Makocha wa kikapu wakwama
- Imeandikwa tarehe 22 Septemba 2012
- By Mwandishi Wetu
- Imesomwa mara: 133
MAKOCHA wapya wa timu ya Taifa ya mpira wa kikapu kutoka Marekani waliokuwa wawasili jana wameshindwa kufanya hivyo.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Phares Magessa ilieleza kuwa siku watakayofika makocha hao itatangazwa.
Makocha ni Albert Sokaitis ambaye atakuwa Kocha Mkuu na msaidizi wake Jocquis L. Sconiers ambao ilikuwa wafike jana kuanza mafunzo kwa timu za Taifa za wanaume na wanawake.
“Kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu ujio huo umesogezwa mbele, tarahe mpya ya kuwasili itatangazwa baadaye mara baada ya kukamilisha taratibu husika,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza kuwa kambi ya timu hizo kwa wanaume na wanawake iliyokuwa ianze leo imeahirishwa hadi itakapotangazwa tena.
“Tunaomba radhi kwa usumbufu wote unaotokana na kusogezwa mbele kwa ujio huu wa makocha wa kigeni.
“Tunachukua nafasi kuwashukuru watu wa Marekani kupitia ubalozi wao wa Tanzania ambao ndio wamekuwa wa kwanza kuutikia wito wa kusaidia maandalizi ya timu zetu za Taifa kwa kuunga mkono jitihada za Rais Jakaya Kikwete katika kusaidia maendeleo ya michezo hususani mpira wa kikapu," alisema.


