Viingilio mechi ya Twiga vyatajwa
- Imeandikwa tarehe 14 Juni 2012
- By Mwandishi Wetu
- Imesomwa mara: 325
SHIRIKISHO la soka nchini (TFF) jana limetangaza viingilio vya mechi ya kimataifa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wanawake (AWC) kati Tanzania (Twiga Stars) na Ethiopia itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka TFF iliyosambazwa kwa vyombo vya habari jana, kiingilio cha chini katika mechi hiyo ni Sh 2,000. Viingilio vingine kwa mechi hiyo itakayoanza saa 10 kamili jioni ni Sh 5,000 kwa VIP B na C wakati VIP A itakuwa Sh 10,000.
Tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mechi kuanzia saa 3 asubuhi. Mechi hiyo ni muhimu kwa Twiga Stars kwani wanahitaji ushindi ili kufuzu michuano hiyo itakayofanyika Equatorial Guinea baadaye mwaka huu.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Adis Ababa, Twiga ilifungwa mabao 2-1, matokeo ambayo si mabaya sana kwa upande wake kwani ikishinda bao 1-0 itakuwa imefuzu.



