Malima atoa neno kwa wageni

BEKI wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ amesema viwango vya wachezaji wa kigeni wanaokuja kusakata kabumbu nchini vinatia walakini.

Akizungumza na gazeti hili, Jembe Ulaya ambaye ana leseni C ya ukocha ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), alisema wachezaji wanaokuja Tanzania mawakala wanachukua asilimia kumi kwao ndio maana wengi viwango vyao ni vya kubahatisha.

“Mchezaji mzuri hawezi kumpa wakala asilimia kumi kwa sababu anajiamini ana uwezo ila kuna wachezaji wanaitwa wa kimataifa wanakaa benchi kwa kuzidiwa na wazawa,” alisema Jembe Ulaya.

Pia alisifu kiwango cha Donald Ngoma wa Yanga na kusema ni mchezaji unayeweza kusema wa kimataifa na mtu asiwe na maswali.

Jembe Ulaya ambaye aliwahi kuchezea timu za Yanga na Sigara alisema yupo tayari kutumika kama kocha hivyo timu yoyote itakayomhitaji iwe ya daraja la pili, daraja la kwanza na hata Ligi Kuu yupo tayari kuifundisha.

“Nina leseni C ambayo inaniruhusu kufundisha soka kwenye daraja lolote hata kuwa kocha msaidizi wa timu za Ligi Kuu hivyo najiweka sokoni, nipo tayari kufundisha popote Tanzania,” alisema.