24Mei2013

 

Taifa Stars kazeni buti Msumbiji

TIMU ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), kesho inashuka kwenye uwanja wa Zampeto nje kidogo ya Jiji la Maputo kuanzia saa 9 mchana kwa saa za huko kucheza na timu ya taifa ya Msumbiji, The Mambas.

Mchezo huo ni wa marudiano wa mbio za kusaka nafasi ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Afrika Kusini mwakani. Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Februari mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya kufungana 1-1 na kuifanya Stars kuwa, na kazi nzito ya kuifungisha virago The Mambas.

Matumaini:

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Paulsen anasema kuwa, timu yake inahitaji ushindi katika mchezo huo, ili iweze kusonga mbele katika kinyang’anyiro hicho cha kusaka nafasi ya kusonga mbele.

Hata hivyo, katika kikosi chake, Kim atawakosa baadhi ya wachezaji wake kama ; kipa Mwadini Ali, na mabeki Nassoro Masoud ‘Cholo’ na Waziri Salum, ambao ni majeruhi na hawakwenda na kikosi hicho kilichokwenda Msumbiji.

Kim anasema kuwa, baada ya timu hiyo kucheza mechi tatu, mbili za kimashindano na moja ya kimataifa ya kirafiki, timu yake imeonyesha maendeleo mazuri, ingawa bado anafanyia kazi kwa nguvu safu ya ushambuliaji.

Katika mchezo wa hivi karibuni wa kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 Brazil uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Taifa Stars iliibuka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Gambia 2-1.

Kim inabidi kuiongezea nguvu zaidi safu yake ya ushambuliaji kufuatia mabao yote kufungwa na mabeki walipocheza dhidi ya Gambia.

Kusonga mbele:

Stars endapo itasonga mbele baada ya kuitoa Msumbiji kabla ya kupiga hatua nyingine, itabidi kwanza kucheza na moja ya timu zilizoshiriki fainali za AFCON za Januari mwaka huu katika nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon.

Timu hizo mbili zilikutana jijini Dar es Salaam Februari 29 na kutoka sare ya 1-1, katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam . Hata hivyo, wakati Stars ikiikaribisha Msumbiji katika mchezo huo wa kwanza jijini Dar es Salaam, timu hiyo ilikuwa ikiongozwa na Mdenmark mwenzake, Jan Paulsen, aliyemaliza muda wake wa kuifundisha timu hiyo.

Kim wakati huo alikuwa kocha msaidizi wa Jan, kwa hiyo sio mgeni na wachezaji wa Stars na hata hiyo Msumbiji, ambao wanatarajia kucheza nayo kesho.

Mechi zingine:

Tayari Kim tangu achukue timu hiyo, Stars imeshacheza na Ivory Coast katika mchezo wa kusaka nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazil mwaka 2014, na Stars ilifungwa 2-0 ugenini, kabla ya kucheza na Gambia jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita.

Taifa Stars iliibuka na ushindi wa bao 2-1 dhidi ya Gambia na hivyo kuondoka na pointi tatu muhimu na kuifanya timu hiyo kushika nafasi ya pili katika msimamo wa kundi lake la C nyuma ya Ivory Coast inayoongoza ikiwa na pointi nne.

Umuhimu Wake:

Kiujumla mechi zote zina umuhimu wake, hasa ukizingatia kuwa, Tanzania kwa muda mrefu sana haijawahi kushiriki katika fainali za mashindano makubwa, hivyo wakati umefika sasa timu hiyo inatakiwa kufuzu kwa fainali hizo.

Pamoja na kocha wake aliyemaliza muda wake kusema kuwa, sare na Msumbiji katika mchezo wa kwanza ilimkatisha tamaa na inaiweka timu hiyo katika hali ngumu. Hatahivyo, pamoja na wasiwasi wa Jan, Kim mwenyewe anasema kuwa, atahakikisha timu yake inaitupa nje The Mambas.

Matumaini kidogo:

Baada ya Stars kufanya vibaya kwa miaka mingi na kushindwa kushiriki fainali zozote za mabara, wapenzi wa soka walishakata tamaa na sasa mioyo yao ni mizito kila wanapoifikiria Taifa Stars.

Baada ya kuonesha kandanda safi dhidi ya Ivory Coast licha ya kufungwa 2-0 ugenini na baadae kuifunga Gambia, Watanzania wameanza kurejesha matumaini kwa timu yao hiyo, hivyo waendeleze ushindi ili kutowakatisha tamaa wapenzi.

Wakati Stars ikifundishwa na Mbrazili Marcio Maximo, kabla ya kumaliza muda wake, timu hiyo ukiondoa mashindano ya kimataifa kwa wachezaji wanaocheza soka nyumbani tu, timu hiyo angalau ilikuwa na mvuto wa mashabiki.

Kukaza buti:

Taifa Stars sasa ina kazi moja tu kugangamala na kufanya kweli, ili kuiwezesha Tanzania kufanya vizuri katika mashindano hayo makubwa, baada ya kutofanya vizuri kwa miaka mingi. Wachezaji wa timu hiyo wanatakiwa kucheza kwa kujituma huku wakitumia mafunzo waliyopewa na kocha wao Kim ili kuifunga Msumbiji katika mchezo huo wa marudiano.

Hakuna mtu asiye na shauku ya kuona Taifa Stars inashiriki fainali za Mataifa ya Afrika baada ya kufikia hatua hiyo mwaka 1980 tangu Uhuru wakati fainali hizo zilipofanyikia Nigeria , na baada ya hapo haijawahi kufikia.