25Mei2013

 

Barabara ya Makoka inahitaji maarifa zaidi

KITONGOJI cha Makoka kipo Kata ya Makuburi katika Manispaa ya Kinondoni kinachoendelea kukua kwa kasi kama ilivyo kwa maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam kutokana na wananchi wengi kukimbilia kujenga katika eneo hilo.

 

Kama ambavyo shughuli za ujenzi zinavyoendelea katika maeneo mbalimbali yaliyopo mjini na pembezoni mwa mji, kitongoji cha Makoka pia kimeendelea kubadilika siku hadi siku kutokana na idadi ya majengo kuongezeka kwa kasi.

Kitongoji hiki kilichotawaliwa na vijilima vidogo vidogo pamoja na miinuko mikali ya hapa na pale, pamoja na sifa ya kuwa na miti mingi ikiwamo ya asili katika baadhi ya inayokifanya kivutie machoni kinakabiliwa na tatizo la miundombinu ya barabara.

Njia rahisi ya kufika katika eneo hili ambayo ndiyo hasa hutumiwa na wananchi wengi, inaanzia Riverside ambapo hapo utakutana na pikipiki nyingi na daladala kuukuu, zinazoashiria ubovu wa barabara hadi kulifikia eneo hilo suala ambalo hata wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakililalamikia kwa kipindi kirefu.

Kama una roho nyepesi unapoelekea kwa mara ya kwanza katika eneo hilo ukiwa ndani ya daladala, wenyeji wa huko hawatokucheka kama wakikusikia ukilalamika kwa kurushwa rushwa na daladala huku ukimtaka dereva kupunguza mwendo hali ya kuwa mwendo wenyewe hautofautiani sana na mwendaji wa miguu.

Wakazi wa eneo hilo wanasema ‘suala la kurushwarushwa wameshazoea na zaidi kilio chao kikubwa ni kutofika kwa usafiri wa aina yoyote katika kitongoji hicho pindi mvua zinapokuwa zimenyesha zaidi ya usafiri wa pikipiki waliodai hata hivyo ni wachache ndiyo wanaoumudu kwa gharama.

“Maisha ya huku hayatofautiani sana na ya kijijini kama kule wanapata shida ya usafiri na sisi ni vivyo hivyo, tatizo kub- wa ni ubovu wa hii barabara ambayo kwa kipindi kirefu imekuwa ikitolewa ahadi kuwa itajengwa, miaka inaenda na hakuna kinachoendelea,” anasema mkazi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Cathlida Mdendemi.

Anasema kama barabara hiyo ingekuwa imejengwa japo kwa kiwango cha changarawe, ingewarahisishia tatizo la usafiri wananchi sambamba na kupunguza muda kwani kwa sasa wanalazimika kutumia zaidi ya saa moja katika eneo ambalo kama barabara ingekuwa nzuri wangetumia dakika zisizopungua kumi na tano.

Katika hilo anasema kumekuwa na daladala chache zinazofanya safari kuelekea eneo hilo kutokana na wamiliki wengi wa vyombo hivyo kuogopa magari hayo kuchakaa upesi kutokana na ubovu wa barabara, tatizo analosema lisingekuwepo kama barabara hiyo ingekuwa nzuri.

Mkazi huyo anasema tatizo la usafiri zaidi linakuwa kero nyakati za asubuhi na jioni watu wanapokuwa wanakwenda au kurudi kutoka kazini halikadhalika wanafunzi wanakwenda au kurejea kutoka mashuleni. Pamoja na tatizo hilo la usafiri kwa wakazi wa eneo hilo, anachoshukuru Cathlida ni nauli ya Sh 300 wanayotozwa katika daladala, na kudai kwamba pengine siyo sahihi sana kutokana na muda ambao magari hayo yanatumia na ubovu wa barabara hiyo.

Anasema kama mtu hapendi kubanwa sana ndani ya daladala hizo jambo alilodai kuwa ni kawaida kwao, atalazimika kukodi pikipiki ambayo atatozwa nauli kuanzia Sh 1,500 hadi 2,000 au kuomba lifti kwa wenye magari yao binafsi aliodai kuwa wapo baadhi wanaoelewa tatizo na hivyo wanatoa msaada.

Hivi karibuni wakazi wa eneo hilo kupitia vyombo mbalimbali vya habari, walilalamikia suala la ubovu wa barabara hiyo na kumtaka diwani wao kutimiza wajibu wake wa ahadi aliyitoa kuwa anafanya kila analoweza kufikisha kwa wahusika kilio cha wakazi hao kuhusu tatizo la barabara hiyo.

Walisema tangu ahadi hizo zimetolewa ni kipindi kirefu bila uwepo wa jitihada zozote za awali za kulitatua tatizo hilo, suala walilodai kuwa ni vyema kiongozi huyo akalivalia njuga ili kuwakomboa dhidi ya kero hiyo waliyodai kuwa ndiyo kikwazo kikubwa kwao.

Walisema kitendo cha barabara hiyo kutopitisha magari nyakati za mvua kutokana na utelezi katika milima, ni kero ukizingatia kuwa wakazi wanaoishi eneo hilo ni binadamu ambao wanaweza wakapatwa na tatizo lolote likiwamo ugonjwa na hivyo kulazimika kuwahishwa hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Wananchi hao wanasema kuwa ‘kimsingi wana imani kubwa na kiongozi wao’ lakini jambo jema na la muhimu kwa sasa analopaswa kulifanya ni kutekeleza ahadi ya kushughulikia ujenzi wa barabara hiyo wakishirikiana na manispaa ya Kinondoni, ili wao waweze kuondokana na tatizo linalonikabili.’

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Makuburi William Mwangwa alisema kwa sasa wapo katika mpango wa kulipa fidia kwa kaya tisa zinazopisha maeneo yao yanayotwaliwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo zinazopaswa kutolewa na manispaa ya Kinondoni.

Anasema fedha zinazopaswa kulipwa kwa wakazi hao, ni zaidi ya milioni 65, ikiwa ni awamu ya pili baada ya kukamilika kwa malipo ya zaidi ya Sh milioni 125 miezi michache iliyopita huku akiiomba Manispaa ya Kinondoni kuharakisha malipo hayo yaliyosalia.

“Itakuwa jambo la busara kwa manispaa kama itaona umuhimu wa kulipa kiasi hicho kabla ya mwisho wa bajeti ya Mwaka huu, ili kuwapa fursa wahusika wa zoezi hilo kujiandaa mapema kwa ajili ya kuondoka ili kuacha utaratibu mwingine wa kuunganisha barabara hii na ile ya Mandela kukamilika,” anasema Mwangwa.

Anasema Barabara hiyo inayotarajiwa kujengwa kwa kiwango cha changarawe inatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa Makoka kutokana na hali mbaya ya sasa ya barabara hiyo ambao hata hivyo wakati wa mvua imekuwa ikisababisha magari kutopitika kwa urahisi.

“Hiki ni kilio kikubwa cha wakazi hawa ambao wamekubali kwa dhati kuondoka katika maeneo yao na kwenda maeneo mengine, litakuwa jambo jema kama Mkurugenzi na Meya watawaunga mkono kwa kufanikisha malipo yao haraka kabla ya bajeti kuisha,” anamalizia kusema Mwangwa.