Azam yaajiri kocha Mromania

KLABU ya soka ya Azam imemtangaza Mromania Aristica Cioaba (45) kuwa kocha mkuu akichukua nafasi ya Mhispania Zeben Hernandez ambaye mkataba wake ulisitishwa.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Saad Kawemba alisema Cioaba atasaidiwa na Idd Cheche na kocha wa makipa Idd Abubakar.

Tangu kuondoka kwa Hernandez Cheche na Abubakar ndio waliiongoza timu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ambapo jana ilitarajiwa kucheza mechi ya nusu fainali na Taifa Jang’ombe. Kawemba alisema wamesaini mkataba wa miezi sita na kocha huyo na kwamba wataongeza baada ya kuridhishwa na huduma yake.

“Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC inapenda kuwataarifu wadau wote wa mpira na wapenzi na mashabiki wa Azam kwamba klabu imempata mwalimu, ambaye ndiye ataiongoza kwa kipindi hiki hadi mwishoni mwa msimu... “Kwa hiyo kwa mashabiki wetu maana yake ni kwamba tukiingia kwenye mechi inayofuata ya ligi, kocha atakuwa ameanza kazi na Cheche (Idd) atakuwa msaidizi wake na benchi lake zima alilokuwa nalo hivi sasa litaendelea,” alisema.

Kawemba alisema tayari kocha huyo mpya ameshakwenda Zanzibar kuungana na timu ambapo atakuwa akiifuatilia na kutoa ushauri panapohitajia.

“Kazi ataanza rasmi baada ya vibali vyake kwa kazi na kuishi nchini vitakapokamilika,” alisema.

Kwa upande wa kocha Cioaba ameahidi kuifanyia makubwa timu hiyo.

“Najua Azam FC hapa Tanzania ni moja ya timu kubwa yenye historia huko nyuma, napenda kuushukuru uongozi kwa kuniamini na kunipa nafasi kuja kufundisha soka kwenye nchi hii, kwa mashabiki napenda kuwaambia kuwa nalijua soka la Afrika, nimewahi kufundisha Ghana na kupata matokeo mazuri… Msimu uliopita, Cioaba aliiongoza Aduana Stars ya Ghana kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Ghana.

Kocha huyo anafahamiana na nyota wawili wa Azam FC, Yakubu Mohammed na Yahaya Mohammed, waliosajiliwa kutoka Aduana katika usajili wa dirisha dogo.

Mbali na kufundisha soka Ghana pia amewahi kufanya kazi Raja Casablanca ya Morocco, Al Masry ya Misri na timu mbalimbali katika nchi za Romania, Kuwait, Oman na Jordan.