Ligi ya Wanawake yafika patamu

SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF) limetoa ratiba ya Ligi Kuu ya Wanawake hatua ya sita bora inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii.

Hatua hiyo ndio itakayotoa bingwa wa ligi hiyo inayochezwa kwa mara ya kwanza nchini. Kwa mujibu wa ratiba hiyo, timu zote zilizoingia hatua hiyo zitacheza kwenye kiwanja cha Karume ambapo kwa siku zitachezwa mechi mbili.

Timu zitakazofungua dimba Jumamosi ya wiki hii ni JKT Queens ya Ilala dhidi ya Mlandizi Queens ya Pwani zitakazocheza saa nane mchana. Mechi itakayofuata siku hiyo itaanza saa 10 jioni ambapo Fair Play ya Tanga itamenyana na timu ngumu ya Sisterz ya Kigoma.

Jumatatu ya Februari 20, Marsh Athletes ya Mwanza itamenyana na Panama ya Iringa saa nane mchana kabla Mlandizi haijavaana na Fair Play saa 10 jioni.

Sisterz itarudi tena uwanjani Februari 22 kumenyana na Marsh saa nane mchana kabla Panama haijacheza na JKT Queens.

Februari 24 mechi ya kwanza itakuwa kati ya Fair Play na JKT Queens, kabla ya Marsh kumenyana na Mlandizi.

Panama itacheza na Sisterz Februari 26 na siku hiyo pia kutakuwa na mechi kati ya JKT na Marsh.

Sisterz itarudi tena uwanjani Februari 28 kucheza na Mlandizi kabla Panama haijacheza na Fair Play siku hiyo hiyo.

Machi mbili Marsh itacheza na Fair Play na Mlandizi itacheza na Panama na siku inayofuata Sisterz itacheza na JKT, katika mechi inayotarajiwa kuwa ya vuta nikuvute kutokana na timu zote hizo kusheheni wachezaji wa timu za taifa za Twiga Stars na ile ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Tanzanite.

Ligi hiyo ilianza kwa kushirikisha timu 12 zilizogawanywa kwenye makundi mawili yenye timu sita kila moja.

Timu zilizoishia hatua ya makundi ni Evergreen Queens ya Temeke, Mburahati ya Kinondoni, Majengo ya Singida, Baobab ya Dodoma, Viva Queens ya Mtwara na Victoria Queens ya Kagera.