda mrefu aliamka katika mchezo uliopita dhidi ya Mwadui kwa kuifungia timu yake mabao mawili pekee yaliyoipa Yanga ushindi wa 2-0 . Mavugo ana mabao manne wakati Ajibu ana mabao matatu bado wana kazi ya kupambana na kuzisaidia timu zao kufanya vizuri. Kwa sasa ninaweza kusema ni mapema kutabiri mfungaji bora kwa sababu wachezaji hao hubadilika.

Leo anavuma Tambwe kesho Bocco pengine kiatu kikaangukia kwa kiungo mshambuliaji au mkabaji. Licha ya washambuliaji hao kuvutana mashati kwa idadi ya magoli, bado wale wa Yanga watasifiwa kwa kusaidia timu yao kufikisha jumla ya mabao 42 mpaka sasa. Yanga inaongoza kileleni kwa idadi kubwa ya mabao ikionesha wazi kuwa safu yao ya ushambuliaji ni bora ukilinganisha na nyingine. Ikifuatiwa na Simba ambapo imefunga magoli 30 katika michezo 20.

Kuna utofauti mkubwa kutoka anayeongoza hadi nafasi ya pili inayoshikiliwa na wekundu hao. Ikifuatiwa na Kagera Sugar, Azam FC na Mtibwa ikifanana kwa idadi ya mabao 24. Bado kuna kazi kwa timu nyingine kuifikia Yanga katika idadi hiyo ya magoli.

Kujua zaidi nani atakuwa mkali wao wa kufunga inahitaji jitihada za mchezaji mwenyewe kuonyesha uwezo kwa kufunga mabao mengi. Siri pekee ya mshambuliaji kufanya vizuri ni juhudi binafsi na kushirikiana na wenzake. Washambuliaji wengi wakishapata umaarufu kidogo na sifa basi hujisahau na kuwa wavivu badala ya kuongeza juhudi katika kufikia mafanikio yao.