19Juni2013

 

TBL kudhamini mashindano ya pool kwa Sh milioni 60

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Safari Lager imetangaza kudhamini mashindano ya Taifa ya mchezo wa pool ambazo fainali zake zimepangwa kufanyika Mwanza baadaye mwaka huu.

 

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa Bia ya Safari,Oscar Shelukindo alisema kuwa, jumla ya Sh milioni 60 zitatumika kwa ajili ya zawadi kwa washindi wa mashindano hayo ambazo yanafahamika kama'Safari Lager National Pool Champion Ship 2012.

"Nia yetu ni ileile kuinua vipaji kwa vijana na kuwainua kiuchumi kwa kuzingatia michezo ni ajira, hivyo kwa mara ya tano mfululizo tunatangaza kudhamini mashindano ya taifa ya pool,"alisema Shelukindo.

Shelukindo alizitaja zawadi za washindi kwa ngazi za mkoa ni Sh 700,000 kwa bingwa,Sh 350,000 kwa mshindi wa pili,Sh 200,000 kwa mshindi wa tatu na Sh 100,000 kwa mshindi wa nne.

Alisema kuwa ,kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja wa kiume, bingwa ataondoka na kitita cha Sh 350,000, mshindi wa pili Sh 200,000,wakati bingwa kwa upande wa wanawake akiweka kibindoni Sh 250,000 na mshindi wa pili Sh 150,000.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Pool Tanzania(TAPA)Amos Kafwinga alisema kuwa katika kuyaboresha mashindano hayo na kuyafanya yawe na mvuto zaidi chama chake kimebadilisha mfumo wa uendeshaji kutoka kushirikisha mikoa na sasa klabu.

Mashindano hayo yamepangwa Juni 21 jijini Tanga kwa kushirikisha klabu kutoka mikoa 16 ikiwemo Manyara, Mbeya Dodoma, Mwanza, Kilimanjaro, Tabora, Kagera, Lindi, Temeke, Ilala, Kinondoni, Shinyanga, Iringa, Morogoro, Arusha na Tanga.