Mwinyi mgeni rasmi tuzo za Taswa
- Imeandikwa tarehe 14 Juni 2012
- By Mwandishi Wetu
- Imesomwa mara: 376
RAIS mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaji Ali Hassan Mwinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za utoaji wa tuzo ya mwanamichezo bora wa mwaka wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Michezo nchini (TASWA) kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee leo usiku.
Akizungumza na waandishi wa habari katika mgahawa wa City Sport Lounge jana Katibu Mkuu wa TASWA Amiri Mhando alisema kuwa Mwinyi ‘Mzee Ruksa’ atapamba usiku wa tuzo hizo kwa kuwa mgeni wa heshima kwenye sherehe hizo.
Kwenye sherehe za utoaji wa tuzo hizo kwa mwaka jana Makamu wa Rais Dk. Mohamedi Gharibu Bilal alikuwa mgeni rasmi ambapo ilishuhudiwa Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu Benjamini Mkapa akikabidhiwa tuzo ya heshima ya chama hicho.
Alisema utoaji wa tuzo hizo utakaosindikizwa na bendi ya muziki wa dansi ya Extra Bongo zitafanyika kwenye ukumbi wa kawaida wa Diamond Jubilee na sio ukumbi wa watu maalumu kama ilivyofahamika awali.
Wanamichezo mbalimbali kutoka michezo tofauti tofauti watawania tuzo ya mwanamichezo bora wa mwaka wa TASWA ambapo kwa mwaka jana ilikwenda kwa mcheza netiboli Mwanaidi Hassani.
Miongoni mwa majina yanayowania tuzo hizo kwa upande wa soka ni mlinda mlango nambari moja nchini Juma Kaseja wa Simba, mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara msimu uliopita John Bocco wa Azam na beki wa kati wa Azam Aggrey Moris.
Wengine ni Shomari Kapombe wa Simba na Salumu Abubakari wa Azam wanaowania tuzo ya mwanasoka bora chipukizi, huku Mbwana Samatta wa TP Mazembe, Henry Joseph wa Konsivinger ya Norway na Sophia Mwasikili anayecheza soka Uturuki wakiwania tuzo ya mwanasoka bora wa Tanzania anayecheza nje ya nchi.
Wengine ni Emmanueli Okwi wa Simba, Haruna Niyonzima wa Yanga na Kipre Tche tche wa Azam wakiwania tuzo ya mwanasoka bora kutoka nje anayecheza soka Tanzania.


