Simba kumekucha Zanzibar

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba leo wanashuka dimbani kucheza na vijana hatari wa Jang’ombe Boys katika mchezo wa kuhitimisha mechi za Kundi A utakaofanyika kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Mchezo huo ni kama fainali kwa timu zote mbili, licha ya Simba kuongoza wakiwa na pointi saba mkononi baada ya kucheza mechi tatu, lakini wakifungwa leo, Jang’ombe watafikisha pointi tisa. Simba iko kieleni katika Kundi A baada ya zifunga 2-1 Taifa Jang’ombe , 1-0 dhidi ya KVZ na kutoka suluhu na Mamlaka ya Mapato Uganda au URA.

Jang’ombe Boys wakiipumulia Simba kwa pointi sita, hivyo wakishinda au kutoka sare watafikisha pointi saba au tisa na kuifikia au kupita kabisa Simba. Taifa jang’ombe nao wana pointi sita na URA, ambao ni mabingwa watetezi wa kombe hilo, wenyewe wana shika mkia wakiwa na pointi zao nne, lakini wana uwezo wa kufikisha saba, endapo watashinda leo.

URA wenyewe leo watakuwa na kibarua wakati watakapotoana jasho na Taifa Jang’ombe katika mchezo utakaofanyika kuanzia saa 2:30 usiku kwenye Uwanja huo huo wa Amaan.

Simba wenyewe wanajua kuwa mchezo wa leo utakuwa mgumu pamoja na umuhimu wake kutokana na Jang’ombe Boys pamoja na uchanga wao, lakini wameonesha uwezo mkubwa hata kuifunga URA, ambayo Simba walitoka nayo suluhu.

Kitu kingine kinachofanya mechi zote za leo kuwa muhimu, hadi sasa hakuna timu yoyote yenye uhakika wa kucheza nusu fainali kutoka katika kundi hilo, huku kila moja ikiwa na nafasi ya kufuzu kwa hatua hiyo kutegemea na jinsi itakavyochanga karata zake.

Simba wanaweza kujikuta wakirudi Dar mapema endapo watafungwa, kwani watabaki na pointi zao saba wakati Taifa Jang’ombe na Jang’ombe Boys kila moja inaweza kufikisha pointi tisa endapo itashinda mchezo wake wa mwisho.

Aidha, Kocha Mkuu wa Simba Mcameroon Joseph Omog alisema anatarajia upinzani mkali kutoka kwa Jang’ombe Boys katika mchezo wao huo. Omog alisema kwamba Jang’ombe Boys ni timu nzuri na ilidhihirisha hilo baada ya kuwafunga mabingwa watetezi, URA 2-1, hivyo hata mbele ya Simba watakuwa tishio tu.

Kwa sababu hiyo, Omog amesema kwamba amewandaa vizuri vijana wake kwenda kucheza kwa tahadhari ili kuepuka kuingia kwenye mitego ya Jang’ombe Boys.

Nusu fainali ya kwanza ya mashindano hayo itapigwa kwenye Uwanja huo Januari 10 saa 10:00 Jioni wakati ile ya pili itafanyika kuanzia saa 2:30 Usiku wakati fainali itakuwa Januari 13 kuanzia saa 2:30 Usiku.

Katika Kundi B, Yanga tayari imeshajihakikishia nafasi ya kucheza nusu fainali na jana usiku ilikuwa na kibarua cha kucheza na Azam FC ikisubiri wa kukutana naye katika hatua hiyo. Mashindano hayo ni ya kusheherekea miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika mwaka 1964, ambayo yaliuondoa utawaka wa Waarabu.