OMARI KIPUTIPUTI: Najivunia kuzalisha wataalamu wa biashara
- In Makala
- Post 13 Juni 2012
- By Mwandishi Wetu
- Imesomwa mara: 652
BIASHARA ni eneo ambalo limekuwa kimbilio kwa watu wengi kwa maana ya kujiajiri na kuajiriwa.
Omari Kiputiputi ni Mkuu wa Chuo cha Biashara cha Aseki Dodoma, ambaye katika makala haya anaeleza juhudi na shauku yake ya kuona ongezeko la wataalamu waliobobea katika biashara. Kiputiputi anasema ongezeko la taasisi zinazotoa elimu ya biashara ni fursa ambayo Watanzania hawana budi kuitumia. Analinganisha miaka iliyopita na sasa .
Anakumbuka miaka ya 1970; kipindi ambacho nchi haikuwa na wigo mpana wa elimu ya biashara. Hata idadi ya wanafunzi waliokuwa wakijiunga katika vyuo husika haikuwa kubwa ikilinganishwa na sasa ambapo mahitaji yamepanuka.
Anaelezea historia yake kwamba baada ya kuhitimu Shahada ya ualimu wa masomo ya sayansi mwaka 1979 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliajiriwa na Chuo cha Biashara (CBE) Dar es Salaam na kufanya kazi chuoni hapo kwa miaka 31, kabla ya kustaafu mwaka juzi kwa mujibu wa sheria.
Miaka 10 ya mwisho licha ya kuendelea na kazi ya ufundishaji, anasema alipewa dhamana ya kuwa Makamu Mkuu wa Chuo cha CBE Dodoma. Akielezea hali halisi juu ya mahitaji ya elimu ya biashara, anasema “Nilikuta CBE Dodoma ikiwa na wanafunzi 183 tu, lakini hadi ninaondoka (mwaka 2010) niliacha wanafunzi zaidi ya elfu nne.
Uwezo wa kampasi ile ni wanafunzi 200 tu, lakini tuliweza kufanya yote haya kutokana na stadi za kijasiriamali,” anasema Kiputiputi.
“Nilipokea kampasi ile ikiwa inaendesha programu moja tu ya Stashada katika fani tatu tu yaani Uhasibu, Uendeshaji Biashara na Uboharia, lakini nimeiacha kampasi ikiwa inaendesha programu tatu, Cheti, Stashahada na Shahada katika fani tano za uhasibu, uendeshaji biashara, masoko, uboharia na Tehama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano),” anasema.
Kutokana na mazingira hayo, anasema kadri siku zinavyokwenda, ndivyo mahitaji ya elimu ya biashara yanavyoongezeka nchini. Anasema uanzishwaji wa Chuo cha Aseki , umezingatia mahitaji hayo. Anasema licha ya kwamba alishastaafu, anaona ni fahari kubwa kuendelea kuelimisha umma hususan vijana wanaohitimu kidato cha nne na sita .
“Aseki kimedhamiria kutoa wahitimu bora wanaoweza kujiajiri wenyewe au hata kuajiriwa kila pembe ya dunia,” anasema . Anasisitiza kuwa upo uhitaji mkubwa wa wataalamu wa masuala ya uendeshaji wa biashara ambalo ni eneo muhimu linalopaswa kutiliwa mkazo nchini. Eneo lingine ni la manunuzi na ugavi.
“Tunatoa Stashahada katika uendeshaji wa biashara, uhasibu na manunuzi na ugavi...haya ni maeneo ambayo sisi kama wadau tunaona yanahitaji kutiliwa mkazo kwa ustawi wa uchumi wa nchi yetu,” anasema.
Kiputiputi anatoa mwito kwa wawekezaji, kujitokeza zaidi katika kuwekeza kwenye elimu ya biashara ili kusaidia malengo ya Serikali ya Milenia, yanayotaka taifa liwe imara katika nyanja mbalimbali.
Kwa mujibu wake, katika kutimiza azma ya kupanua wigo wa wahitimu mbalimbali kupata elimu ya biashara, mwanafunzi yeyote aliyemaliza kozi ya cheti kutoka kwenye chuo chochote kilichosajiliwa na Baraza la Taifa la Ufundi (NACTE) ; au aliyemaliza kidato cha sita na kupata angalau alama moja ya ufaulu, anaweza kujiunga na kozi ya Stashahada chuoni kwake.
Anasisitiza kwamba wanafunzi lazima waandaliwe katika misingi bora ya uendeshaji bora wa biashara na hatimaye taifa lipate wataalamu waliobobea watakaokuwa chachu ya maendeleo. Vilevile anasema suala la gharama za masomo ni kikwazo kwa Watanzania walio wengi jambo ambalo anasema wamelizingatia katika kuwezesha wanafunzi wengi wanapata elimu ya biashara.
“Tunajitahidi chuo hiki kiwe cha kipekee nchini kwa kutoa wahitimu bora katika menejimenti, ujasiriamali na ujuzi kupitia mafunzo, utafiti, utumishi wa umma na huduma za kijamii katika kanda hii na hata nje ya mipaka ifikapo mwaka 2020”, anasisitiza.
Anasema, “Tumepania kuwa kituo kilichotukuka, yaani kituo bora katika kutoa elimu, mafunzo na stadi katika nyanja za biashara, uendeshaji na ujasiriamali kupitia mafunzo, utafiti, huduma kwa umma na shughuli za nje ya chuo katika kanda hadi kufikia mwaka 2020,” alisema.
Miongoni mwa mambo anayosisitiza Kiputiputi, ni juu ya taasisi zinazotoa elimu hiyo ya biashara kuwa na walimu wenye uwezo wa kumwandaa mwanafunzi siyo tu kufaulu mitihani kwa lengo la kuajiriwa, bali pia kumwezesha kujiajiri. Anasema chuo chake kimezingatia hilo.
Anasema changamto hizo zikitatuliwa, zinatoa mwanya kwa wahitimu kuwa na viwango vinavyowawezesha kufanya vyema wanapojiajiri, kuajiriwa au wanapoendelea na masomo ya juu. “Hata wanapojiajiri, lazima wawe watu wa kupigiwa mfano na jamii ione umuhimu wa kusomea fani hiyo ya biashara,” anasema.
Kiputiputi anasisitiza umuhimu wa vyuo vinavyotoa elimu hiyo kujisajili katika mamlaka zinazohusika ili kuwawezesha wahitimu kutambulika rasmi katika soko la ndani na nje ya nchi. Anatoa mwito kwa Watanzania kuchangamkia fursa za kuanzishwa kwa taasisi mbalimbali zinazotoa elimu ya biashara, kikiwemo Aseki ambacho licha ya kuanzishwa mwaka jana, anasema kinaonesha mustakabali mzuri.
Anasema chuo hicho kichanga kina huduma muhimu yakiwemo madarasa, maktaba yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 60 na maabara ndogo ya kompyuta, zilizounganishwa kwenye mtandao wa intaneti. Anawaasa vijana wanaohitimu kidato cha nne na sita, kutokata tamaa juu ya uwezekano wa kupata elimu ya biashara.
Anaamini katika miaka michache ijayo, nchi itakuwa na wataalamu wengi wa biashara kutokana na vyuo mbalimbali binafsi, kikiwemo Aseki kupanua wigo wa wanafunzi wanaojiunga na kozi husika.
“Wanafunzi wanapokuja hapa, sisi licha ya kumpa stadi muhimu za maisha tutampa pia sifa za kuweza kujiunga na chuo kikuu chochote nchini ndani ya miaka mitatu, tutampa stadi za kuweza kujiajiri yeye mwenyewe au kuajiriwa baada miaka hiyo mitatu ya kwanza endapo atashindwa au ataamua kutoendelea na masomo zaidi,” anasema Kiputiputi.
Kiputiputi anaamini kwamba elimu bora na ujuzi wa hali ya juu ndiyo siri ya utatuzi wa tatizo la ajira miongoni mwa Watanzania. Anasema ujuzi ndiyo utakaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa katika maeneo tofauti. Hata hivyo anasisitiza kwamba kufanya kazi kwake kwa bidii, utiifu, ubunifu na uadilifu mkubwa ni siri nyingi ya kufanikisha malengo ya taasisi katika kuwezesha wanafunzi kupata elimu iliyotukuka.
“Nilipostaafu mwajiri wangu alinipa zawadi nyingi, ikiwemo cheti cha utumishi uliotukuka hivyo nawahimiza wazazi na walezi walete watoto wao kwangu ili waendelee kufaidi utumishi wangu uliotukuka,” anasema na kusisitiza kuwa anajivunia kuendelea kuzalisha wataalamu wa biashara.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Aseki, Dk. Richard Mushi, chuo hicho kimeanzishwa kwa ubia. Mushi anawahimiza Watanzania kuwa na utamaduni wa kuunda ubia na kufanya miradi mikubwa kama huo wa chuo badala ya biashara kuwa ya mtu mmoja mmoja.
Anasema walioanzisha Chuo cha Aseki kwa ubia, wamefanikiwa tofauti na dhana iliyojengeka dhidi ya biashara ya ubia. Anasema chuo kinazidi kusonga mbele kutokana na uongozi uliotukuka wa Kiputiputi. “Waanzilishi wa chuo hiki wanastahili pongezi sana.
Baraza linaona fahari kuongoza chuo hiki kwani licha ya kuanzishwa na watu binafsi chuo kimetimiza masharti yote ya msingi ya kuandikishwa yaliyowekwa na Baraza la Vyuo vya Elimu ya Ufundi (NACTE ) na ndiyo maana kimepata usajili kamili”, anasema Dk Mushi.
Anasema Baraza la Chuo limedhamiria kuona wakufunzi wa chuo hicho wanapata elimu ya ngazi ya juu zaidi ili waweze kumudu majukumu yao ipasavyo na wawe na viwango vinavyokubalika popote.
Mwenyekiti wa Baraza la Mitihani, Balozi Job Lusinde, pia licha ya kusifu uongozi wa chuo hicho kwa ujumla, anasema Baraza lake limepania kuhakikisha linasimamia viwango vya juu vya taaluma ili wahitimu watakaotoka Aseki wawe watu wa kupigiwa mfano.



