`Uchovu uliiangusha Taifa Jang’ombe’

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Jang’ombe, Sheha Khamis amesema kuwa uchovu wa wachezaji wake ulichangia kushindwa katika mchezo wa nusu fainali wa michuano ya Kombe la Mapinduzi kati yake na Azam FC.

Mchezo huo ulipigwa kwenye Uwanja wa Amaan saa 10:00 jioni na Azam kufanikiwa kushinda kwa bao 1-0, ambalo lilifungwa na Frank Domayo, ambapo sasa itacheza na Simba katika fainali kesho Ijumaa.

Alisema kuwa timu yake ilionesha kiwango kizuri, lakini wachezaji wake walichoka sana kutokana na kutopumzika kabla ya kucheza mchezo uliofuata.

Alisema kuwa mashindano ni mazuri lakini ugumu wake ni kutokana na nmapumziko kuwa mafupi kietendo ambacho alikisemea kuwa kinaawachosha wachezaji.

Hivyo aliwataka waandaaji wa michuano hiyo kujipanga ili kutoa muda wa mapumziko kabla ya timu kurudi tena uwanjani.

“Waandaaji wajiandae vizuri kwa sababu huwezi kucheza siku moja na kupumzika siku moja inakuwa ngumu kwa kweli kwa wachezaji wao.”

Akizungumzia mchezo huo alisema kwamba alikuwa na wasiwasi mkubwa na Azam kwa vile wana viungo wazuri, wachezaji wazuri, uelewa mzuri, suala ambalo alizungumza tangu awali.