Ligi ya Wanawake hakuna kulala

LIGI Kuu ya soka ya wanawake inatarajiwa kuendelea leo, kwa viwanja sita kuwaka moto katika miji tofauti.

Ligi hiyo ambayo ipo kwenye makundi mawili yenye timu sita kila moja, inaingia mzunguko wa saba na timu zote zitakuwa uwanjani kusaka pointi tatu.

JKT Queens itakuwa ugenini kwenye uwanja wa Nangwanda dhidi ya Viva Queens na kocha wa JKT, Robert Ngoliga aliliambia gazeti hili kwamba wanakwenda kwa tahadhari kwenye mechi hiyo kwani wanafahamu kila timu imejiandaa vizuri.

“Mchezo uliopita tulifungwa na Mlandizi na kuvuruga hesabu zetu, hivyo mchezo na Viva Queens tumejiandaa kuondoka na pointi tatu kwani tupo sawa na Mlandizi ila tumewazidi kwa mabao ya kufunga na kufungwa,” alisema Ngoliga.

JKT Queens ambayo inaongoza kundi A ikiwa na pointi 13 baada ya kucheza michezo sita inafuatiwa na Mlandizi Queens yenye pointi 13 pia.

Mlandizi leo itakuwa mwenyeji wa Evergreen yenye pointi tisa mchezo utakaochezwa Uwanja wa Mabatini, Pwani.

Mburahati Queens yenye pointi tano itakuwa mwenyeji wa Fair Play ya Tanga ambayo ina pointi tisa mchezo utakaochezwa Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Kundi B vinara Sisters FC yenye pointi 18 itaialika Victoria Queens yenye pointi nne mchezo utakaochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Baobab ambayo inashika mkia kwenye kundi B ikiwa na pointi mbili itaialika Majengo ya Singida kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na Panama ya Iringa yenye pointi tano itakuwa mwenyeji wa Marsh Athletes kwenye Uwanja wa Samora Iringa.