Pumzika kwa amani David Burhan

WIKI hii ilikumbwa na huzuni hasa kwa mashabiki wa soka nchini baada ya kumpoteza golikipa wa Kagera Sugar, David Burhan.

Golikipa huyo alifariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita katika hospitali ya rufaa ya Bugando mkoani Mwanza alipopelekwa kwa matibabu zaidi baada ya hali yake kuwa mbaya katika hospitali ya kiwandani huko Kagera. Awali, kabla ya umauti kumkuta ilidaiwa alikuwa akisumbuliwa na tumbo na baadaye macho yake yakageuka na kuwa ya njano na ndipo hali ikazidi kuwa mbaya zaidi kwa kadiri muda na siku zilivyokuwa zinasogea.

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime anasema mchezaji huyo alianza kuumwa tangu wakiwa wanakwenda kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho (FA Cup) mkoani Singida na alikuwa acheze siku hiyo kwenye kikosi cha kwanza. “Tulienda naye Singida na nilitarajia kumpanga kwenye kikosi siku hiyo, akasema hajisikii vizuri, kwa hiyo nikampanga kipa Juma Kaseja,” anasimulia.

Hali haikuwa hali, hapo ndipo alipoanza kuumwa. Mchezaji huyo inaonekana alichelewa kwenda hospitali kuchukua vipimo pengine kutokana na majukumu ya kuzunguka kwenye kazi. Daktari wa zamu aliyekuwepo katika hospitali hiyo ya Bugando, Domician Ndiyamukama anaelezea kifo cha Burhan. Ni huzuni kubwa sana kwa wapenzi na wadau wote wa soka hapa nchini kutokana na kifo cha golikipa wa timu ya Kagera Sugar, David Burhan aliyefariki katika hospitali ya rufaa ya Bugando.

Kwa mujibu wa daktari aliyempokea David hospitalini hapo, kifo cha Burhan kilisababishwa na matatizo ya ini pamoja na mapafu ya marehemu yalikuwa yamejaa maji, ambapo kwa kitaalamu ni ‘Pleural efussion’. Dokta huyo alisema David alipokewa hospitalini hapo saa tano asubuhi siku ya Jumapili na kisha alifariki alfajiri ya saa nane. Hata hivyo, gazeti hili lilifanya juhudi za kuwatafuta ndugu zake, ambapo lilifanikiwa kumpata mjomba yake, Moses Melele aliyesema David alizaliwa mwaka 1985 jijini Dar es Salaam.

David ni mtoto wa mzee Abdallah Burhan na Edna Micheal. Mzee Burhan aliwahi kuchezea timu za Pan African na Yanga, huku mama yake, Edna aliwahi kucheza netiboli katika timu za Jeshi Stars,Bora na General Tyre. David alikuwa wa kwanza kuzaliwa kati ya watoto wawili, ambapo wa pili ni dada yake anayejulikana kwa jina la Atupele Burhan. Miezi sita badaa ya kuzaliwa kwake David alipelekwa kwa bibi yake mkoani Iringa ambako ndiko pia alikopatia elimu yake ya msingi katika shule ya Wilolesi kabla ya kujiunga na Chuo cha Ufundi cha Veta mkoani Iringa.

David alianza kucheza mpira akiwa katika klabu ya Lipuli kisha akaenda Twiga kabla ya kuchezea timu za Polisi Iringa, Baada ya kutoka Tanzania Prisons alihamia Mbeya City mwaka 2012 halafu akatimkia timu ya Majimaji ya Songea kabla ya kujiunga na Kagera Sugar, ambapo aliitumikia hadi mauti yalipomkuta. David ameacha mjane Rachel Ngwale na watoto wawili, Bryan Burhan na Raymond Buruhan.Familia ya marehemu ipo Iringa.

Wadau wa soka watoa maoni Meneja wa klabu ya Kagera Sugar, Mohamed Hussein alisema timu yao imeumizwa sana na taarifa hizo kutokana na umuhimu wa mchezaji huyo katika timu yao. ‘’Hali yake haikuwa nzuri tuliamua kumsafirisha kwa ndege kutoka mkoani Kagera mpaka huko Mwanza. Burhan alianza kuugua siku tatu baada ya mchezo wetu wa FA dhidi ya Singida United na wakati wa mechi hiyo alikuwepo benchi. Kifo ni wajibu wa kila mtu ila tumeumia sana,’’ Hussein alisema.

Hussein alisema timu yao imeumizwa sana na msiba huo, lakini hakuna namna ni kazi na mipango ya Mungu. Kwa upande wake moja wa makocha waliowahi kumfundisha Burhan ni kocha wa zamani wa timu ya Mbeya City,Kimondo FC na Simba SC, Maka Mwaluis alisema taarifa hizo zimeumumiza sana kwani hakutarajia kabisa.

‘’Nimeumia sana nakumbuka David mwaka 2012 nikiwa kocha wa Mbeya City yeye alikuwa akichezea Tanzania Prisons sisi tulipokuwa daraja la kwanza, David na wenzake Sibo Aziz ambaye anachezea Ndanda kwa sasa walikuwa wanatufuata na kutupa moyo kazeni mtapanda Ligi Kuu. Mimi niliwaambia uongozi wetu tukipanda Ligi Kuu lazima tumsajili David ana moyo wa kuchezea timu yetu kweli timu ilipopanda tulimchukua yeye(David) pamoja na Paul Nonga akitokea Jkt Oljoro,’’ Maka anasema.

Mwili wa David Burhan uliagwa Jumanne katika hospitali ya rufaa ya Bugando mkoani hapa muda wa saa tatu asubuhi na baadhi ya wadau wa soka ambao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Soka mkoani Mwanza( MZFA), Leonard Malongo, Katibu wa Chama cha Soka la Wanawake(TWFA), Hawa Bajanguo, meneja uwanja wa CCM Kirumba Steven Shija na Katibu Mkuu wa Toto African Ernest Mpiwa.

Marehemu David alizikwa Jumatano mkoani Iringa Kocha mwingine aliwahi kumfundisha David ni Hassan Banyai aliyemfundisha katika timu ya Majimaji aliyesema David ni mmoja ya watu muhimu sana ambao walisaidia timu timu hiyo kubaki Ligi Kuu msimu uliopita. Banyai alisema alikuwa bado na mikakati ya kufanya kazi na David ila tatizo ni mauti kumkuta. Akizungumza na gazeti hili,wakati wa kuaga mwili wa marehemu David katika hospitali ya rufaa ya Bugando Jumanne daktari mkuu wa Kagera Sugar, Abeid Shindika alisema msiba huo ni pigo kubwa kwa timu yao, kwani walimtegemea David sana katika timu hiyo.

“David alipata tatizo tukielekea mkoani Singida kwa ajili ya mechi ghafla alianza kuharisha kisha akatapika ikabidi tumpe huduma ya kwanza ndipo alipata nafuu. Aliendelea kueleza kuwa ilipofika saa nne usiku alikuwa anaendelea vizuri tu na saa saba usiku alinitumia ujumbe niende kwani alikuwa amezidiwa, nikaenda kumuangalia na alikuwa amezidiwa,’’ Shindika alisema. Shindika alisema kabla ya mechi yao na Singida United ya mkoani Singida kipa huyo alimeza dawa za Malaria aina ya Malafin na akawa akiendelea vizuri.

Dr Shindika alisema muda wote alioishi na marehemu hakuwai kumwambia kuwa ana tatizo la kiafya zaidi ya kufanya akifanya mazoezi kwa bidii muda wote. Katibu Mkuu wa MZFA alitoa pole kwa wadau wa soka wote hapa nchini pamoja na timu ya Kagera Sugar kwa kumpoteza kipa huyo. Malongo alisema msiba huu ni wa taifa zima hivyo wanamichezo na jamii waendelee kuiombea familia ya marehemu David Burhan. Mungu ailaze mahali pema peponi Amina.