26Mei2013

 

Michuano ya Botswana Open ilikuwa mateso

MICHEZO kawaida ni burudani, furaha na ushindani, lakini inapokuwa kinyume na hapo ni mateso. Hivyo, ndivyo ninavyoweza kuelezea michuano ya gofu ya Wanawake ya Botswana Open.

Michuano hiyo ilifanyika baada ya kuisha kwa michuano ya Kombe la Challenge Afrika Gaborone, Botswana mwishoni mwa wiki iliyopita. Michuano ya Afrika ilifanyika kwenye viwanja vya Klabu ya Phakalane Resorts, kabla ya ile ya Open kutimua vumbi viwanja vya Klabu ya Gaborone, Botswana.

Kulikuwa na mazingira tofauti kati ya viwanja hivyo, viwili na hali ilikuwa mbaya katika michuano ya Open. Ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania bado haina viwanja bora vya gofu ukifananisha na nchi nyingi, lakini kilichotokea uwanja wa Gaborone ni vigumu kufananisha na ilivyo nchini.

Kipindi cha Juni wenyeji Botswana wanakiri ni cha baridi kali na hivyo, wachezaji walilazimika kuvaa zaidi ya nguo moja kujikinga, hali ambayo kwa wale ambao hawatoki kwenye nchi za baridi ilikuwa ngumu kwao. Lakini michuano ya Botswana Open ilikuwa balaa, kwani pamoja na nyasi za uwanja kukauka, baridi na hali mbaya ya uwanja vilifanya mashindano hayo kugeuka mateso.

Wachezaji sita wa Tanzania wakiwepo wa timu ya taifa Madina Iddi, Hawa wanyeche na Ayne Magombe ni miongoni mwa zaidi ya wachezaji 100 walioshiriki kutoka nchi za Namibia, Kenya, Senegal, Botswana, Uganda, Gabon, Misri, Nigeria, Ghana, Swaziland, Sierra-Leone, Reunion, Malawi, Lesotho, Rwanda, Togo, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe na Mauritius.

Katika michuano hiyo, viwango vya wachezaji wengi hata wale mabingwa kutoka Afrika Kusini ambao wanaogopewa matokeo yao hayakuwafurahisha. Mchezaji nyota wa Afrika Kusini, Kim William ambaye alikuwa tishio kwenye Kombe la Challenge alikaribia kulia siku ya kwanza ya michuano aliporejea na mikwaju 79 ambayo kilikuwa ni kiwango kibovu kulingana na uwezo wake.

Gofu ni mchezo wa makosa kama ilivyo mingine na kuna wakati mchezaji anaweza kucheza chini ya kiwango, lakini sio katika mateso. Kilichotokea Uwanja wa Gaborone unaweza kuita mateso na sina hakika kama kuna mchezaji nje na wenyeji atapenda kurejea kwenye kiwanja hicho kipindi kama hiki.

Wachezaji wengi walikiri kuteseka na kuhoji wenyeWE kilichowaleta kwenye michuano. Pengine ingekuwa miezi mingine hali ingekuwa tofauti, lakini kwa hapo nina hakika wenyeji walichemka. Kibaya zaidi ni pale baadhi ya wachezaji kushindwa kurejea uwanjani siku ya pili ya raundi ya mwisho, kitu ambacho sio cha kawaida katika mashindano makubwa kama hayo.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Zambi na Uganda walikuwa ni miongoni mwa walioshindwa kutokea siku ya pili. Lakini wachezaji wa Tanzania na nchi nyingine walionesha uungwana na ujasiri kukabili hali halisi.

Kutokana na ombi maalumu la Tanzania kutaka kucheza mapema zaidi ili kuwahi kumaliza na kuanza safari ya basi hadi Johannesburg kuwahi ndege ya Precision ambao ndio wadhamini wao wa safari, wachezaji wote sita walilazimika kuwahi asubuhi kucheza pamoja na hali mbaya.

Pamoja na mateso wachezaji wote waliingia uwanjani baadhi yao wakivaa suruali mbili na fulana zaidi ya mbili na sweta mbili na koti kukabili baridi kali iliyokuwepo hasa muda wa asubuhi ambayo ilikuwa vigumu hata kushika fimbo ya gofu. Burudani ya mchezo haikuwepo zaidi ya kukamilisha raundi, lakini ujasiri wa kijeshi ndio ulichukua nafasi kwani moja ya sifa ya mchezo huo ni kuwa jasiri.

Mchezaji wa timu ya taifa, Hawa Wanyeche pamoja na hali hiyo mbaya alifanya vizuri zaidi raundi hiyo ya pili baada ya kurejea na mikwaju mitatu zaidi ya kiwango 75 baada ya siku ya kwanza kucheza 89. Mikwaju hiyo 75 ilimwezesha kuondoka na zawadi ya mchezaji bora wa raundi ya pili.

Mbali na hali hiyo mbaya na kucheza katika mazingira magumu wachezaji wote walifanya vizuri zaidi raundi ya pili katika michuano ambayo ubingwa kama ilivyokuwa kwa Kombe la Challenge ulikwenda Afrika Kusini. Hawa, ambaye alikuwa na wakati mgumu kwenye Kombe la Challenge akisumbuliwa na mafua, aliweza kuamka na kufanya vema kwenye Botswana Open na huo ni ujasiri mkubwa.

“Nimefurahi kwamba kwa mara ya kwanza tangu kutua Botswana nimecheza katika kiwango changu,” anasema Wanyeche. Hata hivyo, anakiri kwamba angetamani kiwango hicho angeonesha kwenye Kombe la Challenge akiwa na timu ya taifa kwani matokeo kama hayo yangeweza kubadili nafasi ya Tanzania ambayo ilimaliza katika nafasi ya nne kati ya nchi 21.

Lakini kwa hali ilivyokuwa michuano ya Botswana Open imeacha kumbukumbu ya aina yake kwa wachezaji. Pengine hilo litakuwa somo la kujifunza kwa waandaaji wengine wa michuano ya Afrika kuweka mashindano kipindi sahihi vinginevyo inaweza kufikia wakati wachezaji wote wakagoma kuingia uwanjani.