16 zathibitisha Ligi ya Kikapu Dar

TIMU 16 za mchezo wa kikapu zimethibitisha kushiriki ligi ya mkoa wa Dar es Salaam (RBA) itakayoanza kutimua vumbi Januari 28 kwenye uwanja wa ndani wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana Mwenyekiti wa chama cha kikapu Dar es Salaam, Okare Emesu alisema kati ya timu 16, nane ni za wanawake na kwamba ligi hiyo itachezwa kwa mfumo wa nyumbani na ugenini katika hatua za awali na timu nane za juu za wanaume zitacheza mtoano hadi kupata bingwa.

“Viongozi wamekuja na mikakati ili kuleta chachu kwani kutakuwa na ligi ya watoto chini ya umri wa miaka 14, ligi ya daraja la kwanza, ligi ya vyuo, ligi ya mashirika, ligi ya mashule, program maalumu kwa ajili ya kukuza vipaji kwa mpira wa kikapu nchini,” alisema Emesu.

Pia Emesu alisema leo watafanya maonesho ya awali ya ligi ya RBA itakavyokuwa kwenye viwanja vya mpira wa kikapu vya Gymkhana hivyo wanakaribisha wadau kuona mfano wa ligi ya RBA.

Timu zinazotarajiwa kushiriki kwa upande wa wanaume ni JKT, Mgulani, Ukonga Kings, Magereza, Savio, Pazi, DB Youngstars, Magnet, ABC, Mabibo Bullets, Outsiders, Kurasini heat, Oilers, Vijana, Chui na Jogoo.

Timu za wanawake ni JKT Stars, Jeshi Stars, Vijana Queens, Don Bosco Lioness, Ukonga Queens, Kurasini Divas na Oilers Princess.