Tenga aingilia sakata la Yondani
- Imeandikwa tarehe 09 Juni 2012
- By Mwandishi Wetu
- Imesomwa mara: 908
RAIS wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Leodegar Tenga ameagiza kufanyika uchunguzi jinsi mchezaji wa timu ya taifa, Kelvin Yondani alivyoondoka kambini usiku wa kuamkia Juni 7.
Tenga ameagiza hilo lifanyike baada ya kudaiwa kuwa Yondani ambaye amesaini mkataba na Yanga aliondoka kambini Stars, iliyopo hoteli ya Tansoma Kariakoo na kwenda kusaini mkataba huo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Simba iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, Tenga ameuandikia barua uongozi wa klabu hiyo na kuahidi kufanyika kwa uchunguzi na endapo itabainika kweli Yondani aliondoka kambini usiku, hatua kali zitachukuliwa kwa wote waliohusika.
Kwa takriban wiki sasa Simba imeingia kwenye mgogoro wa usajili na hasimu wake Yanga, baada ya Yanga kumsainisha Yondani mkataba huku Simba ikidai beki huyo ni mali yake kwa vile ana mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Simba iliyosainiwa na Ofisa habari wake Ezekiel Kamwaga, uongozi wa Simba umefurahishwa na kitendo hicho cha Tenga kuingilia kati suala hilo na kutafuta ukweli.
“Katika barua ambayo Tenga ameiandikia Simba, ameahidi kwamba uchunguzi utafanyika katika maeneo makuu mawili. Mosi, iwapo ni kweli Yondani aliondoka kambini usiku, pili iwapo aliondoka kwa ruhusa maalumu au alitoroka.
Tenga ameahidi kwamba kama ikibainika kwamba aliondoka bila ruhusa, basi hatua zitachukuliwa kwa wote waliohusika chini ya taratibu za maadili kwa wachezaji (Players Code of Conduct),” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Simba.
Aidha, taarifa hiyo iliongeza kuwa kutokana na kauli hiyo ya Tenga, uongozi wa Simba umeamua kutozungumza lolote kuhusiana na masuala ya Yondani.
“ Tayari timu imewasilisha vielelezo vyake TFF na kote kwingine ambako suala hilo linaweza kufika. Kilichobaki sasa ni kusubiri vyombo husika vifanye kazi yake,” ilisema taraifa hiyo.
“Simba SC inapenda kuchukua nafasi hii kuwaomba wapenzi na wanachama wake kutulia na kutobabaishwa na taarifa za wachezaji wake kusajiliwa na timu nyingine.
Kwa sasa Simba inaendelea na mikakati yake ya usajili unaokidhi vigezo vya kimataifa ambao ulisababisha msimu uliopita itwae ubingwa wa Tanzania na kuifunga Yanga goli 5-0”.
Taarifa hiyo iliendelea: “Simba si timu ya maneno mengi kwenye usajili, bali vitendo. Tunaomba wanachama wetu watulie na mara ifikapo tarehe 15 Juni mwaka huu, mbivu na mbichi zote zitajulikana.
Siku hiyo, Simba itatangaza wachezaji wake wote iliyowasajili na iliyowaacha”. “Simba ndiyo mabingwa wa Tanzania na mashabiki wake wanatakiwa kutembea vifua mbele popote pale walipo na wasichanganywe na taarifa za pembeni.
Uongozi wa Simba uko makini na unafanya kazi zake kisayansi,” ilisema taarifa hiyo.


