Matumaini ya ubingwa yamerudi - Simba

KOCHA msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja amesema ushindi mkubwa waliopata dhidi ya Prisons ya Mbeya na kurudi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, umewapa tena mwanga wa kuwa mabingwa.

Mchezo huo umeifanya Simba kurejea kileleni kwa kufikisha pointi 51, juu ya Yanga yenye pointi 49 ikiwa na mchezo mmoja kibindoni.

Katika mchezo huo uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Simba ililipa kisasi kwa ushindi huo mnono baada ya kufungwa mabao 2-1 katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyofanyika uwanja wa Sokoine Mbeya.

Kabla ya mechi hiyo, Simba pia iliifunga Majimaji kwa mabao 3-0 kwenye uwanja wa Majimaji Songea.

Alisema hana budi kuwashukuru wachezaji wake ambao wameonesha jitihada na kushinda na kwamba idadi ya mabao mengi baadaye itawasaidia kuamua bingwa mpya wa ligi endapo timu zitafungana.

“Nawashukuru wachezaji wangu kwa kuonesha jitihada na kufunga.

Ni dhahiri sasa tunaona mwanga kwamba tutakuwa mabingwa kwa sababu tumerudi kileleni,” alisema.

Pia, aliongeza kuwa tayari wamewalipa Prisons mabao waliyowafunga katika mchezo wa raundi ya kwanza.

Kwa upande wake Kocha wa Prisons, Abdallah Mohamed alisema huenda uchovu wa safari na kubana kwa ratiba umechangia kikosi chake kushindwa kufanya vizuri.

Pia, alisema kumekuwa na makosa madogo kutoka kwa wachezaji wake ambayo atayafanyia kazi ili yasijirudie na kuahidi kufanya vizuri michezo ijayo kutimiza lengo lao la kushika nafasi ya nne.

Lakini pia, kocha Mohamed amelalamikia ratiba ya ligi kuwa inazibana baadhi ya timu na kusababisha kupoteza mechi.

“Timu ilikuwa na uchovu, tulicheza mechi Jumatano tukasafiri kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam bila kupumzika, hiyo ndio sababu ya kupoteza mchezo wakati Simba ilicheza na Majimaji mwishoni mwa wiki iliyopita,” alisema Mohamed.

Pia alisema kucheza mechi Mbeya halafu wanasafiri kucheza Jumamosi bila kupumzika inasababisha wachezaji kuchoka kwani wanatakiwa kurudi tena Mbeya kucheza na Kagera Sugar keshokutwa lakini akasema wanajiandaa na mapambano bado yanaendelea.