Tutumie rasilimali zetu kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo

MIAKA minne iliyopita Halmashauri ya Jiji la Mwanza ilisaini mkataba na Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) kwa ajili ya kuweka nyasi bandia kwenye uwanja mkongwe wa mpira wa Nyamagana ulioko jijini Mwanza.

Mkataba huo ambao pia ulishuhudiwa na Rais wa wakati huo wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, FIFA ilitoa kiasi cha dola za Marekani 500,000 huku uongozi wa jiji la Mwanza ulitakiwa kuchangia dola 118,000 ili kufikisha 618,000 za mradi huo. Tangu kusainiwa kwa mkataba huo zimekuwepo taarifa zinazotofautiana za kusafirishwa kwa nyasi hizo bandia kuja hapa nchini ili ziwekwe kwenye kiwanja cha Nyamagana na zingine katika Uwanja wa Kaitaba ulioko mkoani Kagera.

Mengi yalizungumzwa juu ya viwanja hivyo kuwekewa nyasi bandia, huku baadhi ya wadau wa soka na wadau wa michezo wakiona ni fahari sana kwa viwanja vyetu hivyo kuwekewa nyasi hizo. Swali kuhusu Nyasi bandia Nimejiuliza maswali mengi kuhusu hoja hii ya viwanja vyetu kuondolewa nyasi za asili na kupandikizwa nyasi bandia na kufanya tuwe na viwanja vyenye nyasi bandia (artificial pitches). Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo imekuwa ikifanya mambo bila ya kufanya utafiti wa kina.

Nasema hivi kwa sababu, kama nchi tumetumia fedha nyingi za walipa kodi kwa kusafirisha nyasi hizo za kutengenezwa kutoka nje ya nchi. Ni bahati mbaya sana, jambo hilo liliungwa mkono na watu wengi wakiwemo wanaofanya maamuzi kwenye sekta ya michezo, ambao bila hofu waliafiki ujio wa nyasi hizo bila kufahamu kuwa nyasi hizi zinatumika kwenye nchi zenye hali ya hewa ya baridi.

Lakini baada ya kufanya uchunguzi wa kina juu ya hoja hiyo, nimegundua kuwa na kiwanja kimoja au viwili vinavyotumia nyasi bandia hapa nchini zina madhara makubwa ya kimazingira na kiuchumi. Madhara ya nyasi bandia Kwa kawaida nyasi bandia zina muda maalumu wa kutumika na ukiisha inabidi zitupwe au ziteketezwe kitaalamu ili zisiweze kuharibu mazingira na kusababisha madhara kwenye viumbe hai. Kuna aina nyingi za nyasi bandia ambazo zinatumika kulingana na muda wa matumizi yake.

Zipo zinazotumika kwa muda wa miaka mitatu hadi mitano kama uwanja unaohusika ni ule unaotumika kwenye michezo ya ndani (indoor games) ili kuzuia madhara ya uharibifu wa mazingira ambayo yanayoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na kwa wachezaji. Lakini zipo zinazotumika kwa muda wa miaka miwili, mitatu hadi sita kutegemea ni namna gani nchi ina uwezo wa kutunza viwanja vya aina hiyo kwa kuangalia mabadiliko ya tabianchi.

Inadaiwa pia kuna viatu maalumu ambavyo hutumiwa na wachezaji watakaokuwa wakicheza mpira na michezo mingine kwenye viwanja vya aina hiyo, ambavyo itabidi hapa nchini vitengenezwe au viagizwe. Muda wake wa kutumika ukiisha inabidi zikusanywe na kutupwa kama uchafu au ziteketezwe kulingana na teknolojia ya kisasa ya uteketezaji wa nyasi za aina hiyo ambayo sina hakika kama tunayo hapa nchini. Na hata kama zikitupwa baadhi zitakuwa na madhara makubwa ya uharibifu wa mazingira na afya ya viumbe hai.

Pili, tutaagiza nyasi hizo kwa fedha zipi kama hatua ya awali ya kupata nyasi hizo ambazo zimeingia nchini kwa kuchelewa kinyume na mkataba uliosainiwa kati ya Jiji la Mwanza (Nyamagana), TFF na FIFA. Kusafirisha nyasi bandia kutoka nje ya nchi na kuzileta katika uwanja wa Nyamagana ni jambo ambalo halikufanyiwa utafiti wa kina. Kuchukuliwa kwa nyasi hizo kunaonesha jinsi taifa tunachukua malighafi za kutengeneza kutoka nchi zilizoendelea, ambazo zimekosa mahali pa kuzihifadhi au kukosa jalala la kutupia.

Nchi hizo zina msisitizo mkubwa wa kulinda na kuhifadhi mazingira yao na mataifa makubwa duniani mengi yao yana viwanja vichache sana vya nyasi bandia kwa ajili ya wanamichezo wao. Nyingi ya klabu kubwa duniani hazina viwanja vya nyasi bandia bali vimepandwa nyasi za asili! Baadhi ya viwanja hivyo vilivyopandwa nyasi za asili ni pamoja na kiwanja cha Manchester, St Mary’s Southampton, Britania, Aston Villa na vingine vingi.

Nyasi za asili ambazo tungezipanda sisi wenyewe kwa kutumia wataalamu wetu wengi tulio nao zinabadilishiwa matumizi kulingana na muda wake wa kupandwa na matumizi, je hizi za bandia zikichoka tutapata wapi nyingine za kubadilisha. Gharama ya kuzitunza na kuzihifadhi hizo nyasi bandia baada ya muda wake kumalizika itatoka wapi? Na zitaenda kutupwa wapi maana haziozi?

Au ndio utakuwa mwanzo wa kutengeneza dampo nyingi kwa ajili ya kutupwa kwa nyasi hizo za bandia, ambazo naamini pia hata tekonolojia ya kuziteketeza ina gharama kubwa. Lakini hivi ni kweli Tanzania nchi yenye wataalamu wengi wa kilimo na maua inashindwa kuwatumia watalaam wake katika kupanda nyasi za asili na kuvisimamia viwanja hivyo?

Uwanja wa Nyamagana Uwanja wa Nyamagana ambao uko umbali wa nusu kilometa kutoka ndani ya ziwa Victoria ungeweza kupitia kwa watalaam wetu nyasi za asili zikapandwa na zikatoa ajira kwa vijana wetu Uwanja wa CCM Kirumba miaka ya 80 -90 ulikuwa ni miongoni mwa viwanja vizuri kwa nchi za Afrika Mashariki, baada ya kuajiri watu wakishirikiana na watalaam ambao walikuwa wanang’oa magugu sanjari na kumwagilia maji uwanja huo.

Nakumbuka wakati fulani uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza ulikuja na mawazo ya kuubadilisha uwanja huo matumizi, ambapo ulimtafuta mwekezaji kwa ajili ya kujenga viwanja vingi vya michezo kwa ajili ya michezo ya ndani (indoor games). Ujenzi huo ulihusisha pia uboreshaji wa uwanja wa mpira wa Nyamagana ili kuwezesha jiji la Mwanza kupata mapato na wakati huo huo kuboresha mchezo wa soka na michezo mingine kupitia uwekezaji huo.

Lakini hoja hiyo ilipingwa vikali na baadhi ya wanasiasa na wadau wa soka ambao baadhi yao inadaiwa walikuwa wanapata mapato kupitia uwanja huo huku baadhi ya wanasiasa wakivuna uongozi kupitia hoja hiyo. Vinginevyo nakubali hoja ya uwekezaji huo ambao ungeifanya uwanja huo kuwa na muunganiko wa michezo mingi (indoor games) kama kikapu, tenisi, wavu na mingine mingi ukiwemo mpira wa mguu.

Michezo hiyo ingeweza kutoa ajira kwa watu wengi, lakini pia ungeongeza mapato kwa klabu ya michezo ya Nyamagana na kwa uongozi wa jiji la Mwanza. Tusiwe haraka kupokea bidhaa kama za nyasi bandia na nyingine zinazotolewa na nchi za kigeni kabla hatujazifanyia utafiti wa kina na kuacha kutumia bidhaa zetu za asili ambazo hazina gharama kubwa. Bado naamini kwa kuwatumia wataalamu wetu tulio nao tunaweza tukavijenga viwanja vyetu vya michezo nchini, sio Nyamagana peke yake kwa kutumia nyasi za asili, tusikubali kuwa dampo la kupokea uchafu kutoka nchi za kigeni.