Simba yaionya Mtibwa Sugar

KOCHA msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja ameionya Mtibwa Sugar kwamba isidhani kesho itashinda katika mechi yao la Ligi Kuu itakayochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Simba kesho itakuwa mgeni wa Mtibwa Sugar baada ya kutoka kapa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ambapo ilifungwa bao 1-0 na Azam mjini Zanzibar.

“Kwa vile Azam imetufunga, wasidhani nao wanaweza kutufunga, mzunguko wa kwanza tuliwafunga na mzunguko huu pia tutawafunga,” alitamba kocha Mayanja.

Simba tayari ipo Morogoro tangu juzi ikifanya maandalizi ya mwisho kwa ajili ya mechi hiyo ambayo kama itashinda itaendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo. Wekundu hao wa Msimbazi kwa sasa wanaongoza ligi kwa pointi 44, huku Yanga ikimfuatia kwa pointi 40 katika nafasi ya pili.

Kocha ya Mayanja alisema anatambua ugumu wa mechi hiyo kwani hata wapinzani wao wako kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo, lakini uwezo wa kushinda tunao.

“Kikubwa ni kwamba wachezaji wetu wana mazoezi ya kutosha maana michuano ya kombe la Mapinduzi ni mazoezi tosha kwao ilikuwa hivyo naweza kusema wako vizuri zaidi ya Mtibwa Sugar,” alisema.

Simba inasaka ubingwa baada ya kuukosa kwa takriban mwaka wa nne sasa. Hata hivyo timu hiyo pamoja na uimara wake kwenye safu ya kiungo na beki, haijawa vizuri kwenye washambuliaji na hilo ndio huwa tatizo la kukosa mabao kwenye mechi zake.

Add a comment