Yanga, Azam ni kisasi

Yanga, Azam ni kisasi Na Vicky Kimaro INAPOWADIA mechi ya Simba na Yanga, hiyo ni ya wapinzani wa jadi katika soka ya Tanzania, lakini kwa sasa ‘Mechi Kubwa’ zaidi ni ile inayozikutanisha Azam FC na Yanga SC.

Timu hizo leo zitakutana kwenye mchezo wa tatu wa Kundi A kwenye Uwanja wa Amaan, ambapo timu hizo zinachuana kwa karibu kutaka nafasi ya kuongoza Ligi Kuu Tanzania Bara, ila kisasi sasa kimehamia katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi.

Timu hizo leo zinakutana mara 27 kwenye mashindano yote, ambapo kwenye Ligi Kuu wamecheza mechi 17 Yanga wameshinda mara tano, Azam nao wameshinda mara tano, wametoka sare mara saba, timu hizo zimefungana kwa idadi ya mabao 25.

Kwa upande wa Kombe la Mapinduzi, timu hizo zimekutana mara mbili, awali zilikutana mwaka 2012, ambapo Azam FC inaonekana kuwa na rekodi nzuri pale ilipoifunga Yanga kwa mabao 3-0 Azam kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 mwaka 2016 katika michuano hiyo.

Hivyo, pamoja na Yanga kuwa na tiketi yake mkononi ya kucheza nusu fainali, mchezo huo kwao utakuwa wa kulinda heshima na kutaka kulipa kisasi cha kufungwa na Azam FC mwaka 2012, hivyo Wana lambalamba hao wasitarajie mteremko kutroka kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Yanga ndio inaongoza kundi lao wakiwa na pointi sita mbele ya Azam wenye pointi nne, huku Jamhuri ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi yake moja wakati Zimamoto haijambulia pointi baada ya kila timu kucheza mechi mbili.

Azam FC inahitaji sare tu ili iweze kufikisha pointi tano, ambazo hazitaweza kufikiwa na timu nyingine yoyote ukiondoa Yanga, ambao tayari imeshasonga mbele. Kikosi cha Azam kinatarajiwa kusheheni wachezaji wa kimataifa kama Yahaya Mohamed, Enock Agyei, Yakubu, na wengine, huku Yanga ikiwatumia zaidi Thaban Kamusoko, Donald Ngoma, Tambwe na Msuva katika kupata mabao.

Kocha George Lwandamina amekuwa akitumia mfumo wa pasi ndefu za katikati ya uwanja kutengeneza mabao huku Thabani Kamusoko na Haruna Niyonzima ndiyo wakipewa jukumu hilo. Wawili hao, wamekuwa wakipiga pasi ndefu kwa Amissi Tambwe, Donald Ngoma au Simon Msuva ambao wamekuwa wakimalizia pasi hizo.

Msuva anaongoza kwa kuwa mfungaji bora katika michuano hiyo hadi sasa ana mabao manne. Akizungumzia mchezo huo, Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema kikosi chake hakina wasi wasi na wapinzani wao na ana matumaini ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

“Kila mchezo una umuhimu wake kwetu, tunauchukulia kwa uzito wa juu tukiwa na lengo moja tu la kupata ushindi na siyo jambo jingine, ”alisema Mwambusi. “Tunawajua Azam kwamba wamekuwa wakitupa upinzani wanapokutana na sisi, lakini kwa safari hii niwaambie kwamba wasahau hilo kwani tunataka kushinda na kumaliza nafasi ya kwanza kwenye kundi.

Kwa upande wa kocha wa muda wa Azam, Idd Nassor Cheche, amejinasibu kuwa ni lazima atoke na ushindi katika mchezo huo dhidi ya Yanga. Cheche ambaye anasaidiana na Idd Abubakar baada ya uongozi kutimua benchi lote la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Zeben Hernandez, alisema wameenda Zanzibar kushindana na nsio kufanya utalii, hivyo ni lazima warudi na Kombe.