Mwenyekiti ARFA apania makubwa

MWENYEKITI mpya wa Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA) Peter Temu, amesema moja ya mikakati yake ni kushirikiana na wilaya za mkoa huo kuhakikisha soka linachezwa kote.

Akizungumza na gazeti hili, Temu alisema heshima ambayo wajumbe wamempa anaitumia vema kwa kuandaa mpango kazi wa kurejesha soka la mkoa huo kama ilivyokuwa zamani enzi za timu za Ndovu na AFC.

“Arusha ni aibu kukosa timu ya kucheza Ligi Kuu hivyo baada ya uchaguzi nataka nikutane na viongozi wa wilaya zote tuwekeane mikakati endelevu,” alisema Temu.

Pia Temu aliwasihi wadau wa soka wawe na matumaini kuwa mpira utarejea kulingana na safu mpya kwani ina morali ya kusaidia na kuendeleza mpira.

Uchaguzi wa ARFA ulifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita wilayani Monduli ambapo viongozi wake watakaa madarakani kwa miaka minne.

Katika uchaguzi huo, Temu alimshinda Omary Walii kwa kura 13 kwa 6, Katibu mkuu Zakayo Mjema alipapata kura 18.