18Juni2013

 

Stars itaifunga Msumbiji- Kim

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Kim Poulsen amesema kuwa timu yake itashinda mechi yake ya marudiano ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika dhidi ya Msumbiji Jumapili hii.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana Kim alisema kuwa anaamini timu yake itaifunga Msumbiji na kusonga mbele kwenye hatua inayofuata ya mashindano ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika mwakani.

Alisema anafahamu Msumbiji wanaweza kuwa wazuri zaidi ya walivyokutana nao kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam ambapo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 lakini alisema kuwa anaamini timu yake imeiva kiasi cha kuwafunga Msumbiji nyumbani.

“Haitakuwa rahisi kuwafunga Msumbiji kwani wanacheza nyumbani, lakini naamini timu yangu kwa sasa ni nzuri na inaweza kushinda mchezo huo,”alisema Kim ambaye huo utakuwa mchezo wake wa tatu wa mashindano toka apewe jukumu la kuinoa timu hiyo mwezi uliopita.

Kim alisema kuwa wataenda Msumbiji kwa lengo moja tu la kushambulia na kupata mabao ili waibuke na ushindi katika mchezo huo na kuongeza kuwa tofauti na mechi iliyopita dhidi ya Gambia safari hii anaamini washambuliaji wake watafunga mabao kwenye mechi hiyo.

“Tunajua tunapaswa kwenda kule na kushambulia, na kama uliangalia mechi yetu iliyopita mabao yetu yalifungwa na mabeki, Shomari Kapombe na Erasto Nyoni, lakini mchezo huu wa Maputo tunahitaji kuona tukipata mabao yetu kupitia kwa washambuliaji wetu,” alisema Kim.

“Kwenye mechi iliyopita dhidi ya Msumbiji tulitoka sare ya 1-1, sasa tunaenda Maputo, tunacheza ugenini, tunajua itakuwa mechi ngumu lakini tunahitaji kushinda ili tusonge mbele, na naamini tutashinda,” alisema Kim.

Kim pia alimzungumzia mshambuliaji wa TP Mazembe Mbwana Samatta ambaye ana muda mrefu toka alipoifungia timu hiyo bao na kusema kuwa ni mchezaji mzuri lakini anapaswa kucheza kwa faida ya timu.

“Nilimwambia kuwa asipende kukaa na mpira kwa muda mrefu, anatakiwa kutoa pasi na kisha kuomba tena, ulimuona kwenye mechi iliyopita alikimbia na mpira kwa muda mrefu baadaye akachoka akapoteza,”alisema Kim, alionekana kutofurahishwa na aina ya uchezaji wa mshambuliaji huyo mwenye kipaji cha hali ya juu.

Kikosi cha wachezaji 18 cha Taifa Stars kitaondoka kesho kuelekea Msumbiji ambapo kinatarajia kucheza na timu ya taifa ya nchi hiyo kwenye Uwanja wa Machava Jumapili.

Kim alisema katika msafara huo yumo kiungo Nurdin Bakari na Thomasi Ulimwengu ambao walikuwa majeruhi lakini kwenye kikosi hicho hatokuwepo kipa namba moja wa Azam Mwadini Ally na beki Waziri Salim ambao ni majeruhi.

Faraja kwa kocha huyo ni kumaliza adhabu kwa beki wa kati wa timu hiyo Aggrey Moris ambaye alitolewa kwa kadi kwenye mchezo waliofungwa mabao 2-0 na Ivory Coast, uliochezwa Abidjani Juni 2.