Yanga yapiga mtu mkono

WAWAKILISHI wa Tanzania Bara kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga jana walianza vema michuano hiyo baada ya kuifunga mabao 5-1 Ngaya de Mde ya Comoro katika mechi iliyochezwa mjini Moroni.

Kwa ushindi huo, Yanga imejiweka kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo kwani sasa matokeo yoyote yasiwe kufungwa zaidi ya mabao 3-0 katika mechi ya marudiano itakayochezwa mwishoni mwa wiki ijayo kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa habari kutoka Moroni, Yanga ilianza kufungua hesabu ya mabao katika dakika ya 43 kupitia kwa kiungo Mzambia, Justin Zulu, likiwa ni bao lake la kwanza Yanga tangu aliposajiliwa.

Dakika mbili baadaye, Simon Msuva aliiongezea Yanga bao la pili, matokeo yaliyowapeleka mpaka mapumziko.

Dakika ya 59, Obrey Chirwa aliifungia Yanga bao la tatu kabla Amisi Tambwe hajaongeza la nne dakika ya 65 na Thabani Kamusoko kufunga kitabu hicho cha mabao kwa kufunga bao la tano katika dakika ya 73.

Bao la kufutia machozi la Ngaya lilifungwa dakika ya 66 kupitia kwa mchezaji wake Said Mohammed.

Timu itakayovuka raundi hiyo itacheza na mshindi wa mechi kati ya Zesco ya Zambia na APR ya Rwanda.

Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Justin Zullu, Simoni Msuva/Emmanuel Martin, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe/Juma Mahadhi, Obrey Chirwa na Haruna Niyonzima/Said Juma ‘Makapu’.