Bahati nasibu bila kudhibitiwa ni hasara kwa Taifa
- In Makala
- Post 13 Juni 2012
- By Lucy Lyatuu
- Imesomwa mara: 380
UDHIBITI wa jambo lolote ni suala la muhimu ambalo ngazi mbalimbali zinapaswa kusimamia na kutekeleza kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Ukiukwaji wa taratibu zinazotakiwa katika sekta mbalimbali kunaweza kusababisha uwepo wa malalamiko katika jamii na hata kushusha viwango vya utendaji kazi pamoja na kushuka kwa mapato yanayoweza kupatikana kwa njia moja hadi nyingine.
Michezo ya kubahatisha nchini pamoja na kuongeza ajira kwa baadhi ya vijana lakini pia ina manufaa katika kuchangia mapato ya nchi na vilevile kwa mtu mmoja mmoja.
Akizungumza hivi karibuni katika mkutano Mkuu wa Tisa wa Wadhibiti wa Michezo ya Kubahatisha Afrika (GRAF), Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Joyce Mapunjo anasema Bodi ya Kudhibiti Michezo ya Bahati Nasibu nchini inatakiwa kusimamia sheria, viwango pamoja na mfumo mzima ili kudhibiti uingizwaji holela wa mashine zinazotumiwa na kusababisha kuiba fedha za wananchi.
Mkutano huo ulihusisha washiriki kutoka nchi 10 za Afrika ambazo ni Botswana, Swaziland, Kenya, Malawi, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Zambia na Tanzania. Mashine ama vifaa vinavyotumiwa katika michezo hiyo vinapaswa kudhibitiwa ili visiingie kiholela bila kukaguliwa na kujulikana ubora wake kwani inaweza kuwa kichocheo cha kuiba fedha za wateja pamoja na kuharibu maana halisi ya michezo hiyo.
Anasema kutokudhibiti vyema sheria pamoja na viwango vya michezo ya kubahatisha ambayo ina nafasi ya kuongeza mapato kwa Serikali, kunaweza kuiletea sifa mbaya sekta husika.
“Ni vizuri kwamba mmekutana katika mkutano huu wa wadau mbalimbali ili kupata taarifa za maendeleo ya mfumo huu na mfahamu changamoto zinazowakabili ili kuweka udhibiti mzuri ambao utaiendeleza sekta hii,” anasema na kuongeza kuwa dunia nzima inanufaika kutokana na michezo ya aina hiyo ambayo huongeza ajira, mapato na burudani pia.
Bodi inatakiwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya Serikali kama Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Uhamiaji na shirika la Viwango ili kudhibiti vifaa na mfumo mzima katika kuongeza mafanikio. Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa GRAF kutoka Tanzania, William Mdundo anasema mkutano huo unalenga wadhibiti kuweka kanuni ambazo zitahakikisha watu hawaibiwi na kwamba hata wasio waaminifu kutoingia katika mifumo hiyo.
Kwa kampuni zinazohusika na michezo hiyo kama kampuni za simu lazima zihakikishe zinapata cheti cha kuchezesha michezo hiyo ili ziweze kusimamiwa ipasavyo lengo likiwa ni kukwepa wasio waaminifu kuingia.
Ipo haja ya kuchunguza kwa kina maeneo ambayo ni nyeti na yanayohusika na kuchezesha michezo hiyo ili kwamba yaweze kudhibitiwa kujua mapato na kiwango ambacho wananchi wananufaika nacho kwani michezo hiyo ni biashara na burudani pia.
Naye Mtendaji Mkuu wa Bodi hiyo nchini, Tarimba Abbas anawataka wananchi ambao wana malalamiko juu ya kutotendewa haki katika mchezo wowote kutoa taarifa katika Bodi hiyo ili kwamba uchunguzi ufanyike na hatua zichukuliwe.
Udanganyifu katika michezo ya aina hiyo hairuhusiwi, hivyo wananchi hawatakiwi kubaki wakilalamika au kunung’unika pale ambapo hawakutendewa haki, badala yake wanatakiwa kutoa taarifa katika Bodi ili uchunguzi ufanyike na hatua zichukuliwe kwani kufanya hivyo ni ukiukwaji wa kanuni na kutotenda haki kwa walengwa.
Hata hivyo, Watanzania wanatakiwa kuifahamu vyema michezo hiyo, ambayo ni biashara na wajue kuwa inaendeshwa kwa mujibu wa taratibu kanuni na sheria na kwamba inawapasa waendeshaji kutumia kanuni hizo ili kuepuka manung’uniko na lawama kutoka kwa wananchi.
Aidha, Bodi imekuwa ikipokea malalamiko kutoka maeneo mbalimbali kwa mfano casino na katika kampuni za simu kuwa haziwaridhishi wateja wao ambapo uchunguzi unaendelea na hatua zitachukuliwa dhidi ya wanaohusika.
Michezo ya bahati nasibu imekuwa na manufaa kwa taifa kwani licha ya kuongeza ajira lakini pia kwa mwaka jana Bodi hiyo imeweza kuilipa Serikali kodi ya Sh bilioni 16 ambapo ukuaji unaongezeka kwa asilimia 20 licha ya kwamba wakati wa mdororo wa uchumi, sekta hiyo iliathirika kwani ukuaji wake ulishuka kwa asilimia 10.
Tarimba anasema katika Afrika Mashariki, Tanzania inaongoza kwa kuingiza mapato mengi ikifuatiwa na Kenya huku nchi za Burundi, Rwanda na Uganda zikifuatia. Anaitaja biashara hiyo ambayo kwa upande wa casino ukuaji wake unaongoza ikifuatiwa na ujumbe mfupi wa kwenye simu, utabiri na hata mashine za biashara ya fedha.
Mwenyekiti wa GRAF, Profesa Linda De Vries kutoka Afrika Kusini anasema ipo haja ya wadhibiti kuweka mikakati ambayo itasaidia kudhibiti mashine zisizo na viwango ambazo zinawaibia watu fedha zao. Kadhalika Bodi hiyo ishirikiane na Mamlaka ya Mapato, Jeshi la Polisi na Uhamiaji ili kuhakikisha wananchi hawaibiwi na hawapotezi fedha zao katika michezo hiyo ila pande zote zinufaike na kutokuwepo kwa malalamiko.
Lazima kuwe na malengo sawa ya udhibiti kwa sekta hiyo, kuimarisha mazingira ya utendaji kazi baina ya wadau wa GRAF ili kuweka miradi ambayo itasimamia mazingira hatarishi katika michezo hiyo.
Vilevile ipo haja ya kuimarisha misingi ya sheria katika mitandao ya michezo ambayo itakuwa ikiwafikia wananchi ili kwamba kila mmoja aweze kusoma pamoja na kuwasaidia waendeshaji kusimamia kanuni na sheria za shughuli za michezo ya bahati nasibu.
Kadhalika kuchukua hatua za kisayansi katika kukuza tafiti kabla ya kupitia sheria na taratibu za sekta hiyo pamoja na kuchukua hatua za kistaarabu katika masoko mbalimbali ya michezo hiyo kama sekta inahitaji kukua zaidi.
Aidha nchi za Afrika zina haja ya kukuza database(kanzidata) kwa ajili ya usajili wa wananchi wanaopata ajira ambapo itasaidia kusimamia viwango na kuratibiwa na nchi wanachama waliomo katika mtandao huo pamoja na suala la kujenga uwezo kupewa kipaumbele ili nchi hizo ziweze kuhusika.



